Utaulindaje ubunifu wako kisheria?

18Mar 2016
Denis Maringo
Nipashe
Utaulindaje ubunifu wako kisheria?

Binadamu tumejaliwa akili na utashi unaotutafaisha na viumbe wengine na jambo hili ni wazi kwa wale wenye imani na wasio na imani za kidini.

nembo ya biashara ya Cocacola, kama anavyoonekana katika shughuli za promosheni. (picha na mtandao).

Katikati ya ukweli huo, tunafahamu pia, hata binadamu tunatofautiana mno kati yetu, kama ilivyo kiyume chake tunapofanana kwa vitu vingi.

Moja ya mambo yanayotutofautisha, ni namna ambavyo binadamu mmoja anaweza kufikiri, kubuni na kutengeneza vitu ambavyo wenzake hawakuwahi kuviwazia au kudiriki kuvitengeneza.

Mara nyingi tunatumia maneno kama ubunifu, kipaji na kadhalika kumtambulisha yule ambaye amethubutu kufanya jambo ambalo kama lisingefanyika, pengine lingeonekana ni kama ndoto.

Baadhi ya mifano halisi ya kazi za ubunifu wa binadamu, inajidhirisha katika vyombo vya kisayansi kama magari, ndege, meli, treni, kompyuta, simu za mezani na za viganjani, televisheni (luninga) na friji (majokofu).

Mifano mingine ni mashine za benki za kutolea fedha (ATMs), programu za kompyuta na tovuti za kijamii kama vile facebook, whatsapp, instagram, na kadhalika.

Angalia pia ubunifu wa dawa kama vile asprini, panadol na Viagra au viatu, nguo, viberiti, taa za umeme, tungo na santuri za miziki na kadhalika.

Mara moja mtu utagundua kuwa, yote hayo yalitokana na uwekezaji uliofanywa na mtu, kikundi cha watu, kampuni na hata nchi katika kukifanya hicho kilichofanyika.

Uwekezaji huo huhusisha muda mrefu wa kutafakari, kupanga na kufanya jambo hilo na matumizi ya jitihada za kimwili na fedha.

Kwa hivyo, utaona kuwa ni lazima kungehitajika sera na sheria za kuwalinda wale wanaotumia muda, akili, nguvu na fedha zao nyingi kuvumbua au kutengeneza vitu ambavyo vinazidi kurahisisha maisha yetu.

Hiki ndicho tunachokizungumza hapa kwa sasa, yaani ni sheria zipi zinamlinda mtu wa aina hii?

Ndugu wasomaji, sheria zinazolinda kazi za ubunifu wa akili (kimombo Intellectual Property Laws) zinaangukia katika makundi takribani matatu hivi, kama si manne, japo tumezoea kuziita kwa ujumla kwa jina la sheria za Hakimiliki.

Tanzania tuna sheria mahsusi za jambo hili na taasisi ama mamlaka kama COSOTA na BRELA zinahusika kwa karibu.

Mosi, sheria zinazolinda uvumbuzi wa kazi za kisayansi kama mashine, programu za kompyuta, kanuni zilizounda ama dawa au kinywaji na kadhalika. Hizo zinajulikana kwa kimombo kama Patent Law na bahati mbaya sijapata neno mbadala la Kiswahili.

Basi kama unatengeneza aina moja ya kitasa cha mlango, unavumbua dawa ya kutibu malaria, au kinywaji chenye ladha mpya, basi eneo hilo linakuhusu.

Kundi la pili katika sheria zinzaolinda kazi za ubunifu, ni ile inayoitwa kwa kimombo copyright laws inalinda kazi kama za utunzi wa vitabu na riwaya, tungo za muziki na filamu.

Zungumza na wataalam walioko katika chama kinachohusika na hati miliki za kazi za wasanii - COSOTA au wanasheria waliobobea katika maeneo na kazi hizo, watakupa mwanga mpana zaidi.

Kundi lingine ni linalolinda ubunifu wa majina, nembo na alama za biashara. Yaweza pia kuwa ‘logo’ ama kauli mbiu. Mathalan, kaulimbiu za kibiashara au kisiasa (motto) kama ‘IPP Cares for You’ ya kampuni ya IPP au ‘Hapa Kazi Tu’ ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, zimewahi kuvuma sana nchini na zinamtambulisha kirahisi yule anayehusika katika jitihadaza zake za kujitofautisha na wengine.

