Uhakiki watumishi wa umma uwe endelevu

01Apr 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Uhakiki watumishi wa umma uwe endelevu

UHAKIKI wa watumishi wa umma uliofanywa katika mikoa yote nchini umebaini kuwapo kwa zaidi ya watumishi hewa1,850 katika idara na taasisi za serikali na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya Shilingi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, watumishi hewa ambao hadi juzi walikuwa wamebainika katika ukakiki huo ni 1,855 ambao taarifa za awali zinaonyesha kuwa katika nyakati tofauti wamelipwa Sh. 3,562,670,000.

Taarifa ya Waziri Simbachawene inaonyesha kuwa mikoa ya Mwanza, Arusha na Singida inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa, huku Mkoa wa Mwanza ukitajwa kuwa kinara kwa kuwa na watumishi hewa 334 na kufuatiwa na mikoa ya Arusha 270 na Singida 202.

Mikoa mingine ni Kigoma (171), Kilimanjaro (111), Dodoma (101), Morogoro (122), Mara (94), Mbeya na mkoa mpya wa Songwe (98), Dar es Salaam (73), Pwani (150), Ruvuma (37), Njombe (34) na Rukwa (180), Simiyu (33), Tabora (48), Tanga (24), Lindi (57), Kagera (14), Geita (4) na Manyara (watano).

Kwa mujibu wa wakuu wa mikoa yote nchini waliokuwapo jijini Dar es Salaam wakati Waziri Simbachawene alipokuwa anawasilisha taarifa hiyo, watumishi hewa waliobainika ambao wamekuwa wakilipwa mishahara ni walimu na madaktari ambao ni marehemu na wastaafu.

Kugundulika kwa watumishi hao hewa ambao wamekuwa wakiigharimu serikali mamilioni ya fedha, kumetokana na agizo alililitoa Rais John Magufuli, wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wampya Ikulu, jijini Dar es Salaam Machi 15, mwaka huu na kuwataka kusimamia uhakiki huo.

Hali hii inatisha na inatoa somo kwa serikali kwamba inalo jukumu kubwa la kukabiliana na vitendo vya hujuma vinavyofanywa na watumishi kadhaa ambavyo siyo kwamba vinaisababishia hasara bali pia kuiacha nchi na wananchi wake aktika umaskini.

Hatua inayopaswa kuchukuliwa haraka ni kuubaini mtandao mzima unaonufaika na mishahara ya watumishi hewa. Ni wazi kwamba wakuu wa idara husika, idara za uhasimu na mishahara wanawafahamu watumishi hewa ambao wanaendelea kulipwa mishahara. Tunasema hivyo kwa kuwa hao ndio wanaoandaa orodha ya malipo, kusaini na wengine kuipeleka benki, hivyo hawana namna yoyote ya kuukwepa mkono wa sheria.

Kutokana na hasara ambayo watumishi hawa wameisababishia serikali wote wanapaswa kusakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria na za kinidhamu ikiwamo kufikishwa mahakamani na kufilisiwa mali zao. Hili linaweza kuwa fundisho kwa watumishi wengine ambao wanaihujumu serikali.

Hata hivyo, tunaishauri serikali kwamba utaratibu wa kuwahakiki na kuwatambua watumishi wa serikali uwe endelevu kwa sababu bila kufanya hivyo, baadhi ya wajanja waliozoea kuiibia serikali watatumia mianya hiyo kuendelea kuiba kwa kutumia njia hiyo.

Mapema miaka ya 1990, serikali ilitumia utaratibu wa kuwalipa mishahara watumishi wake kupitia madirishani, lengo likiwa ni kuwatambua watimishi wake. Hata hivyo, utaratibu huo ulitumika kwa muda mfupi na utaratibu wa kulipa mishahara kupitia benki ukaendelea.

Inaelezwa kuwa utaratibu wa kulipia mishahara benki ndiyo uliosababisha kushamiri kwa vitendo vya sasa vya kulipa mishahara watumishi hewa.

Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuchukua hatua za kupambana na vitendo hivyo, lakini pia tunasisitiza kwamba uhakiki na utambuzi wa watumishi wa umma uwe endelevu, kuhakikisha kwamba ulipaji mishahara watumishi hewa unakomeshwa kabisa.