Tamongsco: Bila chombo huru kusimamia elimu, hatutafanikiwa

22Mar 2016
Restuta James
Dar
Nipashe
Tamongsco: Bila chombo huru kusimamia elimu, hatutafanikiwa

WAKATI serikali ya Tanzania ikifanya jitihada za kila aina kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anafanikiwa kuingia shuleni, tafiti zinaeleza kuwa takribani wasichana milioni 16 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 11 hawatopata fursa ya kusoma wala kuandika kwenye shule za msingi.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Lupemba.

Ripoti ya Taasisi ya Takwimu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sanyansi na Utamaduni (Unesco), iliyotolewa mapema mwezi huu inaeleza kuwa wavulana wenye umri huo ni milioni nane ikilinganishwa na wasichana.

Ripoti hii ilitolewa wakati wa kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake Machi 08 na takwimu hizo za Unesco kuhusu ‘usawa wa kijinsia katika elimu’ zinaonyesha kwamba wasichana bado ni wa kwanza katika kunyimwa haki ya elimu licha ya juhudi zote zilizofanyika na hatua zilizopigwa katika miaka 20 iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pengo la kijinsia ni kubwa hasa katika mataifa ya Kiarabu, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini na Magharibi mwa Asia.

Inaeleza zaidi kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo, wasichana milioni 9.5 hawatowahi kuhudhuria shule ikilinganishwa na wavulana milioni tano.

Kwa jumla ripoti ya Unesco inafafanua kuwa watoto zaidi ya milioni 30 wa umri wa miaka sita hadi 11 hawasiomi hivi sasa.

ELIMU BURE
Wakati ripoti ya Unesco ikieleza hivyo, serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.

Hata hivyo, sekta ya elimu nchini inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo uhaba wa madarasa na kulazimisha ama shule kufungwa kwa muda usiojulikana au wanafunzi kusomea chini ya miti.
Changamoto nyingine ni uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, maabara pamoja na maktaba kwa shule za sekondari.

Mpango wa elimu bure umeibua changamoto lukuki kutokana na ‘mafuriko’ ya wanafunzi hasa elimu ya msingi ambao wamekosa madarasa.

Mathalani, baadhi ya shule za msingi jijini Dar es Salaam wanasomea chini ya mti wakiwa wamekaa kwenye matofali wakati kwenye baadhi ya mikoa, ni jambo la kawaida kwa wanafunzu kusoma wakiwa kwenye madarasa yaliyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi wakiwa wamekalia matofali.

Changamoto kama hizo zimelazimu baadhi ya shule kufungwa kwa muda usiojulikana kama ilivyotokea wilayani Magu, mkoani Mwanza ambako Shule ya Msingi Lupemba imefungwa kutokana na kukosa huduma muhimu.

Shuleni hapo, wanafunzi walioruhusiwa kuendelea na masomo ni wale tu wenye mitihani ya taifa ambao ni wa darasa la nne na la saba.

Kufungwa kwa shule hiyo yenye wanafunzi 651, kwa muda usiojulikana kunathibitishwa na Mwalimu Mkuu Daniel Matemi.
Hata hivyo, aliyekuwa mhadhiri mwanzamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Donath Olomi, anasema pamoja na kwamba kuna watoto ambao hawatapa kabisa fursa ya kwenda shule, bado elimu inayotolewa ni duni na hailengi kuwakomboa maskini.

Dk. Olomi ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali (IMED), akizungumzia ripoti ya Unesco anasema hapa nchini kuna watoto hawaendi shule kwa sababu mbalimbali ikiwamo wanaotoa jamii za kifugaji kama Wamang’ati ambao wanajua jukumu la msingi la mtoto ni kuchunga ng’ombe.

“Lakini kuna shule ziko mbali kiasi kwamba wazazi hawawezi kuwaandikisha watoto shule hasa wadogo,” anasema.
Anaongeza pia kuwa: “Kuna watu ambao hata uwezo wa kununua sare hawana na ndio maana mradi wa Tasaf (Mfuko wa Jamii), zinasadia kaya maskini ili angalau ziweze kumudu kununua sare.”

