Kuna mshabiki mmoja aliwahi kuagiza idadi ya tarakimu alizokokotoa kuhusu pai ipambe kaburi lake. Nafurahi pia kusikia wako washabiki wa pai hapa nchini na sehemu mbalimbali duniani. Tuendele kuienzi.
Pai ni namba katika hisabati ambayo imewavutia watu wengi kuitumia hata kuichambua na pia kuichakata. Wako wale wanaoikokotoa kupata thamani sahihi zaidi.
Kwa mfano, wako ambao wameikokotoa kwa nafasi milioni za desimali, na bado wanaendelea. Mjapani aitwaye Dk Kanada ndiye kwa sasa anashikilia rekodi ya tarakimu nyingi.
Baadhi ya watu wanahoji kwa nini wanafanya hivyo. Kwanza wanataka kuweka rekodi ya nani amewahi kufanya hivyo kwa idadi kubwa, na pili wanatafuta kama inamuundo fulani.
Wangependa kugundua kama inajirudia mahali fulani ili iundiwe kanuni. Historia inatuambia kuna mshabiki mmoja aliyeagiza kwamba akifa, kaburi lake lipambwe kwa tarakimu alizoweza kupata wakati wa kukokotoa pai. Huyu shabiki aliyekuwa mfalme, alikuwa na mapenzi makubwa na pai,
Inawezekana kuwa wewe hujaisikia pai au hujaielewa vizuri. Pai ni hisa inayopatikana ukigawanya mzingo wa duara kwa kipenyo chake. Mzingo ni urefu wa kuzunguka duara mara moja, wengine huuita mduara.
Kipenyo ni urefu kuanzia kwenye nukta moja ya duara kwenda nukta nyingine ya duara kwa kupitia kwenye kitovu kwa mstari mnyofu. Unaweza kutumia uzi au kamba kupata mzingo wa duara wa kifaa chochote chenye umbo la duara.
Pia unaweza kupata kipenyo kwa kupima urefu huo kwa rula. Ukitumia vifaa vingi na kutafuta wastani wa hisa unaweza kupata thamani ya pai inayokaribia 3.14.
Pengine unajua fasili hiyo lakini hujaihusisha na kile ulichofundishwa shuleni. Huenda walimu wako walikukaririsha kanuni zihusianazo na pai. Huenda ulikariri kwa kuogopa kukaripiwa na mwalimu au kuadhibiwa.
Hebu sahau hayo machungu na ifanye pai rafiki yako sasa. Kutokana na fasili : Mduara (M)/kipenyo(K)=pai(π), tunaweza kuandika M=πK kwa kuzidisha kila upande kwa K. Unaona, sio lazima kukariri.
Unaweza sasa kufuata malekezo ya vitendo kupata kanuni za kutafuta eneo la duara, eneo la mcheduara uliofungwa pande zote au upande mmoja, eneo la uso mviringo wa mcheduara, ukubwa wa tufe na hata ukubwa wa pia. Jaribu uone jinsi vitendo hivyo vinavyosisimua.
Pengine ulikuwa unafikiri pai iko shuleni tu. Ukweli ni kwamba pai iko popote. Kwanza iko majumbani mwetu kwa sababu vyombo vingi vina umbo la duara. Urembo wa majumba na hata bustani zinatumia duara.
Uundaji wa vitu hivyo na mapambo hayo huhitaji gharama ambapo ni pamoja na kujua eneo au ukubwa.Kwa mfano, fundi seremala anayetaka kutengeneza meza ya mviringo lazima ajue ni eneo gani anahitaji ili anunue mbao kiasi kinachohitajika na akwepe gharama zisizokuwa za lazima.
Ujenzi wa mashimoduara ya kuchuja maji huhitaji eneo na ukubwa kwa hiyo ukokotoaji unafanyika.
Pai ipo viwandani kwa uzalishaji wa bidhaa za umbo la duara.
Pai imeendelea kuwa sisimko kwa watu wengi duniani kote. Mwaka 1988 Mmarekani mmoja huko San Fransisco alipendekeza kuwe na siku ya pai ili kuimarisha msisimko huo. Wazo lilikubaliwa.
Hapa Tanzania wazo hilo lilanza kutekelezwa mwaka 2004. Hata hivyo kasi ya kuisherehekea siku hiyo imekuwa ndogo.
Baadhi ya watu wanahoji kwa nini pai ipewe siku yake wakati ziko namba nyingi maalumu za Hisabati. Ukweli ni kwamba pai ni namba inayoanza kufundishwa katika ngazi ya msingi na kuendelea hadi elimu ya juu. Ni namba pekee.
Siku ya pai inatumika sasa kwa kuwakutanisha wadau wa hisabati wakiwepo wanafunzi, walimu, wahadhiri, wakuza mitaala na viongozi kuhamasisha hisabati hapa nchini. Ukiona wanakujia kwa msaada wa hali na mali wapokee.
Wana uchungu na kudorora kwa somo la hisabati la hisabati. Wamechoka kusikia kuwa somo la Hisabati limeongoza katika kufeli. Wanataka Siku ya Pai ifanane fanane na ile ya Wapendanao (Valentine Day). Wanataka kukushirikisha uwaunge mkono katika juhudi za kuboresha hisabati. Naamini umehamasika.










