Utamaduni huo umetokana na mazingira yanayozunguka mchezo huo wenye historia ndefu na unahusisha wachezaji, mashabiki na timu zao.
Kwa mfano ukizungumzia masuala ya wachezaji kuna mambo mbalimbali ya kuangalia kama wachezaji nyota, asili yao, tabia zao ndani na nje ya uwanja.
Ukija kwa mashabiki, nao utaangalia tabia zao kama staili ya ushangiliaji, vurugu na furaha au maumivu yao timu zao zinapopoteza mechi na wengine kwenda mbali kucheza kamari ili kutabiri nafasi ya timu zao au zile pinzani.
Kwa upande wa timu, unaangalia rangi wanazotumia, viongozi na hata matumizi ya fedha, rushwa na `fitna’ za kushinda mechi.
Soka ni moja ya michezo inayounganisha makundi yote ndani ya jamii, wakiwemo watoto, vijana na wazee bila kujali jinsia zao.
Ili utamu wa mechi uonekane, pande mbili za mashabiki huonyeshana tambo na hii hufanyika ndani ya uwanja, mtaani au majumbani.
Wapo ambao hufikia hatua ya kuwa maadui na uhasama huu hudumu katika mechi zote zenye upinzani mkali ama kawaida.
Wengine kutokana na ushabiki uliopitiliza, huzimia na kuna baadhi hufikia hatua ya kushindwa kuficha hisia zao na kujikuta wakifanya mambo tofauti, ikiwemo kuvunja sheria ili mradi ni moja ya kuishabikia timu zao.
Moja ya kisa kilichotokea ni kile cha mchezaji na shabiki sugu mwanamke aliyeamua kujitoa ‘ufahamu’na kuvunja sheria na kuingia katika uwanja uliokuwa na mashabiki wanaume huko nchini Saudi Arabia.
Mwanamke huyo aliyeingia uwanjani kwa kuvalia mavazi ya kiume alijikuta mashakani kutokana na viwanja vya soka nchini humo vina masharti yake, wanawake hawaruhusiwi kuchanyikana na wanaume.
Wanasema ushabiki hauna mipaka na hii inadhihirishwa na mashabiki wa Tanzania ambao wameshindwa kuficha hisia zao dhidi ya ligi za Ulaya na wamejikuta wakitumia fedha nyingi kuwekeana dau pindi timu pendwa zinapocheza.
Upenzi wa soka kwa makundi hayo ni kidhihirisho tosha ama kimeua au kufifisha michezo mingine, miongoni ni ule wa ‘Pool Table’ ambao ulikuwa na mashabiki wengi.
Katika kudhihirisha hilo miaka mitano iliyopita vituo vya mchezo wa kubashiri matokeo (betting) vilianzishwa maeneo tofauti nchini na mashabiki wamekuwa wakimiminika kuweka ‘karata’ zao dhidi ya mechi za ligi za kimataifa ili kujipatia fedha.
Matokeo yakiwa chanya, mashabiki hujinyakulia fedha kwa viwango tofauti kulingana na pointi ya timu alizochagua.
MASHABIKI WAFUNGUKA
Bundala Didi mkazi wa Makongo Juu, jijini hapa ni mmoja wa mashabiki wa kubashiri timu ambazo anaamini zitafanya vizuri kwenye ligi ya dunia.
Didi, ambaye sasa ana miaka mitatu kutoka aanze kubashiri anasema mchezo huo tofauti na ule wa ‘Pool Table’ unalenga kuleta matumaini ya utajiri.
“Mchezo huu unalenga kubadilisha maisha ya mtu wakati wowote, kama utabashiri vizuri na matokeo ya timu yakawa kama ulivyobashiri ndivyo unavyopata fedha,” anasema.
Anaeleza inapotokea kunakuwa na mechi nzuri siku hiyo hujikuta akitumia zaidi ya Sh. 100,000 ingawa kushinda kunatokana na bahati.
“Hii ni bahati nasibu kuna kupata na kukosa na kukosa ndio kwingi kuliko kupata, unatumia fedha nyingi faida ni ndogo, labla itokee kile ulichobashiri kikawa kweli hapo utavuna kulingana na timu na hela uliyoweka,” alisema.