Inamaanisha kuwa, kaulimbiu hizo zinaweza kusajiliwa, ili mtu au taasisi nyingine isitumie pasipo ridhaa ya mmiliki.
Tuseme tu kwamba, hakuna sheria inamkulazimisha mtu au mfanyabiashara asajili alama fulani ya biashara kama vile nembo na kadhalika.

Na kwa vile sheria hukua na kubadilika kila siku, inawezekana kabisa, yapo maeneo ambayo mfanyabiashara au mtoa huduma, akashurutishwa kufanya hivyo.

Iiwapo hiloi lipo, basi ni katika maeneo machache sana na litakuwa eneo lenye tofauti ndogo sana kutoka kanuni ya jumla na iliyozoeleka na wengi (Exception to the General rule) kwamba kusajili mambo hayo ni suala la hiari lisilohitaji shuruti. Labda tufafanue kidogo hapa.

Kabla ya mfanyabiashara kujikita katika uuzaji wa bidhaa (vocha za simu, magazeti, chakula, duka, uuzaji magari, n.k) ama biashara ya kutoa huduma (mathalan usafirishaji wa abiria, utabibu, ufundishaji wanafunzi, au kutoa ushauri kwa fedha), basi ni lazima kwanza asajiliwe na mamlaka husika za serikali (yaweza Kuwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, na kwingineko).

Kwa mfano, mtu akitaka kujihusisha na uchimbani na uuzaji wa madini, itabidi kwanza asajiliwe na kupata hati safi kutoka kwa mamlaka husika kama vile Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela), Kamishna wa Madini, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Leseni ya biashara katika halmashauri husika au moja kwa moja kutoka viwanda na biashara, na kadhalika.

Tuchukulie sasa umeshakidhi matakwa yote hayo na ukaanza biashara, zipo changamoto kadhaa ambazo mara moja hujitokeza na ambazo zitakulazimu uwe na hekima ya kuisajili (kama ni moja) au kuzisajili (kama ni zaidi ya moja).

Nembo au alama fulani ambazo zitakusaidia kuitambulisha biashara yako iliko nchini, na hata katika soko la dunia. Basi mada hii ndiyo inahusika hapa.

Labda waweza kujiuliza: Kuna faida ama hasara zipi za kusajili au kuchelea kusajili nembo na alama za biashara ninayoimiliki.

Pia inaweza kuwa jukumu nililopewa kuhakikisha biashara inanawiri (hapa yawezekana ni kijana wa kiume au binti aliyeamniwa na mzazi wake kusimamia raslimali za familia).

Faida zipo nyingi na vivyo hivyo hasara. Hatutazungumzia hasara, kwa sababu iwapo tunazitaja faida, basi hasara ni kinyume cha kukosekana kutumika kwa fursa zinazoweza kuleta faida zilizoainishwa.

Faida kuu ya kusajili alama ya biashara ni kuitambulisha kwa haraka na uhakika zaidi biashara yako. Wataalam wa masuala haya (Branding Experts) wanatueleza kuwa, bidhaa au huduma inayofanikiwa na kuleta faida kubwa ni ile iliyo bora kuliko nyingine, inayotolewa kwa kuwajali wateja, na zaidi ni ile yenye vitambulishi mahsusi, vinavyoifanya isimame peke yake sokoni.

Pia ni zile zilizo rahisi kukumbukwa na mteja wa nyuma na pia yenye uwezo wa kumshawishi mteja mpya kuisogelea pale ilipo.

Alama za biashara kama nembo za kibiashara (logos) na hata jina lenyewe hucheza nafasi kubwa katika kuifanya baishara fulani isisahaulike haraka miongoni mwa wana-jamii walioizunguka.

