"Wanawake kuongea na kujiamini kwa kiasi kikubwa ni muhimu katika kupambana na VVU/Ukimwi," Chitongo kiongozi wa jamii anayepambana kupatia uwezo wa kulinda jamii nchini Zimbabwe na kiongozi wa kitaifa wa shirika la "Groots Zimbabwe Home-Based Care Alliance", aliiambia IPS.
Unyanyasaji wa majumbani unaongeza moja kwa moja nafasi ya kupata maambukizi ya magonjwa ya ngono ambao yanafanya wanawake kuambukizwa VVU.
"Kama wanawake wanatoa sauti zao kiasi cha kutosha, wanakuwa na uwezo wa kujadili kuhusu kufanya ngono salama kama wapenzi sawa na wala siyo wanaokandamizwa," Chitongo alielezea.
Mwandishi wa habari wa IPS Julia Kallas alizungumza na Chitongo kuhusu uhusiano kati ya unyanyasaji wa kingono na VVU/Ukimwi na jinsi gani jitihada za wanawake katika ngazi ya chini kabisa katika jamii zinaweza kukuza huduma za VVU na kusaidia wagonjwa.
Swali: Mwaka 2005, kesi yako ya unyanyasaji majumbani ilivutia vyombo vya habari kitaifa na pia ulikuwa ukionewa huruma. Ni kitu gani kilikushawishi kuanzisha shirika la "Ray of Hope na kusaidia wanawake wenye VVU?
Jibu: Kuanzishwa kwa shirika la "Ray of Hope" kunaanzia mwaka 2005, wakati nilipoona makala ya video katika kipindi cha TV na kujifunza kuwa shirika la "Girl Child Network" lilikuwa likitoa mikopo kwa wanawake chini ya Mpango wa Maendeleo na Kuwezesha Jamii.
Kwa kuliona hili kama fursa pekee ya kujinasua na unyanyasaji wa majumbani, ambako nilidhani kumetokana na utegemezi wa kiuchumi kwa mume wangu, niliamua kuifuata GCN.
Wafanyakazi wa shirika hilo walinipeleka kwa mwanamke anayeitwa Betty Makoni, wakati walipoona kesi yangu ilikuwa hatari sana kwa wao, kwa kuwa mume wangu alikuwa anatumia sana nguvu na hakufuata sheria.
Betty aliguswa sana na hadithi yangu na ya watoto wangu watatu, ambao waliishia mitaani wakati nilipokuwa najificha kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu katika nchi jirani ya Botswana.
Hapo kabla, nilifuata mashirika kadhaa ya wanawake na watekelezaji wa sheria bila mafanikio na hivyo kupoteza matumaini. Hata ndugu zangu wa karibu waliogopa kunipatia hifadhi katika makazi yao. Lakini Betty alinipatia hifadhi katika eneo la kijijini la Mutasa.
Wakati naishi huko, mwanamke wa eneo hilo aliuawa kikatili na mume wake mbele ya macho ya watoto wake watatu na kulikuwa na kesi ambazo hazikuripotiwa. Kwa msaada wa Betty nilipata hamasa kushawishi wanawake wengine waliopatwa na unyanyasaji wa majumbani kuanzisha kikundi cha kuwasaidia, ambacho kilitoa nafasi ya kuzungumza kuhusu matatizo yao wakiwa mbali na wanaume zao.
Matokeo yake ni kuongezeka kwa kasi kwa wanawake waliomiminika wakiwa na habari za kutisha kuhusu unyanyasaji. Wanawake walisafiri zaidi ya kilomita 30 wakiwa hawana viatu ili kuja kuelezea mizigo waliyokuwa nayo kwa muda mrefu.
Kitu kilichokua kikiumiza kwa wanawake hawa waliokuwa na matatizo ni kwamba hawakupatwa na unyanyasaji wa majumbani pekee lakini pia na watoto wao. Jambo la kusikitisha watoto wao ni sababu kuu ambayo iliwafanya kunyamaza kimya bila kusema kitu katika uhusiano uliokuwa ukitishia maisha yao.
Mikutano hii ilibadili wanawake. Waligeuka kuwa wakimya na kuwa kikundi ambacho kilikuwa na nia ya kubadili maisha.
Katika moja ya mikutano yetu, tuligundua kuwa robo tatu ya wanawake hao katika kikundi, ambacho kilikuwa na wanachama zaidi ya 100, walikuwa wanaishi na VVU na kuwa karibu wanachama wote wako katika kazi za kutunza wagonjwa wa Ukimwi katika ngazi za chini au za kati.
Ndipo tukakubaliana kuwa kila mpango ambao tutakwenda kutekeleza unatakiwa kuingiza suala la VVU/Ukimwi.
Kinachohitajika ni kuanzishwa kwa sera za makusudi katika ngazi ya kitaifa kupatia wanawake upatikanaji wa teknolojia ya habari inayostahili kueneza taarifa za VVU/Ukimwi. Kuanzisha vituo vya habari katika ngazi za vijijini na nje ya miji kungesaidia kuwapatia wanawake fursa ya kupata habari hizo.
Watu pia wanapaswa kujikusanya katika vikundi na kutaka kutumia kompyuta na vifaa vingine vya Tehama.










