Mshindi wa Taifa Kidato cha Nne 2015

23Feb 2016
Romana Mallya
Dar
Nipashe
Mshindi wa Taifa Kidato cha Nne 2015
  • *Ameongoza siku zote, isipokuwa ‘siku moja’

"Butogwa Shija hapendi kushindwa. Hataki mtu ampite, kama alivyoeleza. Alilia wakati huo akiwa darasa la tano. Ni kweli nakumbuka nilitoka ofisini nikamkuta analia baada ya wenzake kumcheka kuwa amefeli. Pia ni mtoto anayependa kutimiza malengo yake.

Butogwa Shija akiwa na mama yake.

Mara kwa mara hutuambia anasoma kwa nguvu zote, kwa sababu amepata taarifa kuwa, watoto wanaofanya vizuri wanapata udhamini," Angela Shija, mama mzazi wa mshindi wa jumla wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne 2015 aliyasema hayo baada ya matokeo kutangazwa hivi karibuni.

Butogwa amepata matokeo hayo akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam ambaye kwa kauli yake anasema;

“Safari yangu ya ushindi haikuanza leo, toka utoto wangu nimekuwa mtu ninayependa kutimiza malengo yangu kwa vitendo. Sijali kama kuna vizingiti mbele yangu.

Nikipanga jambo lazima nilitimize. Lakini yote haya hayawezi kutimia kwa nguvu binafsi, bali kwa kushirikisha wale wanaokuzunguka,”anasema mshindi huyo wa jumla wa mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2015 , Butogwa Shija (17).

Butogwa akizungumza katika mahojiano maalum nyumbani kwao Kipunguni B, kata ya Kiluvya, jijini Dar es Salaam, alisema anaamini kuwa, ushindi wake licha ya kujisomea mwenyewe kwa bidii, lakini wanafunzi wenzake nao wana mchango mkubwa kwenye mafanikio hayo.

Matokeo ya mtihani huo, yalitangazwa mwishoni mwa wiki na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), na kuonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa asilimia 1.85 ikilinganishwa na mwaka 2014. Matokeo yanaonyesha kuwa, wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 25 na waliopata daraja la nne na sifuri ni asilimia 74.66.

Watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa ni 394,065, lakini waliofanya mtihani ni 384,300 (asilimia 97.52) wasichana wakiwa 195,413 (asilimia 97.22) na wavulana 188,887 (asilimia 97.83). Watahiniwa 9,765 sawa na asilimia 2.48 hawakufanya mtihani.

Mwanafunzi huyo Butogwa ambaye ni kinara wa matokeo hayo juzi (Jumapili) alisherehekea siku yake ya kuzaliwa, anasema kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ni kusoma kwa bidii kila wakati bila kuchoka.

“Akili ya binadamu huwa zinasahau, ndivyo zilivyoumbwa na Mungu. Lakini kwa sababu nilikuwa najua nini nataka… nini natafuta nilipokuwa shuleni wakati wote niliutumia ipasavyo kujisomea,” anabainisha.

Ratiba yake ya masomo
Butogwa aliishi bweni shuleni hapo, anaamini kuwa kamwe mtu hawezi kufanikiwa ikiwa atashindwa kuipangilia ratiba yake ya siku nzima ya maisha yake.

“Uwe mwanafunzi, mfanyakazi, mama wa nyumbani, mkulima kama kuna malengo umejiwekea, huwezi kuyatimiza ikiwa ratiba yako ya siku hujaipangilia. Lazima ujipe muda wa kufanya mambo mengine na muda wa kupumzika,” anasema na kuongeza:

“Shule yetu imetupangia ratiba nzuri, ambayo tuna muda wa kujisomea binafsi, makundi na wanafunzi wawili wawili kwa anayejua zaidi na anayehitaji msaada wa kujua asivyovijua. Hii imenisaidia sana kusoma na kujua vitu vingi ambavyo sikuvitarajia,”anabaisha.

Butogwa chakula anachokipenda ni ugali kwa maharage, anasema anapokutana na wenzake kwenye makundi hujadili mada mbalimbali za masomo na kujiweka vizuri zaidi.

Kwa upande wa walimu anasema kwamba, wametumia utaratibu wa kuwapanga wawili wawili kwa anayejua zaidi ya mwingine lengo ni kusaidiana kuinua uwezo.