Anasema katika kipindi cha miaka mitatu kutoka aanze kubashiri ameambulia Sh. 180,000 kati ya fedha alizotumia ambazo sasa zinazidi Sh. milioni tano.
AUFANANISHA NA ‘FREEMASON’
Didi anaenda mbali na kusema mchezo huo ni sawa na ‘Freemason’ kwa sababu mtu anayeingia hatamani kutoka.
“Nimeliwa fedha nyingi, lakini huweziamini sitamani kuuacha, huu mchezo ni kama ulevi wangu nikilala nikiamka nawaza kubashiri tu, kwa hiyo kwa wiki nabashiri mara mbili na inaweza ikapita miezi miwili sijashinda, lakini sitamani kuacha, sijui ni kwa nini,” anabainisha.
Didi ambaye ni baba wa watoto wanne anasema mara atokapo kwenye biashara zake mjini, hawezi kurudi nyumbani kabla ya kwenda kwenye kituo kubashiri timu kama kumi.
“Kila wiki natumia kati ya Sh. 20,000 hadi Sh. 25, 000, nilivyoanza washabiki tulikuwa wachache na timu zilizokuwa kwenye chati ni zile kubwa na zilikuwa zinafanya vizuri, lakini sasa hivi hazifanyi vizuri kwa hiyo tumehamia kwenye timu ndogo," anasema.
Didi anafafanua kuwa timu kubwa zimepunguziwa pointi, hivyo kama mtu ameweka Sh. 100,000 atapata Sh. 110,000.
Zile za daraja la tatu anasema endapo mtu ameweka Sh. 10,000 akifanikiwa hupewa Sh. 30,000.
Kuhusu changamoto, Didi anasema ni kubwa kwa sababu mchezo huo ni hatari unaomfanya mtu kuwa mkereketwa aliyepitiliza.
“Ukishaingia kwenye haya mambo ni shida huwezi kuacha ni kama mvuta bangi au mbwia unga, huwezi kuwa na amani na ukalala bila kununua tiketi hata kama huna hela utajikuta unafanya kila namna uipate hii ni hatari zaidi inaweza kumfanya mtu akaingia kwenye vitendo visivyofaa kisa apate hela,” anasema.
Anabainisha kuwa, mchezo huo unawafaa matajiri lakini kwa watu wenye kipato cha kawaida, anapoingia hawezi kukubali ipite siku bila kununua tiketi.Anasema mteja anaweza kununua tiketi kwa njia mbalimbali ikiwemo simu ya mkononi.
“Asilimia 45 ya watu hususan vijana wanajihusisha na mchezo huu iwe kwenye simu au kuja sehemu kama hii na kununua tiketi zake, unajua kila mtu anawaza utajiri, hivyo mchezo huu ni kamali ambayo unaweza kutajirika au ukawa maskini zaidi,” anasema.Kuhusu kipato, anasema mchezo huo haumwongezei kipato chochote zaidi ya kummalizia fedha zake.
“Siwezi kuuacha kwa sababu mimi sio mlevi, sio mvuta sigara wala sio mtu wa wanawake, huu mchezo ndio ulevi wangu ila hatari yake kama nilivyosema unamaliza fedha na ukiingia hutamani kutoka,” anasema.
Shabiki mwingine kijana, Godfrey Nkoswe, mkazi wa Mbezi Beach, anabainisha kuwa, vijana wengi wanaupendelea mchezo huo kwa sababu ya mazingira yake.
“Sio vijana wote wanapenda kwenda baa, `pool’ nyingi zipo baa na kuna watu hawapendi mazingira hayo, lakini pia vijana wamekimbilia mchezo huu wa kubashiri kwa sababu ya kutaka fedha za haraka,wanaamini huku kuna fedha kuliko kule,” anasema.
Anaeleza alijiunga na mchezo wa kubashiri miezi saba iliyopita na amewahi kupata Sh. 200,000 wakati awali alitumia Sh. 2,000 tu.
