Maelezo ya kutosha yanahitajika utekelezaji wa sera ya elimu bure

15Jan 2016
Nipashe
Maelezo ya kutosha yanahitajika utekelezaji wa sera ya elimu bure

MOJA ya ahadi kubwa za Rais Dk. John Magufuli ilikuwa kutoa bure kuanzia elimu ya msingi hadi ya sekondari.

Rais Dk.John Magufuli (kushoto) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia)

Ahadi hii aliinadi wakati wa kampeni zake za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi watakuwa wanasubiri utekelezaji wake.

Kipindi hiki ndicho wazazi wengi wanahangaika kupeleka watoto wao kujiunga na darasa la kwanza.

Hata hivyo, kumetokea mkanganyiko wa utekelezaji wa sera hiyo ya elimu bure.

Suala la elimu bure ni kati ya ahadi kubwa za Rais Magufuli.

Hata hivyo, kuna tatizo limejitokeza la wazazi kutoelewa majukumu yao na yale ya serikali katika utekelezaji wa sera hii.

Kutokana na hali hiyo, kumeanza kujitokeza hali ya mkanganyiko huku baadhi ya wazazi wakiamini kuwa elimu bure maana yake serikali itatoa kila kitu kwa wanafunzi.

Matokeo yake kumeanza kuzuka malalamiko ya baadhi ya wazazi kushindwa kupeleka wanafunzi kwa madai kuwa bado wanatozwa michango.

Serikali inapaswa kuwaelimisha wananchi wafahamu majukumu yake katika utekelezaji wa sera hii.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na serikali, unaonyesha kuwa wajibu wake ni kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara.

Pia kununua samani yakiwamo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo, kujenga na kukarabati miundombinu ya shule na kutoa ruzuku kwa kila mwanafunzi.

Majukumu kwa wazazi ni kununua sare za shule, madaftari, kalamu, chakula kwa wanafunzi wa kutwa, matibabu, nauli, magodoro, shuka na vifaa vya usafi.

Tungependa kuona ahadi ya Rais inatekelezwa kwa vitendo, lakini pia wananchi wakielewa vizuri mchango wao katika utekelezaji wa sera ya utoaji elimu bure.

Pia pamoja na utekelezaji wa sera hiyo, lakini kuna haja ya serikali kuboresha mazingira ya shule zake.

Hakuna mazingira mazuri ya mtoto kufaulu wala kuishi kwenye shule zake na matokeo yake wazazi wengi wameelekeza nguvu zao kusomesha watoto wao kwenye shule za binafsi.

Katika miaka ya nyuma, lilikuwa jambo la fahari kwa mtoto kujiunga na shule za serikali, lakini katika miaka ya karibuni hali imekuwa tofauti.

Ushahidi ulio wazi ni jinsi wanafunzi wa shule binafsi wanavyofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

Watendaji wenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu nchini wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaboresha mazingira ya utoaji wa elimu ya shule za serikali.

Serikali ya awamu ya nne ilikuja na mpango kamambe wa kujenga shule katika kila kata.

Ni kweli shule zilijengwa kwa kasi, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa shule zenyewe zina matatizo makubwa kama yale ya uhaba wa walimu na zana za kufundishia.

Kutokana na mazingira duni ya shule; nyingi za serikali kulichochea baadhi ya wakuu wa shule kuanzisha michango mbalimbali.

Tunaomba wakuu wa shule watumie vizuri fedha zinatolewa na serikali, lakini pia ziendane na hatua madhubuti ya kuboresha mazingira ya shule hizo.

Bahati nzuri Rais Magufuli amerudia mara kadhaa kuwa suala la elimu bure linawezekana na amelisisitiza hata baada ya kuchaguliwa.

Ndiyo maana tunatoa wito wa serikali kuwabana wakuu wa shule ili kuhakikisha ahadi ya elimu bure inatekelezwa kwa vitendo, lakini pia mazingira ya utoaji elimu katika shule za serikali yanaboreshwa.