RIPOTI MAALUM: Wagonjwa watoroka MOI kukimbia madeni

20Feb 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe
RIPOTI MAALUM: Wagonjwa watoroka MOI kukimbia madeni

TAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI) inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwapo kwa wagonjwa wanaotoroka hospitalini hapo kukwepa madeni, imefahamika.

Wagonjwa wanaotoroka madeni katika taaisi hiyo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamekuwa wakilalamikia kuwapo kwa gharama kubwa za huduma ya matibabu.

Vitendo hivyo vinavyofanywa na wagonjwa wanaokuwa tayari wameshapata huduma huuweka katika wakati mgumu uongozi wa MOI, ambao hulazimika kuwa na jukumu la ziada kukabiliana na matatizo ya kifedha yanayotokana na kutolipiwa kwa huduma zitolewazo zikiwamo za vipimo, dawa na upasuaji.

Wiki iliyopita, Nipashe ilibaini kuwa baadhi ya gharama za matibabu yanayohusisha upasuaji katika taasisi hiyo huwalazimu wagonjwa kulipia mpaka Sh. milioni 10 kwa upasuaji wa nyonga. Gharama kwa ajili ya ufunguaji wa jalada kwa mgonjwa huwa ni Sh. 50,000.

Hata hivyo, wakati baadhi ya wagonjwa wakitoroka kukwepa madeni ya huduma wanazopewa na taasisi hiyo ya umma, Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othman Kiloloma, alisema gharama zinazotozwa katika taasisi hiyo ni za chini mno kulinganisha na hospitali nyingi binafsi.

Katika hospitali hizo, alisema, upasuaji kama wa nyonga huhitajika dola za Marekani 15,000 (sawa na Sh. milioni 32).
Uchunguzi wa Nipashe umebaini gharama za matibabu zinazotozwa na MOI ni za chini kulinganisha na hospitali nyingi binafsi.

Hata hivyo, baadhi ya wagonjwa walisema kiwango cha ada ya huduma MOI kinaonekana ni kikubwa kwa walio wengi kutokana na hali yao kiuchumi kuwa duni na hivyo, baadhi yao hutoroka wanapojiona wamepata nafuu.

Kwa mujibu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wastani wa kipato kwa kila Mtanzania katika robo ya pili ya mwaka 2015 kilikuwa Sh. 1,828,022 kwa mwaka, sawa na Sh. 5,000 kwa siku.

“Kwakweli hali ya ulipaji huduma kwa baadhi ya wagonjwa ni ngumu… wengine huishia kutoroka na hili siyo jambo zuri. Serikali ingalie namna ya kupunguza zaidi gharama hizi za matibabu MOI,” alisema mmoja wa watu waliozungumza na Nipashe.

Akizungumzia na Nipashe, Msemaji wa MOI, Almas Jumaa, alikiri kwamba malipo ya matibabu kwa wagonjwa ni changamoto kubwa kwao kwani baada ya kuhudumiwa, baadhi hugoma kulipia ankara wanazopewa na wengine hutoroka.
Kadhalika, alisema kuna matukio mengi ya wagonjwa wanaoruhusiwa kutoka baada ya kupata nafuu kutorejea tena kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi afya zao na wengi hufanya hivyo kukwepa wajibu wa kulipa deni.

“Kuna wagonjwa wengine wakisaidiwa na ndugu zao huwa wanatoroka baada ya kupata nafuu," alisema Jumaa na "tunapowafuatilia, tunagundua wanakwepa kulipia gharama za matibabu waliyopata.

"Sisi tunashauri kuwa kama kuna tatizo, wahusika watoe taarifa na tutawasaidia. Hakuna haja ya kutoroka.”

IDADI YA WAGONJWA

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wauguzi wa MOI walisema licha ya kuwapo kwa tatizo la baadhi ya wagonjwa kutoroka gharama za matibabu, hukabiliana na changamoto ya kuhudumia wagonjwa wengi kwa siku.

Wauguzi hao walisema kuwa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaowahudumia, nao hujikuta wakipata matatizo ya kiafya kama maumivu ya mgongo na shingo.

Muuguzi Kiongozi, Uwezo Nkomola, alisema hupata matatizo ya kiafya kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu wakiwa wamesimama.

Alisema kanuni ya kazi yao inawataka kila muuguzi kuwahudumia wagonjwa sita au saba kwa siku, lakini wakiwa MOI hutoa huduma kwa wagonjwa 15 hadi 25 wawapo kazini.

“Hatuna muda wa kutosha wa kupumzika kama kanuni inavyosema. Wakati wote tunasimama kutoa huduma… tunaona kwamba hiyo ndio njia pekee ya kuwafikia wagonjwa wote kwa ubora unaotakiwa,” alisema Nkomola.

Bernadina Rambau, alisema wanakabiliwa na chamgamoto mbalimbali ikiwamo upungufu wa vifaa tiba na muda mrefu wa kufanya kazi.