“Hii ya kutugawa wawili wawili imenijenga zaidi, kwa sababu unapofanya majadiliano na mtu asiyejua zaidi yako, anakuwa na maswali mengi ambayo yanakufanya usome kwa bidii ili umuelewezeshe. Nilikuwa na Martha Ng’omu ambaye amenisaidia sana kujifunza vitu vingi ili nimueleweshe kile alichokuwa hakijui. Namshukuru Mungu kwamba naye ana ufaulu wa daraja la 1.14, wakati mimi nina 1.7,” alifafanua.

Butogwa ambaye ni mtoto wa mwisho katika familia yao, akiwa na dada yake, Ilacoze Shija anayesomea Computer Science Engineering.

Kimsingi anaamini kuwa mafanikio hayo yametokana na ratiba nzuri waliyojipangia na mwenzake baada ya darasa wajadiliane kimakundi na baadaye wawili wawili.

“Bila ratiba kama mwanafunzi, utajikuta unasoma mambo ambayo baadaye utashindwa kufanya vizuri katika mitihani kwa sababu utafika muda wa mitihani mambo mengine ukawa hujasoma,” anasema.

Pia anasema, shule hiyo imekuwa ikitoa mazoezi mengi na mitihani kila mara na mwisho wa siku wamekuwa wakipewa matokeo ya kile walichokipata ambacho ndicho kinachowatia moyo wa kuongeza bidii zaidi.

Anakiri ushindi wake pia umechangiwa na ratiba nzuri ya nyumbani kwao aendapo likizo, ambayo ilipangwa kwa kuzingatia urefu wa likizo.

“Kama likizo ni fupi, zile kazi za shule nilizopaswa kuzifanya nyumbani nilizigawa kwa kuzingatia kutoichosha akili,” anasema.

MATARAJIO
Butogwa anasema kwa sababu alitarajia ushindi huo kutokana na miaka yake yote akiwa shuleni hakuwahi kujibweteka, anaamini safari yake ya kuutumikia umma kupitia taaluma ya udaktari inaelekea kutimia.

Mwanafunzi huyo anabainisha kuwa, ndoto yake ni kuchukua taaluma hiyo kupitia Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani.

Mara zote anabainisha amekuwa akiwahimiza wazazi wake wamlipie ada kwa kipindi hicho, ili afanye vizuri kimasomo na baadaye aweze kupata udhamini atakapoingia chuoni hapo.

“Nataka kusomea udaktari. Napenda kuwatumikia watu naamini kupitia taaluma hii, nitatimiza ndoto yangu. Tayari nilishaanza kuifanyia kazi. Shuleni wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniamini… wakiumwa walikuwa wanakuja kwangu kuomba ushauri na kuwapa dawa za kutuliza maumivu,” anasema na kuongeza:

“Nimemaliza shule, lakini nimekuwa nikifanya kazi ya kujitolea kupitia shirika lisilo la kiserikali liitwalo Friends of Children.Tumekuwa tukienda hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukutana na watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na wale wanaotakiwa kunyooshwa viungo vyao. Huwa tunacheza nao na kuwafundisha,” anabainisha.

Anaongeza: “Huwa tunakutana na watoto tunaongea nao na kucheza kuna mtoto aitwaye Abas pale Muhimbili wodini huwa namfundisha somo la hesabu kwa sababu analipenda. Sitaki akose masomo yake eti kwa sababu yupo hospitali anaumwa,” anasema.

Anasema baada ya kumaliza mtihani wake, alikuwa akimtania baba yake anunue suti ambayo ataivaa wakati anamsindikiza kwenda kumshika mkono Rais, Dk. John Magufuli akiwa kama mshindi.

“Matokeo haya niliyatarajia ili nitimize ndoto yangu ya kumshika mkono Rais Dk. John Magufuli nikiwa mshindi wa kwanza kitaifa,” anasema.

Historia yake ya ufaulu
Mshindi huyo anasema tangu alivyojiunga na elimu ya awali katika shule ya Faith kwa sasa Remnant Academy jijini Dar es Salaam alikuwa akishika nafasi ya kwanza.

“Nilivyofika darasa la tano nilihamia shule nyingine ijulikanayo kama Masaka Pre and Primary iliyopo Kipunguni, Dar es Salaam nikiwa darasa la tano nilishika namba tatu darasani. Matokeo hayo yaliniumiza sana … nililia nakumbuka rafiki zangu walinisindikiza hadi nyumbani huku wakinitania,”alibainisha.

“Nisidanganye nilikwazika kwa sababu, hata wenzangu walikuwa wakinicheka kwa maana walinizoea kuwaongoza, changamoto hii ilinipa ari ya kusoma zaidi kwa bidii na tangu hapo hadi namaliza sasa nimekuwa nikishika nafasi za juu, alisema na kuongeza:

“Mitihani yangu yote kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne nilikuwa naongoza. Lakini ipo tuliyokuwa tukiifanya kwa shule zetu inajulikana kama TAHOSA, lakini ni mtihani wa majaribio (Mock), nilishika nafasi pili kishule.

