Malinzi aliyasema hayo wakati akitoa salama zake za kufunga mwaka kwa wadau wa soka nchini, akieleza kuwa hakuna hata klabu moja inayoshiriki ya Ligi Kuu Bara (VPL) msimu huu iliyo na sifa za kuitwa klabu ya Ligi Kuu.
Kiongozi huyo wa juu wa soka nchini, alisema kuwa licha ya kuziagiza klabu kukamilisha taratibu za kanuni mpya ya Leseni za Klabu (Club Licensing), hakuna hata klabu moja iliyotekeleza agizo hilo.
“Tumeshatoa fomu kwa klabu zote za Ligi Kuu, wajaze ili tuwapatie leseni, lakini hadi sasa (jana saa 5 asubuhi) hakuna hata klabu moja iliyofanya hivyo,” Malinzi alisema.
“Watanzania wasishangae watakaposikia Yanga na Azam zimeondolewa na CAF kwenye mashindano ya Afrika mwakani. (CAF) wameshaagiza kila klabu ya Ligi Kuu lazima ikidhi matakwa ya kanuni ya ‘Club Licensing).
“Muda wowote wanaweza kuja hapa (Tanzania), na siku hizi wana utaratibu wa kufanya ukaguzi wa siri, wataona klabu hazina sifa za kuitwa klabu za Ligi Kuu.”
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana visiwani Zanzibar Juni 20 mwaka huu, ilipitisha Kanuni za Ligi msimu huu na kusisitiza kuwa hakuna klabu itakayopitishiwa usajili wake kama haina leseni ya klabu, agizo ambalo linaonekana wazi kupuuzwa.
‘MURO, MANARA WAFUNDWE’
Malinzi alizungumzia pia malumbano yaliyoibuka hivi karibuni kati ya wasemaji wa Simba na Yanga, Hajji Manara na Jerry Muro, akiiagiza Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF kuandaa semina ya ‘kuwafunda’ maofisa habari wa klabu za soka nchini.
Rais huyo pia alieleza kuwa mwakani kutakuwa na michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake, huku akiahidi pia kutakuwa na mashindano ya Copa Coca-Cola na udhamini mpya wa michuano mbalimbali ya soka nchini.
Huku akizimwagia pongezi taasisi na kampuni mbalimbali zilizojitokeza kuusaidia soka, Malinzi alisema TFF imenunua vifaa vingi vya michezo ikiwamo mipira 5,000 kwa ajili ya watoto.
MIL 250/- ZILIZOKATWA TRA
Malinzi pia alisema wanaendelea kuzungumza na serikali ili iwarudishie Sh. milioni 250 ilizozichota kwenye akaunti za TFF hivi karibuni kutokana na shirikisho hilo kupatikana na hatia ya kukwepa kodi inayofikia Sh. bilioni 1.6.
Kiongozi huyo pia alisema wanaendelea na mchakato wa kusaka mshauri mwelekezi (consultant) wa mfumo wa tiketi za kielekroniki uliositishwa licha ya Bunge la Tanzania kuiagiza Mamlaka ya Masoko Tanzania (TRA) kuhakikisha inaisimamia TFF kutumia mfumo huo wa kisasa kwenye viwanja vyote vya soka nchini.
“TUPENI UMITASHUMTA, UMISSETA’
Malinzi pia aliiomba serikali kuikabidhi TFF kusimamia mchezo wa soka katika mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari nchini (Umitashumta na Umisseta) kwa kuwa “katika miaka ya karibuni yameshindwa kutoa kina Leodegar Tenga wengine” kutokana na kile ambacho Malinzi alisema kukosekana kwa ufanisi katika uendeshaji.