Dk. Olomi ambaye ni gwiji wa uchumi, anasema kimsingi elimu haijapewa rasilimali za kuiweka katika kiwango kinachotakiwa.

Anasema: “Tukitaka tupate maendeleo ya msingi lazima tuwekeze katika elimu bora hasa kwa watu maskini.”
“Wapo wanaosema kuliko kukosa kabisa, bora watoto waende shule wakatupie chochote badala ya kukaa nyumbani…elimu yetu inahitaji uwekezaji mkubwa,” anasema.

Anashauri kwamba ili kumkomboa mwananchi maskini walau kila mkoa uwe na shule 10 bora ambazo zitawekewa walimu wa kutosha, madawati na vitabu vya kiada na ziada.

Anasema bila kufanya hivyo, mfumo wa sasa wa elimu utaendelea kuwabagua zaidi wananchi maskini na kuwadidimiza kwenye lindi hilo.

“Maana yangu ni kwamba kukiwa na hizo shule maskini wachache watakaopata elimu nzuri watakuja kuwakomboa wenzao kuliko hivi tunavyokwenda,” anasema.

UCHANGIAJI
Hata hivyo, Dk. Olomi anakosoa mpango wa elimu bure akieleza kuwa unaondoa ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo zinazowahusu.

Anasema jukumu la kusomesha Watanzania wote haliwezi kuachiwa serikali pekee kwa kuwa ni mzigo mkubwa.
Anasema jamii lazima ijenge mwamko wa kuchangia elimu akitolea mfano shule ya Lupembe iliyofungwa kwamba wananchi wa eneo husika wangeweza kujenga shule nzuri ya miti kwa gharama ndogo.

“Sasa hivi choo cha shule kinaweza kuharibika, lakini wananchi hawajishughulishi kwa sababu wanaamini ni jukumu la serikali, hii ni kwa sababu utaratibu wa kujitolea umepotea,” anasema.

Dk. OIomi anasema: “Tujenga utaratibu wa wananchi kuona hizi ni shule zetu, wachukue wajibu wa kuziendeleza.”
“Nadhani jambo hili linahitaji mjadala kujenga utaratibu wa wazazi kuchangia kwa sababu hii elimu bure inadumaza na ndio maana hata watoto wanashinda shuleni wakiwa na njaa,” anaongeza.

Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Benjamin Nkonya, anasema njia ya kuwasaidia watoto wengi zaidi kupata elimu ni kwa kuweka mfumo huru wa usimamiaji wa sekta ya elimu.

Anatoa mfano kuwa shule za sekondari nchini ni 4,000, lakini zinasimamiwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari, ambaye ni mmoja; hivyo anasema hawezi kufanyakazi kwa ufanisi unaotakiwa.

Badala yake anasema ni vyema likaundwa baraza au chombo mahsusi kitakachosimamia sekta hiyo kama ilivyo kwenye sekta nyingine kama afya, usafiri au Shirika la Viwango (TBS), ambacho kitakuwa na uwezo wa kufunga shule ya serikali au binafsi ambayo haina viwango vinavyostahili.

“Kwa nini elimu yetu inaporomoka ni kwa sababu unakuta shule ina wanafunzi 400 na mwalimu mmoja, lakini serikali haiwezi kuchukua hatua kwa sababu ni shule yake,” anasema.

Anasema katika mazingira hayo, unakuta pia wanafunzi wote wanafaulu, lakini wanamaliza elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma wala kuandika. “Na husikii mtu akichukuliwa hatua.”

Anasema: “Badala yake utamsikia Waziri anatangaza kwamba ufaulu umeongezeka au tumefanikiwa kuandikisha wanafunzi wengi, bila kupima kile mtoto anachokipata shuleni.”

Nkonya anasema tangu mwaka 1976 hadi sasa, bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka huku kiwango cha ufaulu kikiwa kinashuka.

Anasema kinachosababisha elimu iporomoke ni mfumo mbaya wa elimu ambao serikali inamlazimisha kila mtoto kuingia shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu.

Anasema lazima uwepo mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi na kuweka mtiririko wa kuzalisha wataalam kwa kusisitiza elimu ya ufundi stadi.

