Hao hao wawe madaktari wa falsafa na maprofesa kuzalisha wasomi wa viwango vya juu vya elimu.
Mpango huo, wa muda mrefu, utamaanisha mtu akishaingia kwenye ualimu, atakuwa mwalimu kwa maisha yake yote. Kila taaluma atakayoisomea ataitumia kufundishia wengine taaluma hiyo; sheria, uchumi, uhasibu, uhandisi, sayansi, uandishi wa habari na kadhalika.
Kwa utaratibu huo, taifa litakuwa na Waalimu wa Taifa wa kupanda ngazi za shule za kufundisha isipokuwa kwa wenye utaalam maalum wa kufundisha madarasa ya chekechea na madarasa ya chini.
Wanafunzi wa kidato cha nne watakaofaulu vizuri waingie “A’ level” kupata wataalam wa taaluma nyingine zisizo ualimu na kupata waalimu watakaoanzia kufundisha sekondari za “O’ level” miongoni mwa watakaofaulu kidato cha sita kwa kiwango cha pili. Wahitimu wa kidato cha nne watakaofuatia kwenye kufaulu wataenda moja kwa moja kwenye vyuo vya ualimu kusomea ualimu wa shule za msingi.
Waalimu hawa wawe na mishahara mikubwa na marupurupu ya kutosha, makazi bora kwa shule za vijijini pamoja na motisha kadhaa, kwa mfano, mikopo ya masharti nafuu, posho nzuri za likizo na kutembelea nje ya Afrika kila baada ya miaka itakayoamuliwa kuona waalimu wa huko wa ngazi zao wanafanyaje kazi. Hii ni motisha na pia ni njia ya kujenga uwezo (capacity building).
Kwa sababu waalimu wa shule za msingi walifaulu vizuri, hao watasoma na kufika kidato cha sita. Wataandaliwa kufundisha sekondari. Watafundisha “O’ level”, nafasi zao za ualimu wa shule za msingi zikizibwa na wapya watakaofaulu vizuri kidato cha nne.
Waalimu wa “O’ level” wataenda kusoma kwenye vyuo vya elimu ya juu, nafasi zao zikijazwa na wale watakaopanda kutoka kuwa waalimu wa shule za msingi. Baadhi ya hawa watakaomaliza vyuo vya juu, watakuwa waalimu wa “A’level” na wengine watakaofaulu zaidi watakuwa waalimu vyuoni wakianzia kuwa wakufunzi wasaidizi (tutorial assistants).
Wakiendelea kielimu kwa kusomea taaluma zao mbalimbali chuo kikuu, waalimu hao watafikia kuwa madaktari wa falsafa na maprofesa. Kadri watakavyopanda, marupurupu yataongezeka inavyostahili. Kwa njia hii, nchi yetu itakuwa juu kielimu na itakwenda mbele kimaendeleo kwa sababu kila mahali kutakuwa na waalimu bora, wakiwemo wa vyuo vya ualimu.
Mpango huu utakuwa na tija, pia tukizingatia haya:- Kwanza, tujitahidi kadri tuwezavyo kila mafunzo yanayowezekana kutolewa huku wanafunzi wakiyafanya kwa vitendo, yatolewe hivyo badala ya nadharia kwa kila mafunzo. Hii itawafanya wanafunzi waelewe kwa kina kile wanachopaswa kuelewa.
Pili, tusizame kuwaandaa wanafunzi kufaulu mitihani kwa kuwafundisha muda wote maswali yanayoulizwa mara kwa mara kwenye mitihani na kuwapa majibu. Hapo wanafunzi hufaulu kihalali lakini vichwani wanakuwa hawana ufahamu huo. Huu ni ufundishaji wa kutafuta sifa za kufaulisha zisizosaidia maendeleo ya nchi.
Tatu, tujenge mtazamo wa kujiajiri. Tulenge kule ambako nchi yetu inakusudia kwenda kama ilivyokuwa elimu ya kujitegemea enzi zile za siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Wanafunzi waandaliwe namna ya kujenga ustawi wao na wa taifa kwa kupewa mbinu za kujiajiri kwenye kilimo bora, ufugaji wa kisasa, uvuvi na biashara. Wafundishwe kwa nguvu zote kuchukia maovu kama madawa ya kulevya, rushwa, wizi wa mali ya umma na maovu mengine.
Nne, tusiue vyuo vya taaluma za chini na kujaza vyuo vikuu. Ni lazima tutengeneze piramidi ya idadi ya wasomi wetu kwa maana ya kwamba wenye elimu ndogo wanakuwa wengi kuliko wenye elimu kubwa. Tuhakikishe tunakuwa na wenye diploma, vyeti na kadhalika walio wengi ili tuwe na watendaji wengi badala ya kuua ngazi ya elimu ya chini kutengeneza viongozi wengi wenye shahada moja na mbili watakaokosa ajira na watakaozipata, kukosa watendaji.
Miongoni mwa wenye shahada moja mpaka mbili wa sasa ni watu wasio na uwezo unaoendana na kiwango hicho cha elimu! Tunalazimika kulazimisha hata wasio hodari kwa masomo kupata shahada kwa sababu mazingira ya sasa yanalazimisha jambo hilo. Tusiue vyuo vya chini ili wenye uwezo wa ngazi hizo waishie huko, wawe watendaji wazuri.
Tano, wanafunzi wa sekondari za juu waanze kufundishwa sheria kama za jinai, katiba na mikataba kwa wale wa masomo ya sanaa, na sheria za mikataba kwa wale wa masomo ya biashara. Wapewe tu uelewa wa sheria hizo na si kuwafundisha kwa kiwango cha cheti cha sheria, diploma au shahada.
Mwisho, tujifunze lugha za wengine wanaochachamaa mno kujifunza lugha yetu kiswahili. Tukifanya mchezo ajira zote zinazohusu lugha yetu na lugha nyingine duniani zitakuwa za wenzetu tu. Hizo ni kama ukalimani kwenye mikutano mikubwa ya kimataifa, ualimu wa kiswahili kimataifa na utangazaji wa idhaa za kiswahili za kimataifa.
Ajira hizi huhitajika utaalam wa kiswahili na wa lugha nyingine kama kiingereza, kifaransa na nyinginezo.










