Majipu ya Zanzibar haya hapa

10Apr 2016
Mwinyi Sadallah
Nipashe Jumapili
Majipu ya Zanzibar haya hapa

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ya awamu ya saba imekamilisha kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi Rais wa Ali Mohamed Shein, huku rushwa, ufisadi, kukosekana usalama na uwajibikaji duni vikibakia kuwa majipu sugu Visiwani hapa.

Rais wa zanzibar dk ali mohamed shein

Matumaini ya wananchi ya kuondokana na matatizo hayo yalianza kufufuka baada ya iliyokuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kutunga sheria mbili ikiwamo ya kuanzisha mamlaka ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi na ile ya maadili ya Viongozi Zanzibar.

Pamoja na kutungwa kwa sheria hakuna tija inayoonekana kutokana na rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, uwajibika duni kuendelea kuwa saratani inayoitafuna Zanzibar.

Hata hivyo, waliokuwa wajumbe wa Baraza la nane la Wawakilishi Zanzibar (BLW), watakumbukwa kwa kazi waliyofanya ya kusimamia SMZ katika kipindi cha miaka mitano lakini SUK ilishindwa kufanyia kazi ripoti nyingi za uchunguzi za kamati teule za chombo hicho.

Kama ripoti hizo zingefanyiwakazi na hatua kuchukuliwa mafisadi na wabadhorofu wa madaraka na mali za umma na wasiowajibika wakichukuliwa hatua na lengo la kuimarisha misingi na utawala bora lingefikiwa katika kipindi hicho.

Bahati mbaya ripoti za ufisadi wa ardhi, kuuzwa majengo ya umma kwa manufaa binafsi, mali za serikali kukodishwa kwa bei chee kinyume na sheria ya manunuzi pamoja na ubadhirifu kupitia mishahara hewa havikuguswa.

Ripoti za uchunguzi za vitendo kama hivyo katika Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), pamoja na Baraza la Manispaa hazijatatuliwa na hakuna watu waliochukuliwa hatua za kisheria.

Wakati upepo wa Zanzibar kuhusu mwelekeo wa serikali baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa marudio ni kupambana na rushwa, ufisadi, uwajibikaji duni, ukwepaji na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija ni wakati wa kudhibiti maovu hayo kwa vitendo.

Kama serikali haitadhibiti mianya ya ukwepaji na misamaha ya kodi pamoja na biashara za magendo ya mafuta na ongezeko la bandari bubu, SMZ haitaweza kuongeza mapato na kuondoa kero za wananchi kwa kuwapatia huduma bora.

Hatua ya Rais Mohamed Shein ya kutangaza mwelekeo wa serikali na kuonyesha kuwa anataka kupambana na rushwa, ufisadi na uwajibikaji duni akiahidi kutumbua majipu, atafanikiwa kama vyombo vya kusimamia sheria vitatekeleza wajibu wake.

Rais anasema: “Katika kipindi hiki, nitahakikisha Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inafanya kazi ipasavyo ili wote waliotajwa katika sheria hiyop watagaze mali zao kwa mujibu wa sheria na kila kiongozi atatakiwa kuwajibika kikamilifu.”

Hatua ya wananchi kufichua rushwa na ufisadi pamoja na viongozi wazembe na wasiowaadilifu ni njia pekee ya kufanikisha malengo ya Rais ya kuimarisha misingi ya utawala bora katika serikali yake.

Ni jambo la kushagaza kuona mamlaka za kusimamia sheria ikiwamo ya kupambana rushwa na ufisadi zimekosa meno huku vitendo vya ubadhirifu vikiendelea kushika kasi licha ya kulalamikiwa na Wawakilishi Zanzibar.

Ripoti za uchunguzi kutokufanyiwa kazi zikiwamo taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikiali (CAG) ni kwenda kinyume na misingi ya utawala bora.

Serikali inayochukia vitendo vya rushwa na ufisadi ndiyo yenye uwezo wa kuleta maisha bora kwa wananchi, lakini kushamiri kwa rushwa na ufisadi kunaimaliza ndoto ya maisha bora kwa Wazanzibari wanyoge.

Zanzibar ina uwezo wa kujenga uchumi imara wa kujitegemea na kufanikiwa kutoa huduma bora kwa wananchi kama viongozi na watendaji wakuu watatumia uadilifu unaoendelea kuonyeshwa na Rais kama dira ya kuleta mabadiliko ya maisha bora kwa wananchi.

Wakati umefika kwa urasimu kuondolewa katika sekta ya uwekezaji ili kuongeza vyanzo vya mapato kutoka kwenye mafuta, gesi, uvuvi wa bahari kuu pamoja na uwekezaji katika sekta ya utalii, kilimo cha mwani na karafuu.

Bila ya kuimarishwa kwa uzalishaji wa ndani katika sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji na viwanda vya vidogo na vya kati, Zanzibar itaendelea kubaki hoi.

Hatua ya soko la utalii kuendelea kutegemea bidhaa mazao ya kilimo na ufugaji kutoka nje ya Zanzibar ni kasoro kubwa katika malengo ya kujenga uchumi imara wa taifa hili ambalo ni tajiri wa vivutio vya kitalii vya kipekee duniani.

Hakuna njia ya kukabiliana na vikwazo vya misaada ya wahisani zaidi ya kuongeza uzalishaji wa ndani pamoja na kupunguza matumizi yasiokuwa ya lazima zikiwemo safari za nje pamoja na semina na makogamano mambo yanayosheheni kulipana posho tena fedha za kigeni.

Wakati wa uchumi wa kutumikia siasa umepitwa na wakati uamuzi wa Rais Rais John Magufuli , kufuta sherehe za kitaifa na gharama zake kutumika kwa shughuli za maendeleo ni mfano kwa Zanzibar katika kufikia malengo ya kujenga uchumi imara na kuwapatia wananchi maskini huduma bora za kijamii.
Mwisho