Tofauti na mtangulizi wake, Leodger Tenga, utawala wa Malinzi ni kama umevuruga kila kitu kizuri kilichowahi kufanywa na Tenga.
Ni utawala huu ambao kila kukicha umekuwa alama ya malalamiko kuhusu uendeshaji mbovu wa Ligi Kuu Bara, ambayo ndiyo taswira ya soka la Tanzania.
Ni katika utawala huu wa Malinzi, ratiba za ligi zimekuwa kizipanguliwa ovyo na kuifanya ligi kukosa mvuto.
Ligi ya Tanzania Bara sasa haina tena thamani kama ilivyokuwa zamani. Ligi imepoteza mvuto kutokana na mipango mibovu ndani ya shirikisho hilo.
TFF ya sasa ndiyo msingi wa malalamiko ya waamuzi. Hakuna msimu unaopita bila malalamiko dhidi ya waamuzi.
Ndani ya utawala wa Malinzi ndiko tunakoshuhudia makocha wakifanya kazi bila kulipwa mishahara. Mwanzoni mwa wiki hii, Kocha wa Taifa Stars Boniface Mkwasa baada ya kuvumilia muda mrefu, aliamua kuweka hadharani uhusiano wake na TFF.
Kocha huyo mzawa tangu achukue timu, amelipwa mshahara wa mwezi mmoja tu na sasa analidai shirikisho hilo Sh. milioni 200.
Inadaiwa pia kuwa hata kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco anafanya kazi hiyo bila mkataba. Inashangaza TFF kumteua kocha msaidizi wa timu ya taifa na kufanya naye kazi bila mkataba. Haya tunayaona kwenye utawala wa Malinzi.
Katika kuonyesha utawala wa Malinzi umeshindwa kazi, juzi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezikamata mali za shirikisho hilo (magari).
Baada ya kuzifunga akaunti zote za TFF na kuchukua pesa zote zilizokuwamo kiasi cha Sh. milioni 250, TRA ilirejea tena Karume zilipo kwenye ofisi za shirikisho kukamata magari matano kutokana TFF kudaiwa kiasi kikubwa cha fedha.
Shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu ya soka nchini, linadaiwa Sh. bilioni 1.6 ambazo zinatokana na ukwepaji kodi katika mishahara ya makocha wa timu za taifa (Jan Poulsen na Kim Poulsen) pamoja na kutokatwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mapato ya mechi ya Taifa Stars dhidi ya Brazil iliyoingiza Sh. bilioni 1.8.
Kwa mujibu wa TRA, TFF inadaiwa Sh. bilioni 1.118 ambazo ni kodi mchanganyiko kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.
Tunaamini, kama TFF ingekuwa inajiendesha vizuri na kufuata sheria na taratibu za ajira, bila shaka leo hii tusingekuwa tunazungumzia mlolongo wa madeni.
Lakini kutokana na kujiendesha kwa mazoea enzi na enzi, leo TFF imepoteza mwelekeo na inazidi kulizamisha soka letu.
Kutokana na hali hii, kumewafanya hata baadhi ya wadau kupoteza mvuto wa mashindano hayo na kujikita zaidi kwenye soka la Ulaya.
Kuna mifano mingi. Hivi sasa kuna idadi ndogo ya watazamaji wanaokwenda uwanjani kuangalia mechi za Ligi Kuu.
Hata kwenye mechi za Simba na Yanga ambazo ndio kiini cha mapato, idadi ya watazamaji imepungua kuliko maelezo.
Kuna sababu nyingi, lakini tunadhani kubwa ni TFF kushindwa kusimamia ligi hiyo katika hali ya ushindani kutokana na kupangua ovyo ratiba.
Katika kuonyesha soka la sasa limepoteza mwelekeo, upangaji wa matokeo nao ni tatizo kubwa hivi sasa. Ni lini tutafanikiwa kwa kushuhudia timu zikifungana mabao 16-0, 7-0 au 8-0.
Tunahitaji nini kwenye soka letu kama tunaruhusu mambo haya kuendelea kutokea? Zama hizi bado tunaendelea kumezwa na utamaduni wa kupanga matokeo?










