Hiyo ni mara pili kwa uanachama wa taifa hilo kujadiliwa, safari hii ikifanikiwa.
Ni mabadiliko yaliyoendana na kupatikana mwenyekiti mpya wa EAC, Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu mpya kutoka Burundi, mwanadiplomasia Liberat Mfumukeko, akichukua nafasi ya Dk. Richard Sezibera.
Mara ya kwanza, Sudan Kusini na Somalia licha ya kuwa na vigezo vingi muhimu katika maombi yao miaka kadhaa iliyopita, hazikupewa uanachama kutokana na hali tete ya usalama wa ndani katika nchi hizo na hususan mapigano ya wenyewe.
Sudan ya Kusini ni taifa ambalo moja ya utajiri wake ni uwepo wa mafuta ambayo hata ikifuatiliwa kwa kina, ndiyo chimbuko la mapigano ya wenyewe.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, uchumi wake umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 30.7.
Ni kwa namna gani uchumi wake unakua? Umeegemea zaidi bei ya mafuta duniani, kitu kinachohofiwa kuathiri uchumi wa nchi hiyo. Bei inadaiwa kushuka kwa wastani wa asilimia 20.
Kilimo chake bado hakijawa na sura pana zaidi, kwa maana ya uzalishaji uko katika kiwango cha kujilisha na kuna wakati hakitoshi, jambo linalozamisha kuagiza kutoka mataifa jirani kama vile Kenya, huku bidhaa nyingi za matumizi ya kawaida nazo zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Mwaka jana, mafuta ndiyo yalikuwa tegemeo kuu la kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia 99, pia asilimia 95 ya pato la taifa.
Dira njema ya maendeleo nchini humo ilionekana kabla ya kuibuka vita vya wenyewe mwezi Desemba mwaka 2013.
Mbali na uwekezaji wa mafuta, Sudan Kusini inatajwa kuwa na fursa lukuki za uzalishaji wenye kufungua milango ya ajira na uchumi kwa jumla.
Vivutio vinavyotajwa ni kama vile uzalishaji miti ya mipira ambayo ina uwezo wa kusitawi katika majimbo sita, kati ya 10 yaliyoko nchini humo na inachukua asilimia 46 ya ardhi yote kitaifa.
ILIKOTOKEA NA INAKOELEKEA
Mwanachama huyo mpya wa EAC ambaye pia ni mwanachama wa 55 wa Umoja wa Afrika (AU), ikiwa taifa huru kwa wastani wa miaka mitano sasa.
Hiyo ni baada ya kujiengua kutoka Jamhuri ya Sudan. Sasa ina safari ndefu yenye kukumbwa na historia ngumu ya misukosuko ya kisiasa iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50.
Hali hiyo inafanya sehemu kubwa ya raia wake kudumu katika vita na misuguano ya kisiasa, wengi wakiishi uhamishoni, hali iliyojitokeza tena muda mfupi tu baada ya kuanza kujitegemea kwa kuunda taifa la Sudan Kusini.
Kutokana na historia hiyo ya kuyumba kisiasa, taifa hilo jipya lina changamoto kubwa juu ya mustakabali wake wa kupiga hatua ya maendeleo.
Jicho na hatima ya mafanikio yote ni utekelezaji wa makubaliano baina ya Rais Salva Kiir na makamu wake, Dk. Riek Machaar, baada ya kutokea sintofahamu baina yao.
Hata hivyo, inakadiriwa kwamba akiba ya mafuta yaliyoko hivi sasa si nyingi sana na huenda kasi matumizi ya sasa inaweza kudumishwa hadi wastani wa miaka 20 ijayo, kwa maana ya mwaka 2035.
Baadhi ya shughuli kama vile kilimo cha kujikumu kimaisha kinachoendelea sasa Kusini, kinachangia kiasi kidogo tu, kwa mfano mwaka 2014 ilichangia asilimia 15 ya pato la taifa.
Hali ya kususua kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa, mathalan katika siku za karibuni ilishuka kutoka Dola za Marekani 110 hadi Dola 50.
Ni athari inayoelezwa uingizaji baadhi ya bidhaa kutoka nje ya nchi, ikiwemo kukidhi mahitaji ya chakula kitaifa.
Wakati asilimia 83 ya wakazi wakiwa wanaishi vijijini, kwa manaya sehemu ndogo ya nchi imejengeka katika sura ya mji, theluthi mbili ya wananchi ni vijana wenye umri chini ya miaka 230.
Kielimu pia nchi hiyo ina hali ngumu, sehemu kubwa ya wasomi wake wamepata elimu hiyo nje ya mipaka.
Ndani ya nchi ni asilimia 27 tu ya vijana wenye umri chini ya miaka 10 ndiyo wanaojua kusoma na kuandika. Kwa maana fupi, elimu hasa ya msingi bado ni duni.
Pia wastani huo wa wanaojua kusoma na kuiandika kwa wanaume wote ni asilimia 40 na kinamama ni asilimia 16.
Idadi ya vifo vya watoto wachanga ni asilimia 10.5 kwa kila wanaozaliwa na wajawazito wanaopoteza maisha ni asilimia 2.054.
Pia, idadi wenye fursa ya kutumia maji safi na salama ni asilimia 55 ya raia wote na kuna kundi la asilimia 38 kati ya raia wote wanaolazimika kufuata maji umbali wa kutembea kwa zaidi ya nusu.
Katika matumizi ya choo ndiko kwenye hali mbaya, kwamba asilimia 80 na hasa wakazi wa vijijini hawana huduma hiyo.