Baadhi ya mifano ya makampuni ambayo nembo zao za biashara zinafahamika sana ni kama Coca-Cola (soda); Pepsi Cola (Soda), Toyota (magari); Mercedes Benz (magari), Oxford na Longman n (Uchapishaji/Vitabu), Boeing (ndege), CNN (Televisheni), ITV (televisheni), Nike na Adidas (Viatu), Sony (Bidhaa za Electroniki); Microsoft na Dell (Kompyuta); BP (Mafuta ya Petroli na vilainisha mitambo), Hyatt, Holiday-Inn na Days-Inn (Mahoteli), Western Union na Money-Gram (Utumaji fedha kimataifa kwa haraka), VISA na MASTERCARD (Kadi za plastiki zenye kubeba fedha ndani yake badala ya kubeba lundo la minoti) na kwa sasa hapa Tanzania, huduma kama M-PESA.

Yawezekana kabiasa umewahi kutumia moja ya huduma hizi lakini fahamu pia kuwa hadi kufika hapo zilipo kanuni hizo ziliwekeza mamilioni ya fedha, miaka mingi, na ujasiri na uboreshaji wa mikakati kiasi cha kufikia kiawngo cha juu kabisa.

Pia kutambulika haraka, kukua kwa kasi na kujipatia maelefu (kama si milioni) ya wateja. Baada ya maelezo hayo, yatafakari tena majina na alama za biashara (zikiwemo nembo) za kampuni haya.

Utaona kuwa alama za biashara za makamouni haya zimetengenezwa kwa fundi na ubora wa hali ya juu na wamiliki walitumia kiasi kikubwa cha fedha kuandaa tu alama hizo, jambo ambalo kwa wafanyabiashara tusio na upeo hatuthubutu kulifanya kwa kisingizio cha kukosa mtaji, japo ungeweza kuanza na logo hata ya laki 1 (100,000/=) na bado ikawa nzuri tu kuitambulisha biashara yako.

Faida nyingine ya kusajili alama hizo (kama majina na maumbnile yake katik ukubwa na fonts (maumbile ya herufi) maalum za kompyuta ama za kuchora), picha na nembo (logo) ni kwamba zinasaidia sana mmliki wa kamouni/bidhaa/ama huduma kuilinda biashara yake dhidi ya makampuni yanayokuja baadaye kutaka kuvuna kwa kupitia mgongo na jitihada za huyu aliyetangulia.

Katika Sheria za Hakimiliki yapo mashauri mengi tu yaliyofikishwa mahakamani na pia kutolewa hukumu kuhusiana na udanganyifu unapotokea, kampuni fulani hujaribu kuteneneza bidhaa inayofanana na yule aliyetangulia.

Pia, katika kuangalia kama bidhaa ama huduma imefikia kiwango cha juu cha ubora na kukubalika na wengi kiasi cha wafanyabiashara wengine wanaokuja baadaye kutaka kuinakili kwa faida zao.

Mara nyingi ghiliba hutokea ambapo mchakachuaji anayedurufu bidhaa ya mwingne, hufikia hatua ya kusajili jina linalofanana na yule wa awali na kisha kupeleka katika soko (madukani/mitaani) bidhaa ambayo watumiaji wasipokuwa makini huweza kuamini kuwa wananua bidhaa ile ile waliyoizoea. Dhana hii huitwa ‘Passing off’ katika Sheria zinazohusika na wizi wa kazi za ubunifu zilizofanywa na wengine.

Ndiyo maana basi utaona kwamba ni vizuri sana ukaisajli biashara yako ama bidhaa yako ili kukulinda dhidi ya hujuma hizi.

Hii ni hasa pale ambapo biashara yako inakua kwa kasi ama imeshashamiri na unaamini kwamba inashika usukani ama inakaibia kushika usukani katika soko la ushindani.

Haijalishi kama ni mabasi, huduma kwa watalii, unga wa mahindi, korosho zilizobanguliwa, juisi ya maembe, na kadhalika.

Na kwa wanaoanza, usajili ni muhimu kwa sababu utaitambulisha haraka zaidi biashara yako. labda nikuulize? Bila kuwa na nembo ama alama nyingine ama jina la kuvutia la biashara, biashara yako unaamini imefanikiwa kiasi gani?

Tuishie hapa ila makala yanayokuja tutaangalia ni wapi unasajili mambo hayao na taratibu gani unapaswa kuzifanya kishera.

*Denis Maringo ni Mwanasheria/Wakili wa kujitegemea aliyeko jijini Dar es Salaam. Simu: 0719270067. Barua-pepe: dnmaringo@gmail.com