Mpasuko huo, au mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar, unagawanyika katika mafungu mawili makuu mawili. Fungu moja linajiegemeza katika taaswira ya kisheria na kikatiba na jingine limejiinamiza katika sura kamili ya kisiasa kunakohitaji maridhiano na upatanishi.
Makovu ya kisiasa yalikuwa yakizaliwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu kila baada ya miaka mitano kutokana na upinzani wa kisiasa unaoendelea baina ya Chama cha Mapindizi (CCM) na Chama cha wananchi (CUF), tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi Zanzibar mwaka 1992.
Kabla ya kupatikana muafaka na maridhiano kutokana na kazi nzuri iliyokuwa imefanywa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, hali ya kisiasa visiwani ilikuwa mbaya baada ya wananchi kubaguana na kutengana katika shughuli za kijamii ikiwemo misiba, harusi na katika nyumba za ibada.
Hadi kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa yaliopelekea kuundwa kwa SUK, msingi wa mapatano ulianza kujengwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyauko mwaka 1999.
Aidha, Karume na Kikwete historia itawakubuka kwa juhudi walizochukua na kufanikisha kuwaunganisha Wazanzibar na kuwa wamoja katika muda wa miaka mitano, baada ya muafaka na maridhiano ya kisiasa ya mwaka 2009.
Milango ya watu kuchumbiana bila ya kujali tofauti za itikadi ya vyama vya siasa ilifunguka na siasa za chuki na uhasama zikabakia historia. Wahisani pia waliongeza misaada, hatua ambayo ilisadia SUK kufanikisha maradi ya maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Kama wasemavyo waswahili kuwa 'tonge nzuri haifiki mdomoni', SUK imebaki vipande vipande baada ya mawaziri saba na manaibu wake watatu kujivua nyadhifa zao kwa madai imemaliza muda wake wa kubakia madarakani tangu Novemba 2, mwaka jana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Awali, SUK ilianza kuonyesha nyufa na mipasuko pale mawaziri kutoka upande wa CUF walipokataa kupitisha bajeti ya Serikali, wakipinga urasimu wa usajili wa vitambulisho vya Uzanzibari ukazi vinavyotoa fursa ya kusajiliwa kuwa mpiga kura kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Wakati Waziri wa Katiba na Sheria aliyejivua wadhifa Abubaka Khamis Bakar anasema kwa mujibu wa Kifungu cha 28(2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 muda wa miaka mitano wa kubakia madarakani kwa Rais wa Zanzibar ulifika kikomo Novemba 2, mwaka jana, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud anasema Serikali ya Rais Shein bado ni halali kwa mujibu wa Kifungu cha 28(1)(a) cha katiba hiyo hiyo.
Hatua ya CUF kususia uchaguzi mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, imeongeza hali ya wasiwasi kwa wanasheria wa Zanzibar kuwa SUK ipo katika hatari ya kufa iwapo vyama vidogo vilivyojitokeza kushiriki uchaguzi huo vitashindwa kufikia masharti ya kikatiba ya kuunda serikali ya pamoja.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Said Shaban anasema Katiba ya Zanzibar imeweka sharti chama kinachoshika nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi wa rais, kinapewa nafasi ya kutoa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kama kama kitavuka asilimia 10 ya kura zote. Aidha chama hicho hutoa mawaziri kwa uwiano wa viti ndani ya Baraza la wawakilishi Zanzibar (BLW).
Bahati mbaya vyama vilivyojitokeza kushiriki uchaguzi wa marudio, ukiondoa CCM, hakuna kilichowahi kushinda hata kiti kimoja cha udiwani kutokana na nguvu zao za kisiasa kuwa dhaifu, tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi 1992.
Mwanasheria mkongwe Awadhi Ali Said anasema mgogoro mkubwa wa kisiasa na katiba utaibuka iwapo vyama vidogo vitashindwa kufikia mashariti ya kushiriki kuunda SUK kwa sababu CCM watalazimika kuwa na serikali ya peke yao kinyume na Katiba ya Zanzibar.
Anasema hali hiyo italeta mkanganyiko mkubwa kwa sababu serikali ya CCM haitokuwa na nafasi ya kuitisha kura ya maoni ya kubadilisha katiba kutokana na muda wake wa kuwa madarakani kumalizika Novemba 2, mwaka jana.
Nani wa kulaumiwa juu ya hatari inayojitokeza ya kuwepo kwa uwezekano wa kufa kwa SUK baada ya CUF kuamua kususia uchaguzi mkuu wa marudio?
Hakuna sababu ya kumtafuta mchawi. Cha muhimu ni kutafakari na kutafuta muafaka kunusuru uwepo wa serikali ya pamoja kwa kuangalia misingi na madhumuni ya kuanzishwa kwake sasa.
Wakati wa kuziba ufa wa SUK uliotokana na mkwamo wa kiasia kufuatia kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi MKuu ni sasa pia.
Bado viongozi wa vyama vya CCM na CUF wanayo nafasi ya kukaa pamoja na kutafuta njia bora ya kumaliza matatizo yaliyojitokeza bila ya kuweka mbele maslahi binafsi.
Kama viongozi wa vyama hivyo waliweza kusahau yaliyopita katika chaguzi za 1995, 2000, 2005 na 2010 ili kusaidia kuzaliwa kwa SUK, wanashindwa vipi kufumba macho tena kusahau yaliyopita na kumaliza mgogoro wa uchaguzi kwa maridhiano?










