Ameweka rekodi ya kufunga 'hat-trick' ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kwa mwaka huu akiisaidia timu yake ya Azam kuichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 4-3.
Huyu ni kiungo mshambuliaji machachari wa Azam raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche.
Kwa matokeo hayo, Azam imesonga mbele kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 7-3, kwani kwenye mechi ya kwanza ugenini nchini Sauzi, ilishinda mabao 3-0.
Timu hiyo sasa itapambana na Esperance ya Tunisia.
Kwenye mechi iliyofanyika Chamazi, Kipre alihusika na magoli yote manne kwani alimtengenezea pasi safi Bocco aliyefunga goli moja kwenye mechi hiyo.
'Hat-trick' hiyo pia imemfanya Tchetche kuweka rekodi nyingine ya kutupia mabao matatu kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Tanzania na michuano ya CAF tokea alipojiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea Jeunesse Club d'Abidjan Treichville (JCAT) ya kwao Ivory Coast.
Kihistoria hiyo ni 'hat-trick' yake ya pili kwenye soka la ushindani, ya kwanza akiifunga alipokuwa JCAT walipocheza na Bingerville (4-0) katika ligi ya kwao, yeye akifunga mabao yote manne.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kipre alisema ana furaha kubwa kufunga mabao hayo kwani amekuwa akijitahidi sana kila mara kujituma na kufanya vema uwanjani.
“Sina cha kusema sana, ila ni muendelezo wa kujituma uwanjani kwa ajili ushindi na kupata matokeo mazuri kwenye mechi,” alisema mchezaji huyo ambaye kwa sasa ana magoli tisa kwenye orodha ya wafungaji Ligi Kuu, akiwa kinara wa ufungaji kwenye timu ya Azam FC.
Kuhusu mechi dhidi ya Esperance alisema itakuwa ni mechi ngumu.
“Itakuwa ni mechi nzuri, kwani ni moja ya timu nzuri (Esperance), tunatakiwa kufanya kazi vizuri zaidi ya tulivyofanya kwenye raundi ya kwanza.”
Tchetche ambaye pia kuwa wakati Azam humtumia kama straika, badala ya kiungo mshambuliaji wa pembeni ni mmoja wa wachezaji wa kigeni wanaojua nini kimempandisha ndege kutoka mjini Abidjan, Ivory Coast mpaka jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Msimu wa 2012/13, aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na kutwaa kiatu cha dhahabu alipofunga magoli 17 na msimu uliofuata aliisaidia timu yake ya Azam kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa timu hiyo.
Tchetche anakumbukwa na mashabiki wa soka alipokuja kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam na timu yake ya taifa ya Ivory Coast kushiriki mashindano ya CECAFA 2012.
Alikuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani, kiasi kwamba Azam haikufanya makosa, ikarusha ndoano na kumsajili.
Akimzungumzia mchezaji huyo, kocha wa Azam, Stewart Hall, aliwahi kusema kuwa ni mmoja wa wachezaji ambao ni mhimili wa Azam FC.
"Tchetche ni mchezaji mzuri ana kipaji na nguvu za mpira kiujumla ni msaada katika timu. Anacheza kitimu na kwa ushirikiano na wenzake na anafuata maelekezo unayompa," alifafanua.
Hata hivyo, alisema bado ana makosa madogo madogo ambayo wakati mwingine ni kawaida kwa wachezaji wengi duniani.
"Kuna sehemu ambazo ni rahisi kufunga huwa anakosa na nyingine ni ngumu kufunga yeye anafunga na kwangu nachukulia ni kawaida tu," alisema kocha huyo.