Anasema kulishaanzishwa mpango wa Universal Primary Education (UPE), Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem), Mpango wa Elimu ya Sekondari (MES) na hivi sasa wa Matokeo Makubwa (BRN); ambayo hata hivyo haujazaa matunda.

“Hii BRN ni kama imepanua tu magoli ili wengi wafunge. Walishusha kiwango cha ufaulu ili ionekane watoto wanafanya vizuri, lakini kwa hakika haitusaidii,” anasema.

Anasema ambacho serikali ilitakiwa kufanya ni kutoa ruzuku ya vocha kwa wazazi na kuwaruhusu kuwasomesha watoto sehemu yoyote, badala ya inavyofanya sasa.

Anasema hivi sasa serikali inagharamia Sh. 4,000,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari na kwamba kwa mfumo wa vocha, ingeweza kutoa Sh. 2,000,000 na wanafunzi wakapata elimu nzuri.

Hata hivyo, anasema mfumo mzima wa elimu unapaswa kutazamwa kwa kuzalisha watendaji kama madaktari, wahadhiri, walimu pamoja na wataalam wengine na kujenga mfumo wa ufundi ili kuzalisha nguvu kazi kubwa zaidi kwa uchumi wa nchi.

Anasema miaka ya 1970 kulikuwa na shule chache na usimamizi imara, lakini sasa kuna shule nyingi wakati mfumo wa usimamizi ukiwa ule ule.

MATOKEO MAKUBWA
Wakati elimu ikikabiliwa na changamoto hizo, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), uliozinduliwa mwaka juzi uliweka mikakati tisa ikiwa ni pamoja na upangaji rasmi wa shule kwa ubora wa ufaulu, utoaji tuzo kwa shule zinazofanya vizuri, kuandaa kiongozi cha kuimarisha utendaji wa shule na kuanzisha programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na kujifunza.

Mikakati mingine ni upimaji wa kitaifa wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na kutoa mafunzo ya KKK kwa walimu, uimarishaji wa miundombinu ya shule, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, na utoaji wa motisha kwa walimu.

Pia kupandisha kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 31 kwa shule za msingi na asilimia 34 kwa shule za sekondari za mwaka 2013, hadi asilimia 80 mwaka jana. Hata hivyo, mikakati hiyo haijafanikiwa.

UTAFITI WA TWAWEZA 2014
Licha ya matarijio kuwa watoto wote wa darasa la 3 wangeweza kusoma Kiswahili na Kiingereza, pamoja na kufanya hesabu rahisi za darasa la pili, ripoti ya mwaka 2014 ya utafiti inaonyesha kuwa ni wanafunzi wachache wenye uwezo huo.

KISWAHILI
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa nusu ya watoto wa darasa la 3 yaani asilimia 45 wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la 2. aidha, waliofika darasa la 7, wenye uwezo wa kusoma Kiswahili cha darasa la 2 ni asilimia 80. Hii inaashiria kuwa asilimia 20 ya wanafunzi humaliza darasa la 7 wakiwa hawawezi kusoma Kiswahili.

KIINGEREZA
Ripoti ilianisha kuwa bni wanafunzi 2 kati ya 10 yaani asilimia 19 wa darasa la 3 wanaweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la 2.

Waliofika darasa la 7, ni watoto 6 kati ya 10 yaani asilimia 56 wenye uwezo wa kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha darasa la 2. Takriban nusu ya wanafunzi wote wa darasa la 7 hawajui kusoma Kiingereza, lugha ya kufundishia shule za sekondari.

HESABU
Utafiti ulibaini kuwa asilimia 31 ya watoto wa darasa la tatu wanaoweza kufanya kwa usahihi hesabu ya kuzidisha za darasa la 2 wakati asilimia 29 ya watoto wa darasa la 7 hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za darasa la 2.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iitwayo Je, Watoto wetu wanajifunza? Uwezo wa Kusoma na kuhesabu nchini
Tanzania 2014 utafiti uliofanyika mwaka mwaka 2013 ambako watoto 100,000, wenye umri wa miaka 7-16, kwenye wilaya 131 katika mikoa 25 walipimwa.