Ndiyo maana makocha wengi huepuka kubadili makika mara kwa mara.
Timu yenye kipa bora, inakuwa na asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi kuliko ile yenye kipa 'uchochoro'
Kuna makipa wengi, lakini wachache zaidi ndiyo bora. Umakini na jinsi anavyoibeba timu, ndiyo kipa anavyohesabiwa kuwa ni bora.
Mwandishi wa makala haya amekusanya majina ya makipa waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inayoendelea nchini.
1. Vicent Angban-Simba
Kwa sasa ndiye kipa namba moja wa kikosi cha Simba. Kwa muda mrefu Simba ilikuwa na mapungufu makubwa kwenye lango tangu alipoondoka kipa wa kutegemewa, Juma Kaseja.
Pamoja na kusajili makipa wengi, lakini wanachama na mashabiki wa Simba walionekana kutoridishwa nao.
Hii yote inatokana na kuzoea kuwepo kwa makipa bora kabisa kwenye klabu hiyo. Klabu hiyo ina bahati ya kuwa na makipa wa aina hiyo.
Hata kipa wa mwisho kabla ya Angban, Peter Manyika bado hakuweza kukidhi haja ya Wanasimba.
Angban, raia ya Ivory Coast, ameonekana kushusha presha ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutokana na umakini wake mkubwa golini.
Urefu, uwezo wa kudaka mipira ya krosi, kupanga mabeki na kupunguza presha kwa mabeki wake pindi timu inaposhambuliwa kumemfanya kuwa kipenzi cha Wanasimba na kocha wao Jackson Mayanja.
Kwa kiasi kikubwa ameifanya Simba kuwepo hapo ilipo, kwa kuongoza ligi ikiwa na pointi 57.
2. Ally Mustapha 'Barthez'-Yanga
Hakuna ubishi ndiye kipa namba moja wa Yanga. Pamoja na kwamba kikosi hicho kuna wakati humtumia Deogratius Munishi 'Dida', lakini kwenye mechi ngumu inayohitaji matokeo kwa udi na uvumba kwa sasa 'Barthez' ndiye husimama golini.
Ni mmoja wa makipa bora kabisa hivi sasa nchini Tanzania. Yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa Taifa Stars.
Ana uwezo wa kuokoa michomo ambayo kila mmoja akiamini kuwa mpira utaingia wavuni.
Ni mzuri kwenye mipira ya krosi, kupanga mabeki, lakini kubwa zaidi ana 'taimingi' ya kuweza kung'amua na kukaa kwenye eneo sahihi wakati wa hatari golini kwake.
Idadi kubwa ya mechi alizocheza zimeifanya Yanga kukamata nafasi ya pili kwa pointi 53 ilizonazo kwenye Ligi Kuu hadi sasa.
3. Aishi Manula-Azam
Kipa huyu kinda anatabiriwa kuwa ndiye mrithi wa makipa bora kabisa nchini kuwahi kutokea kama kina Omari Mahadhi, Idd Pazi, Mohamed Mwameja 'Tanzania One', Rifat Said na wengineo.
Ingawa hana urefu kama kina Mwameja au Mambosasa, lakini ana uwezo mkubwa akiwa golini.
Tayari anaonekana kuwa ndiye kipa namba moja wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa sasa.
Mbali na kuwa mahiri kwenye kudaka, sifa nyingine ni uwezo mkubwa wa kuokoa penalti kama ilivyokuwa kwa Juma Kaseja na Mwameja.
Mpaka sasa kwenye mechi za Ligi Kuu ameokoa penalti tatu, akiwa kipa anayeongoza kwa kufuta penalti nyingi.
Umahiri wake golini umeifanya Azam kukamata nafasi ya tatu mpaka sasa kwenye mechi za Ligi Kuu ikiwa na pointi 52.
4. Deogratius Munishi 'Dida'-Yanga
Pamoja na kwamba hapangwei kwenye mechi nyingi za Yanga, lakini hakuna atakayepinga kuwa ni mmoja wa makipa wenye uwezo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ni kwa sababu tu kwenye nafasi ya golikipa ni lazima akae mmoja.
Ndiyo maana hata anapokaa golini hufanya kazi ile ile na vitu vile vile vinavyofanywa na mwenzake 'Barthez'.
Kama asingekuwa Yanga, nadhani angeweza kuwa kipa namba moja wa timu anayodakia.
Mara nyingi Yanga inamtumia pale 'Barthez' anapoonekana kuwa amechoka kwa kucheza mechi nyingi au kuwa mgonjwa.
Hata hivyo, ukiitazama Yanga inapocheza golini akiwa Dida, haina tofauti yoyote anapokaa 'Barthez'.
5. Beno Kakolanya-Prisons
Hapana shaka kuwa Tanzania imepata mmoja wa makipa bora kabisa msimu huu. Huyu ni Beno Kakolanya.
Ni mmoja wa walioifanya Prisons kutamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Ni mhimili mkubwa wa timu hiyo, kutokana na ustadi wake awapo golini pamoja na umbile lake lililokaa kikipa.
Kocha yoyote mzungu akitua nchini leo na kumkuta kipa huyo akiwa na Barthez, Dida pamoja na Manula na kuna mechi, Kakolanya atawekwa golini.
Urefu wake na umbile vinambeba mno kabla ya uwezo wake.
Yanga ilipata tabu ilipocheza na Prisons kutokana na uwezo wake mkubwa kabla ya kupata bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti na kuambulia sare ya mabao 2-2.
Mashabiki wa Simba wanamkumbuka walipotaka kuangua vilio Uwanja wa Taifa alipookoa michomo mikali ya kina Danny Lyanga, Ibrahim Ajibu na Hamisi Kiiza, tena kwa ustadi na mbwembwe juu dhidi ya Prisons, kabla ya bao la dakika tatu kabla ya mechi kumalizika la Awadh Juma.
Kuna taarifa kuwa Simba inamuwinda kipa huyo kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Ameifanya mpaka sasa Prisons kukamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 40.
6. Said Mohammed-Mtibwa Sugar
Huwezi kutaja makipa bora msimu huu bila kumtaja Said Mohamed wa Mtibwa Sugar.
Ndiye kipa wa kutegemewa kwa sasa wa Mtibwa, akimuweka benchi aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Hussein Sharrif 'Casillas' ambaye amerejea kutoka Simba.
Pamoja na kwamba haipo kwenye mbio za ubingwa, lakini Mtibwa Sugar imekuwa moja kati ya timu ngumu mno kwenye Ligi Kuu na zisizofungika kirahisi.
Haya yote yana mkono wa Said. Imeifanya timu hiyo kukamata nafasi ya nne nyuma ya Simba, Yanga na Azam, ikiwa na pointi 42.










