MUGABE: Kubaki Rais mpaka Mungu atakapomwita

20Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
HARARE, Zimbabwe
Nipashe
MUGABE: Kubaki Rais mpaka Mungu atakapomwita

WAKATI katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alipowaasa viongozi wa Afrika kutong’ang’ania madarakani kwenye mkutano mmoja mwezi uliopita, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alijibu ataendelea "hadi pale Mungu atakaposema 'njoo'".

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Mugabe anatimiza miaka 92 kesho na, kwa mujibu wa kauli hizo, hana nia ya kuachia ngazi licha ya kuwa ndiye kiongozi mzee zaidi barani Afrika na rais pekee ambaye Zimbabwe imemfahamu tangu uhuru mwaka 1980.

Hata hivyo, nia yake ya urais wa maisha inaweza kuwaudhi vigogo wa chama chake tawala cha ZANU-PF ambao wamekuwa wakijaribu kwa miaka mingi kujiweka wenyewe kwenye enzi ya kisiasa baada ya Mugabe.

Vile vile itachochea shutuma kutoka kwa wapinzani wa serikali, ambao wanasema mgogoro wa ndani unaikwaza kwenye jukumu la kushughulikia uchumi uliokwama na ukame mbaya zaidi kupata kuikumba nchi hiyo kwa kizazi kimoja – madai ambayo hata hivyo yalikataliwa na mawaziri.

"Pamoja na tishio hili la njaa, na uchumi ukiwa kwenye hali mbaya, hakuna anayeshughulikia janga hili la kitaifa. Hakuna jibu la serikali kwa vile ZANU-PF inafikiria tu suala la urithi (wa madaraka) wa Rais Mugabe," kiongozi mkuu wa upinzani, Morgan Tsvangirai, alisema wiki hii.

Wakosoaji wanamlaumu Mugabe kwa mengi kati ya matatizo yanayoikabili nchi hiyo. Wanasema sera zake, ikiwemo ya kuchukua na kugawa upya mashamba ya biashara yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu, zilisababisha moja kati ya chumi zilizokuwa zikienda vizuri zaidi barani Afrika iingie kwenye karibu muongo mmoja wa mdororo hadi mwaka 2008, na kupunguza uzalishaji wake kwa takribani nusu.

Vile vile wanasema uchumi unaoyumba wa Zimbabwe na uzalishaji wa chini – kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia takriban 85 – vimeiacha nchi ikiwa katika hali mbaya kushughulikia ukame ambao umeacha watu milioni tatu wakihitaji chakula cha msaada, ikiwa ni robo ya watu wote wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Mugabe anatetea uchukuaji wa ardhi kama kitu muhimu katika kusahihisha makosa yaliyofanyika enzi ya ukoloni na kusema uchumi wa Zimbabwe umeathiriwa na vikwazo vya nchi za Magharibi ambazo zinamuadhibu kwa kuchukua ardhi inayomilikiwa na wazungu.

TOROLI
Mugabe anabakia kuwa msimamizi mkuu wa uendeshaji wa siku hadi siku wa serikali yake. Bado anasimamia mahafali kwenye vyuo vikuu vyote vya serikali na magwaride ya kijeshi, na anasafiri sana nje ya nchi.

Rais huyo anasisitiza kwamba chama chake kitachagua mrithi. Lakini anapanga kugombea kwenye uchaguzi ujao mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 94, akiwania awamu yake ya mwisho ya miaka mitano chini ya katiba mpya ambayo itamshuhudia akiendelea kutawala hadi akiwa na miaka 99.

Mkewe Grace, mwanamama mwenye sauti sana ndani ya ZANU-PF, aliwaeleza wafuasi wa chama hicho wiki iliyopita kwamba ni mumewe pekee aliye na uwezo wa kuiweka Zimbabwe "pamoja na ikiwa na amani", na kuongeza kwamba atamsukuma hata kwenye toroli kumpeleka kazini kama atakuwa hawezi kutembea.

"Kutokana na uchambuzi wa hali ya kisiasa, hotuba zake za kisiasa, matendo yake ya kisiasa, inazidi kuwa wazi kwamba (Mugabe) anawania kuwepo hapo kwa kipindi chote cha maisha yake," alisema Eldred Masunungure, mhadhiri wa sayansi ya jamii kwenye Chuo Kikuu cha Zimbabwe.

