Bado haijatokea Ligi Kuu 2015/16

21Mar 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Bado haijatokea Ligi Kuu 2015/16

WAKATI Ligi Kuu ikielekea ukingoni, timu zimeweka rekodi mbalimbali hadi sasa.

Wachezaji wa Simba

Kuna baadhi zimeweka rekodi nzuri, zinafurahisha na zingine zinashangaza.
Mwandishi wa makala hii amekusanya baadhi ya rekodi zilizowekwa na timu msimu huu.

1. Yanga kupoteza mechi Taifa

Mabingwa watetezi Yanga ni timu haijapoteza mechi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga yenye pointi 50, imecheza mechi 13 kwenye uwanja huo, ikishinda mechi 11 na kutoa sare mbili tu.
Mechi zote mbili za sare imetoka na Azam FC ikiwa ni mechi ya nyumbani na ugenini.

Timu hiyo inahesabiwa kuwa imecheza mechi 11 nyumbani Taifa, lakini mbili zinaongezeka kutokana na kucheza na Simba na Azam, ambazo pia zinautumia uwanja huo kama wa nyumbani, hivyo kujumlisha kuwa mechi zote hizo iilizocheza Taifa na haijafungwa. Kumbuka kuwa Yanga imefunga Simba mabao 2-0 nyumbani na ugenini.

2. Azam kufungwa Azam Complex

Timu ya Azam haijapoteza mechi yoyote kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Azam imecheza mechi tisa kwenye uwanja huo, imeshinda nane na kutoa sare moja.

Hata hivyo, Azam nayo inahesabika kuwa imecheza mechi 11 nyumbani, lakini kuna mechi mbili za nyumbani ambazo hazikucheza kwenye uwanja huo dhidi ya Simba na Yanga ambazo zilichezwa Uwanja wa Taifa.

Mechi mbili ilicheza na Yanga moja ikiwa ya nyumbani na nyingine ugenini na mechi moja ilicheza dhidi ya Simba iliyohesabika kuwa Azam iko nyumbani ambazo zote tatu zilimalizika kwa sare.

Mechi 11 ukitoa mbili zilizochezwa Taifa, zinabaki tisa zilizichezwa na timu hiyo Chamazi.

3. Simba kutoka sare nyumbani

Timu ya Simba haijatoka sare yoyote kwenye uwanja wake wa nyumbani tangu kuanza ligi.
Timu hiyo imecheza mechi 11 zilizohesabika kuwa ni za nyumbani, ikishinda mechi 10 na kufungwa moja.
Mechi pekee iliyofungwa ni dhidi ya Yanga tu.

Hata hivyo, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam Uwanja wa Taifa, lakini mechi hiyo ilihesabika kuwa yeye ni mgeni, hivyo kikanuni haihesabiwi kuwa ni sare ya uwanja wa nyumbani.

Pia Simba imecheza mechi 13 uwanja wa Taifa, lakini kikanuni inahesabika kuwa ni 11 kwa sababu mbili ilicheza na Yanga na Azam ambazo kwao zilikuwa ni mechi za nyumbani ndiyo maana pamoja na kufungwa mara mbili na Yanga, lakini inahesabika kuwa imepoteza mechi moja tu nyumbani.

4. Prisons kuchapwa Sokoine

Timu ya Prisons nayo imeingia kwenye rekodi kwa kutopoteza mechi yoyote Uwanja wake wa nyumbani Sokoine Mbeya hadi sasa.

Timu hiyo ambayo wiki hii ilikuwa ugenini mjini Tanga kucheza dhidi ya African Sports, imecheza mechi 12 Uwanja wa Sokoine.

Kati ya mechi hizo, imeshinda mechi sita na kutoka sare mara sita uwanja wake wa nyumbani. Imevuna pointi 24 ikicheza nyumbani.

5. Coastal kushinda ugenini

Timu hii yenye maskani yake mjini Tanga haijashinda mechi yoyote nje ya uwanja wake wa Mkwakwani Tanga.
Imecheza mechi 11 ugenini, lakini hakuna hata mechi moja iliyofanikiwa kuondoka na pointi zote tatu.
Rekodi zinaonyesha kuwa imepoteza mechi tisa na kutoka sare mara mbili tu ugenini.

Kwa maana hiyo imevuna pointi mbili tu ugenini mpaka sasa na kuwa timu pekee iliyopata pointi chache ikicheza nje ya uwanja wake wa nyumbani.

6. Majimaji kuifunga timu yoyote nje

Ikiwa imeikaribisha Mbeya City nyumbani wiki hii, timu ya Majimaji ya Songea haijaifunga timu yoyote ile nje ya uwanja huo.
Imekuwa ikiambulia sare ama vipigo tu, kila inapotoka Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Timu hiyo imecheza mechi 13 nje ya uwanja wake wa nyumbani, ikiwa ni moja kati ya timu chache zilizocheza mechi nyingi ugenini.

Imepoteza mechi nane kwenye viwanja mbalimbali ilipokwenda kucheza Ligi Kuu, huku ikiwa imetoa sare mara tano.
Imekusanya pointi tano tu hadi sasa nje ya Uwanja wa Majimaji.