Bandari Bagamoyo hapana jenga ‘airport’

06Mar 2016
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
Bandari Bagamoyo hapana jenga ‘airport’

SABABU za kujenga bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani zina maswali mengi na magumu.Uvumi kuhusu yaliyomo kwenye mkataba wa mradi huo ambao ungegarimiwa na China unaibua mambo mengi ya kutisha yasiyo na majibu.

BANDARI YA BAGAMOYO ITAKAVYOJENGWA

Kungekuwa na wawakilishi makini bungeni wa kuhoji maswali yafuatayo kuhusu mradi huo huenda serikali isingekuwa na majibu ya kutosheleza kutokana na hoja nyingi kutojibikika.

Licha ya kwamba serikali imeuweka kando ujenzi huo ni budi kujiuliza ninini sababu ya msingi ya kuingia kwenye ujenzi huo unaogarimu pesa nyingi mahali ambapo ni umbali wa kilometa 61.1 kutoka bandari ya Dar-es-Salaam, kilometa 43.07 kutoka bandari ya Zanzibar na kilometa 272 jirani na bandari ya Tanga.

Kutoka Bagamoyo hakuna miundo mbinu ya reli (inayohitajika zaidi ili kuunganisha shughuli za bandari) na hivyo kuleta gharama nyingine kubwa ya za ujenzi wa reli hiyo.

Kwanini kujiingiza kwenye gharama za kujenga vyote, bandari na reli, wakati kutoka Dar-es-Salaam na Tanga miundombinu hiyo ipo ? Mtwara inakosa kimoja ambacho ni reli kwa nini tusiweke nguvu ya kujenga reli kutoka Mtwara kuiunganisha na ile ya Mamlaka Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara )au reli ya kati ama ikiwezekana zote mbili?

Kina cha maji Bagamoyo ni kifupi mno kufanya pasifae kwa bandari. Kwa nini serikali igharimike kukiongeza ili bandari hiyo iwepo ? Mbona Mtwara ni moja ya bandari chache barani Afrika zenye kina kirefu cha asili kinachofaa kwa bandari na wote mnalifahamu hilo?

Ndiyo maana jitihada zinahitaji kuiimarisha bandari hiyo ili iwe bora zaidi na siyo kuingia kwenye kazi ngumu ya kulazimisha kupata bandari Bagamoyo.

Kuhusu mkataba huo wananchi wanaogaramia ujenzi huo kwani watalipia deni kwa njia ya kodi, wanajiuliza je ni kweli Wachina watapewa mamlaka ya kuiendesha kwa miaka 50 huku Watanzania na serikali yao wakikatazwa kuhusika kwa lolote linalohusu kitega uchumi hicho?

Je ni kweli kwa muda wote hakutakuwa na shughuli kwenye bandari yoyote ile kati ya hizi zilizoko Dar, Mtwara, Tanga na Zanzibar?

Kama kipengele cha kwanza ni cha kweli, huu ni uwekezaji au ukoloni mkongwe? Si kwamba meno ya tembo, magogo yetu na madini yetu vitapitishwa hapo kama mali za Wachina? Kama makubaliano hayo ni ya kufidia gharama za ujenzi,kulikuwa na ulazima gani kujenga bandari hiyo?

Nini mantiki ya kipengele cha pili cha kuzuia bandari nyingine zisifanye kazi? Tena ndani ya miaka hiyo 50 na baada ya hapo inakuwaje? Watu wangapi watakosa kazi na mashine pamoja na vitendeakazi vitafidiwa na nani baada ya kuharibika?

Kwa bahati mbaya wawakilishi wetu huongea mengi si kwa maslahi ya nchi bali kwa kujijenga binafsi, kuwabana wasiowataka, kuwalegezea wanaowataka na kupigania vyama vyao vizidi kubaki madarakani.

Wangekuwa kimaslahi ya nchi zaidi, wangehoji hayo ya bandari ya Bagamoyo. Ninaomba nichukue jukumu lao kwa kuishauri serikali ieleze ukweli kuhusu uvumi wa vipengele vya mkataba wa mradi huu na kama ni vya kweli, ieleze mantiki ya yake Aidha, ieleze, kwa kuridhisha, sababu ya kuanzishwa kwa mradi huo Bagamoyo.

Inawezekana maelezo yakawa umaarufu wa mji wa Bagamoyo kisiasa na kihistoria,kunakoufanya uwe wa kitalii. Kama ndivyo, basi kuna mantiki kubwa kujenga uwanja wa ndege mkubwa wa kimataifa wa Bagamoyo na kuachana na habari ya bandari.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar-es-Salaam uko mjini mno na si kawaida duniani kwa viwanja vikubwa vya ndege kujengwa katikati ya jiji kama ilivyo kwa Dar-es-Salaam.

Njia ya kutatua changamoto hiyo ni kupata eneo kubwa mbali na kujenga uwanja mkubwa wa ndege na Bagamoyo patafaa.
Kwanza, ni mbali na pili umaarufu wa Bagamoyo kihistoria na hivyo kuwa eneo la utalii.

Kadhalika Bagamoyo iko jirani na maeneo kadhaa ya kitalii kama mbuga ya Saadani , ni si mbali na Mikumi na hifadhi ya Udzungwa zote za mkoani Morogoro. Yapo mapango ya Amboni mkoani Tanga.

Mwisho, ni uhakika wa kupata heka nyingi zitakazozungushiwa uzio kuwa za uwanja wa ndege utakaofanyiwa upanuzi.

Mtu akikuuliza kuhusu tija ya kiuchumi ya mradi huo wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bagamoyo anaweza kuwa na majibu milioni lakini akikuuliza faida ya kujenga bandari Bagamoyo hutakuwa na nusu jibu!

Najua kuna watakohoji umuhimu wa mradi huo wa uwanja wa ndege wakati tayari kuna uwanja mkubwa jijini Dar-es-Salaam.

Hao ni wale wanaoiona Tanzania kufikia mwisho, wao wakiondoka duniani. Hawajui kuwa huo utakuwa mradi wa kudumu miaka mingi ijayo. Mbona hata bandari tunazo? Kama itaonekana la uwanja wa ndege Bagamoyo ni gumu kutekelezeka, la bandari ndilo halitekelezeki zaidi.

Kuna uwezekano mkubwa uamuzi wa kuwa na “bandari ya Wachina” Bagamoyo ni wa wachache huku wengine wakiogopa kukosoa kutokana na uzito wa hao wachache.

Kama ni hivyo, tuache kuamua mambo makubwa ya wananchi kwa kuogopana. Acha bandari, jenga uwanja wa ndege Bagamoyo.