Singano amvimbisha kichwa Stewart Hall

31Dec 2015
Nipashe
Singano amvimbisha kichwa Stewart Hall

BAADA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na kuing'oa Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacaom Tanzania Bara (VPL).

Ramadhani Singano 'Messi'

juzi, kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amemwagia sifa watokeo benchini Ramadhani Singano 'Messi' na Mudathir Yahaya akidai 'ndiyo waliomaliza mchezo'.

Azam, mabingwa wapya wa Kombe la Kagame, waliipata ushindi huo mgumu dakika za mwisho dhidi ya mabingwa hao mara mbili wa Tanzania Bara (1999 na 2000) katika mechi ya kiporo ya raundi ya sita iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam. Shukrani kwa goli la faulo ya nahodha John Bocco lililomfanya afikishe magoli sita msimu huu.
Matokeo hayo yameonekana 'kumvimbisha kichwa' Hall ambaye jana alitamba kuwa mabadiliko aliyofanya kipindi cha pili ndiyo yaliyochochea machozi ya 'Wakatamiwa wa Manungu'.
“Kuingia kwa (Ramadhani Singano) Messi na Mudathir (Yahaya) kulifanya tucheze vizuri sana kwenye sehemu ya kiungo, wote walisaidiana vizuri na (Salum Abubakar) Sure Boy. Kipindi cha kwanza tulipwaya, Mtibwa ilitunyima nafasi ya kucheza,” alisema.
Dakika tano kabla ya saa ya mchezo, Hall alimtoa winga mwenye chenga za fedheha, Farid Mussa na kumwingia Singano, kabla ya nafasi ya kiungo Frank Domayo kuzibwa na Mudathir dakika saba baadaye.
Muingereza huyo alisema ana furaha kubwa kuiongoza Azam FC kuumaliza mwaka 2015 wakiwa kileleni kwenye msimamo wa VPL huku akitamba kuwa hiyo "ni dalili nzuri kutwaa ubingwa, lakini kuna kazi kubwa kufikia mafanikio hayo".
Singano alisajiliwa na Azam hivi karibuni baada ya kuingia katika mgogoro wa kimaslahi uliosababisha kuvunjika kwa mkataba wake na klabu ya Simba.