Mmoja wa wafanyakazi kwenye maeneo hayo ya kubashiri Abdallah Shaban, anasema mchezo huo upo kihalali na kwamba wanaume hususani vijana ndio hujitokeza kwa wingi ingawa sababu hazifahamu.
Anasema mbali ya mchezo huo wa kubashiri mpira wa miguu, michezo mingine ni mbio za farasi, mbwa na ule wa kuchagua namba.
Kuhusu faida anasema pande zote zinafaidika ingawa changamoto kubwa kwao ni kukatika katika kwa mitandao.
Anabainisha kuwa ligi zinazopendwa ni zile za Uingereza na Hispania na wateja wengi hununua tiketi kati ya tano hadi 10.
MCHEZO UPO KISHERIA
Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba anasema mchezo huo upo kisheria na kwamba umekuwa ni mmoja ya ile inayoliingizia kipato taifa.
Anasema mpaka sasa kuna vituo 2,684 vya kubeti nchini na kwa mkoa wa Dar es Salaam pekee vipo 1,344.
Anasema michezo ya kubeti huendeshwa na kampuni zilizosajiliwa kisheria, hivyo vituo vya kubeti ni vya biashara husika na husajiliwa pindi vinapoanzishwa kulingana na biashara inavyokua.
“Kuna kampuni 12 zilizosajiliwa kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2010, ambapo kampuni ya kwanza ilisajiliwa,” anasema.
Anaongeza kuwa kubeti ni miongoni mwa michezo ya kubahatisha inayoendeshwa chini ya bodi hiyo, ambapo changamoto zake ni ukuaji wa kasi wa michezo hiyo ya jiji la Dar es Salaam.
“Hii ni kutokana na michezo kukubalika na pia kwa kuendelea kuwa na fursa ya kiuchumi ambayo inahimili michezo hii. Ukuaji huu wa kasi unaipa changamoto Bodi katika usimamizi lakini tunaimudu kwa kuongeza uwezo wa watu wake,” anasema.
Anataja changamoto nyingine kuwa ni udhibiti wa ushiriki wa watoto katika michezo. “Sheria inakataza watoto kushiriki katika michezo yote ya kubahatisha ikiwemo ya kubeti, Bodi imeendelea kuweka udhibiti imara ili kuhakikisha watoto hawashiriki katika michezo hii kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika sehemu za zinazoendesha, “ anafafanua.
Anaongeza, “Bodi hutumia njia za siri zikiwepo watoa habari wa siri, kwa maana ya “whistle blowers” kupata taarifa.
Taarifa zinazotolewa huisaidia Bodi kuimarisha mbinu za kuhakikisha watoto wadogo hawashiriki,” anasema.
Changamoto nyingine ni waendeshaji kutopenda kwenda mikoani kutokana na mazingira ya biashara na miundombinu iliyopo hivyo kusababisha kusiwe na uendeshaji wa michezo mikoani.
Hata hivyo, kutokana na kuendelea kukua kwa teknolojia, anasema michezo hiyo sasa inaendeshwa kwa njia ya simu na intaneti ambayo huwezesha kufikia kwa watanzania wengi.
MCHANGO KATIKA PATO LA TAIFA
Tarimba anasema kiasi kilichokusanywa kuanzia 2012/13 hadi Desemba 2016 ni Sh. bilioni 14.0 na kwamba imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 7,000.
Pia anataja faida nyingine za kiuchumi kuwa ni pamoja na `resource mobilization’, ambapo fedha ndogondogo huingizwa katika mfumo rasmi wa uchumi, hivyo kutengeneza mitaji.
Kadhalika anasema hutoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania kwa njia mbalimbali, zikiwemo kupangisha nyumba za ofisi, kuchangamsha biashara nyingine kama vile ya mitandao ya simu, kodi kwa njia ya uingizaji wa vifaa vya michezo.
Kuhusu malengo anasema ni kuwa na vituo mahsusi na bora zaidi kwa ajili ya kuendeshea michezo hii na inayoendelea kukidhi matakwa ya sheria ambapo udhibiti utakuwa wa kiwango kikubwa.
Pia kuendelea kuboresha kanuni za kusimamia michezo hiyo ili kuongeza ufanisi wake na pato kwa Taifa.