Mtihani mwingine wa Joint Exam Catholic Schools (JECS) tulifungana na mshindi wa pili kitaifa ambaye ni raia wa China, Congcong Wang (16) aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Fezza. Wote tulishika nafasi ya kwanza,” anasema na kuendelea:

"Hadi namaliza sekondari nina vyeti vya ushindi 18 nilivyotunukiwa baada ya kuongoza kwenye mitihani tuliyokuwa tukiifanya mara kwa mara," anaeleza.

Katika mtihani wa mwisho anasema kuwa alifanya masomo 10 ni somo la Uraia pekee ndilo alipata alama B wakati Hesabu, Kiingereza, Kiswahili, Jiografia, Historia, Kemia, Biolojia, Fizikia na Addition Mathematics alipata alama A.

Mchango wa wazazi na walimu
Anabainisha kuwa, wazazi wake wamekuwa mstari wa mbele kwa kumhimiza kila mara asome kwa bidii, na pale anapoanguka wamekuwa wakienda shule kuhoji, hatua ambazo zimemsaidia kumjenga.

“Baba yangu alitujenga na dada yangu kupitia shindano lake linalosema, ‘Tajirika na Baba’ Kila somo moja ukipata alama A ni anakuzawadia Sh. 30,000 na B ni Sh. 25,000. Hii ni kwa mitihani mikubwa kama TAHOSA na Mock, ilinifanya nisome kwa bidii nisikose hela hiyo,” anaeleza.

Kwa upande wa walimu, anasema walikuwa na utaratibu pindi mwanafunzi akifanya vibaya walimuita kumuhoji ili wajue kama kuna tatizo lolote.

“Binafsi iliniongezea ari ya kusoma kwa sababu, niliamini japo nipo shuleni, wapo wanaonifuatilia kama wazazi wangu kwa lengo la kunifanya nifanikishe ndoto zangu,” anasema.

Kuhusu marafiki, mwanafunzi huyu anasema walikuwa na mchango mkubwa katika masomo yake, kwa sababu wakati mwingine kuna baadhi ya vitu ambavyo alikuwa hajavisoma alivipata kupitia majadiliano ya makundi.

“Nawashukuru kwa mchango wao ila kubwa ni wiki ya mwisho kabla ya mtihani huu, niliugua malaria. Nilipopimwa nilikutwa na wadudu wanne. Huwezi amini walinitia moyo na ugonjwa wangu. Walifanya majadiliano ya kikundi mbele yangu ili nisipitwe. Hakika , nilipata vingi kutoka kwao,” anasema.

Wito kwa wanafunzi
Butogwa amewataka wasitumie muda wa mwisho kukaribia mitihani ndio wasome kwa bidii.

"Unapokuwa vitani wakati wote, unatakiwa kuwa tayari hivyo hivyo shuleni kila mara unatakiwa ujiandae kwa mitihani. Kusoma kila wakati kunasaidia kujua vitu vingi, lakini ukisubiri wiki ya mitihani usome utafeli,"anawafunda.

Mama yake mzazi alonga
Akielezea furaha ya ushindi wa mtoto wake, Angela Shija anasema, kutokana na bidii ya kusoma ya Butogwa, alitegemea asingekosa kuwa kati ya wanafunzi tano bora kitaifa.

Angela ambaye kitaaluma ni Mtafiti katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa mtoto wake ni mtu asiyependa kushindwa mara zote na husoma kwa malengo.

"Butogwa hapendi kushindwa. Hataki mtu ampite, kama alivyoeleza. Alilia wakati huo akiwa darasa la tano. Ni kweli nakumbuka nilitoka ofisini nikamkuta analia baada ya wenzake kumcheka kuwa amefeli. Pia ni mtoto anayependa kutimiza malengo yake. Mara kwa mara hutuambia anasoma kwa nguvu zote, kwa sababu amepata taarifa kuwa watoto wanaofanya vizuri wanapata udhamini," anasema.

Angela ambaye mume wake ni Mshauri wa Biashara ana shahada ya pili ya masuala ya maliasili, anasema anamshukuru Mungu kwa kuitimiza ndoto ya mtoto wake.

Anafichua kuwa baba yake tayari amemwandalia hati ya kusafiria ili aende nje akatimize ndoto yake kwa vitendo.