Tofauti ya mishahara katika sekta ya umma iangaliwe

31Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Tofauti ya mishahara katika sekta ya umma iangaliwe

RAIS Dk. John Magufuli, ameonyesha kukerwa na kofauti kubwa iliyoko katika viwango cha mishahara kwa watumishi wa umma.

Rais Magufuli alisema kuna tofauti kubwa ya mshahara kwa watumishi wa umma na kwamba wako wanaolipwa mishahara mikubwa na kuishi kama malaika na wengine wakilipwa kidogo sana.

Akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Chato, mkoani Geita juzi baada ya kuwasili kwa ajili ya mapumziko, alisema kuna watumishi wanaolipwa zaidi ya Shilingi milioni 40 kwa mwezi wakati wengine wanalipwa Shilingi 300,000.

Akionyesha kutofurahishwa na hali hiyo, Rais alisema kuwa serikali yake itaondoa tofauti hiyo kwa kupunguza mishahara ya wanaolipwa zaidi ya Sh. milioni 40 hadi Sh. milioni 15.

Tofauti ya mishahara iliyoko katika sekta ya umma inabainisha wazi kuwa kuna udhaifu ndani ya serikali kwa kuwa haiwezekani baadhi ya watu wakalipwa mishahara mikubwa kiasi hicho huku wengine wakilipwa kidogo, hali inayoibua matabaka.

Ni jambo linaloshangaza kwa kuwa kuna Wizara ya Utumishi ambayo ina dhamana ya kusimamia masuala ya stahiki za watumishi wa umma likiwamo suala la mishahara. Hata kama taasisi, wakala, mashirika ya umma na idara nyingine zinazojitegemea, lakini bado Utumishi inawajibika kuhakikisha kwamba hakuna taasisi yoyote ya umma inayojipangia viwango vya mishahara inavyotaka.

Moja ya mambo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya kwanza baada ya uhuru ni kuondoa matabaka nchini. Suala la mishahara pia lilidhibitiwa kwa kuweka tofauti ndogo sana ya mishahara ya watumishi wa sekta ya umma.

Hatua hiyo ililenga kuhakikisha kwamba kuna usawa badala ya kuwapo na matabaka miongoni mwao, tofauti na sasa ambako viwango vya miashahara vinatofautiana sana kama alivyobainisha Rais Magufuli.

Inawezekana kwamba tofauti kubwa ya viwango vya mishahara miongoni kwa watumishi wa sekta ya umama ikawa kikwazo cha tija na ufanisi katika utendaji na vilevile kusababisha tamaa kwa watumishi wanaolipwa kidogo kujihusisha na vitendo vya kuihujumu serikali vikiwamo vya mishahara hewa, rushwa, wizi na ubadhirifu.

Tunakubaliana na uamuzi wa Rais Mafufuli wa kufanya marekebisho ya viwango vya mishahara ya watumishi katika sekta ya umma ili vitofautiane kidogo.

Hata hivyo, tunashauri kwamba mfumo wa utumishi serikalini upitiwe kwa kina na viwango vya mishahara vipangwe kwa kuzingalia vigezo kadhaa kama elimu, uzoefu na utendaji wa kila mtumishi.

Haiingii akilini kuona serikali inayolalamika kwamba haina uwezo wa kifedha ikiwalipa baadhi ya watumishi mishahara ambayo inawafanya waishi maisha ya peponi.

Rais Magufuli katika mkutano huo pia aliahidi kuwa kuanzia bajeti ijayo ya 2016/17, serikali itapunguza kiwango cha kodi ya mshahara (PAYEE) hadi kufikia digitali moja. Suala hilo limekuwa kilio kikubwa cha wafanyakazi wote nchini kwa muda mrefu wakilalamikia kukatwa kodi kubwa.

Serikali iliyopita ilikuwa ikiahidi kupunguza kiwango hicho kwa muda mrefu, lakini hadi inamaliza muda wake haikutekeleza ahadi hiyo. Ni matarajio yetu kuwa Rais Magufuli ataitekeleza ahadi hiyo ili kuwapunguzia wafanyakazi nchini mzigo mkubwa wa kodi.