Uteuzi huo ulifanywa muda mfupi baada ya straika huyo matata wa klabu ya TP Mazembe ya DR Congo kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika Anayecheza barani.
Uamuzi huo wa benchi la ufundi la Taifa Stars umeonekana mchungu kwa aliyekuwa nahodha, Nadir Haroub, maarufu kama Cannavaro, ambaye ametangaza kujiuzulu kuichezea timu hiyo, kwa madai kuwa hajafurahishwa na jinsi uteuzi nafasi hiyo kwenda kwa mshambuliaji, Samatta.
Katika maelezo yake, Haroub amesema hakufurahishwa na kitendo cha kupokwa unahodha bila ya taarifa rasmi huku akiwa ameitumikia Stars kwa muda mrefu na kwa kiwango cha juu.
Tukiwa wadau namba moja ya michezo nchini, Nipashe tunaunga mkono uamuzi wa benchi la ufundi la Stars kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa wachezaji wa timu hiyo kutokana na sababu nyingi, kubwa ikiwa ni uwezo wa Samatta hadhi yake kimataifa.
Ingawa tunakubaliana na hoja ya Haroub ya kutopewa taarifa na benchi la ufundi juu ya mabadiliko hayo, tunaamini uteuzi wa Samatta umezingatia saikolojia ya mchezo wa soka -- straika huyo atatumika kuwapa motisha wachezaji wengine kutokana na mafanikio yake kisoka.
Duniani kote, mchezaji mwenye kiwango kikubwa anapewa unahodha wa timu ya Taifa. Lionel Messi (Argentina), Neymar (Brazil) na Wayne Rooney (England) ni mifano michache tu.
Kama ilivyo kwa wakali hao wa soka duniani, tunaamini Samatta atakuwa kiongozi mzuri na anayesikilizwa na wachezaji wote wa Taifa Stars kutokana na kuwa na mafanikio makubwa kisoka.
Mbali na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika, Samatta ni Mfungaji Bora wa Klabu Bingwa Afrika 2015. Na Haroub anapaswa kulitambua hili. Tunaamini benchi la ufundi la Stars halijafanya makosa kumpa kitambaa cha uongozi wa timu hiyo.
Nipashe tunaamini hakuna sababu kuntu za Haroub na wadau wengine wa soka kuendelea kujadili juu ya uteuzi huo kwa sababu umefanywa na mamlaka sahihi na katika muda mwafaka.
Ni imani yetu kuwa kukuzwa kwa mjadala huu kutasababisha mpasuko usio wa lazima ndani ya kikosi cha Taifa Stars, hivyo kuiathiri timu hiyo ambayo imeshindwa kufanya la maana tangu 1980 ilipotinga kwa mara ya kwanza fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika.
Badala ya kukimbilia kuwalaumu makocha wa Stars, Nipashe tunafikiri ipo haja kwa Haroub na wadau wengine wa soka kutathamini mafanikio ya Samatta.
Ni rai yetu kwa wadau wa soka nchini kuheshimu uamuzi wa makocha wa Taifa Stars ambao tunaamini hawajakurupuka katika kufanya uteuzi wa nahodha mpya wa timu hiyo.
------------------
Majadala wa nahodha Taifa Stars hauna tija
18Jan 2016
Mhariri
Nipashe
Majadala wa nahodha Taifa Stars hauna tija
MWISHINO mwa wiki iliyopita benchi la ufundi la Taifa Stars lilifanya mabadiliko katika uongozi wa timu hiyo ya Taifa ya soka likimteua mshambuliaji Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya.
Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta akipambana na Kolo Abib Touré wa Cote d'Ivoire










