Simba imlipe Kerr aondoke

16Jan 2016
Mhariri
Nipashe
Simba imlipe Kerr aondoke

Desturi ya kutimua makocha imeendelea Simba baada ya mwanzoni mwa wiki hii uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi kutangaza kuuvunja rasmi mkataba wa mwaka mmoja na kocha Dylan Kerr.

Muingereza huyo amekuwa kocha mkuu wa 21 kufungashiwa virago na mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara tangu mwaka 1998 'vurugu' za kufukuza ovyo makocha zilipoanza Msimbazi.

Kerr (48), Muingereza wa pili kuzinoa Simba na Yanga tangu 1997 Steve McLennan alipofundisha Jangwani, amefungashiwa virago baada ya kukaa Msimbazi kwa miezi sita alipochukua mikoba ya Mserbia Goran Kopunovic Julai mwaka jana.

Uongozi mpya wa Simba umeonekana kukosa uvumilivu kwa makocha unaowaajiri kwani Kerr ni kocha mkuu wa nne kutodumu Msimbazi tangu Rais Evans Aveva aingie madarakani Juni 29, 2014.

Kerr alitanguliwa na makocha wa kigeni Zdravko Logarusic kutoka Croatia, Mzambia Patrick Phiri na Mserbia Goran Kopunovic.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe hatuungi mkono utaratibu huu wa uongozi wa Simba kutimua makocha unaowaajiri pasi na sababu kuntu.

Hatukubaliani na uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kwa sababu mkataba wa Kerr umekatishwa akiwa ameiongoza Simba katika mechi 13 za Ligi Kuu akishinda nane, sare tatu na kupoteza mbili kwenye nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo kubwa zaidi nchini.

Nipashe pia hutuungi mkono kitendo cha uongozi wa klabu hiyo 'kumkalisha' Kerr nchini kusubiri malipo ya mishahara yake ilhali tayari umeshatangaza na umeshamkabidhi barua ya kuvunja mkataba wake.

Gazeti hili liliripoti jana kuwa kocha huyo anaidai Simba Sh. milioni 21.3, ikiwa ni mishahara yake ya miezi miwili Desemba na Januari kutokana na uamuzi wa klabu hiyo kuvunja mkataba wake na beki huyo za zamani wa klabu za Leeds na Reading za England.

Tunafahamu uongozi wa klabu hiyo umekuwa na rekodi mbaya ya kuchelewesha malipo ya kuvunja kwa mikataba na makocha inayowaajiri kiasi cha kushtakiwa na kufikishwa mbele ya mamlaka za soka.

Nipashe tunaamini uongozi wa Simba ulijiandaa kikamilifu kuachana na Kerr kabla ya kutangaza uamuzi huo na kumkabidhi barua ya kukatisha mkataba wake, hivyo hatuoni sababu za kocha huyo kutolipwa stahiki zake haraka ili arejee kwao.

Shime, viongozi wa Simba wanapaswa kumlipa Kerr stahiki zake ili aendelee na maisha mengine baada ya kumtema.