Pamoja na umri wake mkubwa, Mugabe anabakia kuwa gundi inayokiweka pamoja chama chake cha ZANU-PF, ambacho kinatawala ulingo wa kisiasa nchini Zimbabwe. Anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa wa jeshi, chombo ambacho kimekuwa nguzo kubwa kwenye utawala wake wa muda mrefu.

Wazimbabwe wengi wanafuatilia afya yake kwa karibu, hususani baada ya taarifa za mtandao wa Wikileaks kwamba anaweza kuwa na saratani ya kibofu – kitu ambacho amekanusha.

Huku Mugabe akiwa ametawala nchi hiyo kwa miaka 36, baadhi ya watu wanahofia kwamba serikali inaweza kushindwa kufanya kazi vizuri na nchi kukumbwa na hali ya ukosefu wa utulivu kama atafariki bila kulipatia ufumbuzi suala la mrithi wake.

Mwaka jana alisoma hotuba isiyohusika kwenye bunge, ambapo upinzani ulichukua fursa hiyo kuhoji kama kweli alikuwa bado ana akili timamu, japokuwa msemaji wa rais huyo aliwalaumu wasaidizi wa kiongozi huyo.
Ni dhahiri kusita kwake kuachia madaraka kunaweza kutowafurahisha vigogo ndani ya ZANU-PF wenye nia ya kuchukua nafasi yake.

Vigogo kadhaa ndani ya chama wana nia ya kuwania urais, lakini Emmerson Mnangagwa amekuwa akichukuliwa kama mrithi dhahiri wa Mugabe. Alipandishwa kuwa makamu wa rais mwaka 2014 kufuatia kufukuzwa kwa Joice Mujuru, kiongozi mwingine wa kambi ndani ya chama ambaye alikuwa pia akitajwa kuchukuwa nafasi hiyo ya juu zaidi baada ya kushikilia ofisi ya makamu wa rais kwa muongo mmoja.

Tangu wakati huo Mnangagwa amejichimbia kwenye nafasi yake kwa kufanya washirika wake wateuliwe kwenye nafasi muhimu kwenye baraza la mawaziri na yeye mwenyewe kuchukua jukumu la kufanyia mabadiliko uchumi na mfumo wa sheria.

'MAMBA'

Lakini makamu huyo wa rais – aliyepachikwa jina la 'Mamba', ambalo anasema linaakisi uwezo wake wa kushambulia katika wakati muafaka – anapingwa na kundi moja lililopachikwa na vyombo vya habari jina la G-40, likihusisha mawaziri vijana wa serikali na wanachama wa ZANU-PF walio nyuma ya Grace Mugabe, ukiwemo umoja wanawake wa chama hicho.

Kwa kiasi kikubwa Grace anachukuliwa kwenye chama hicho kama mtu mwingine anayeweza kumrithi Mugabe, pamoja na kwamba mwanamama huyo anasema hana nia hiyo.

Kundi hilo linasema Mugabe anapaswa kuachwa madarakani na limekuwa likirushiana matusi na wapambe wa Mnangagwa, likiwashutumu kwa kupanga kumpindua rais huyo – madai ambayo wanayakataa.

Mnangagwa mwenyewe hajajibu shutuma hizo, lakini washirika wake ndani ya ZANU-PF na jeshi wanasema pembeni kutofurahishwa na ushawishi ambao ‘First Lady’ huyo anao kwa rais huyo.

Wanasema kundi la G-40 linajaribu kumtenganisha Mugabe kutoka kwa makomredi wake wa zamani.
Kwenye mkutano wa chama wa wiki iliyopita, Grace alisema baadhi ya watu ambao hawakutajwa walikuwa wanapanga kumuondoa Mugabe kibabe na kuidhuru familia yake, tuhuma sawa na zile ambazo mwanamama huyo alizitoa mwaka 2014 dhidi ya Mujuru.

Kampeni hiyo dhidi ya Mujuru ilisababisha Mugabe kumshutumu makamu huyo wa rais wa zamani mbele ya wafuasi watiifu wa chama kwamba alikuwa ni kiongozi wa "kundi la wasaliti" wanaotaka kumuondoa madarakani, na akamtimua.
Grace Mugabe ameshagusia kwamba zaidi ya yote Mnangagwa anaweza asiwe ni mtu aliyechaguliwa.

"Wanapitapita wakisema Mama Mugabe anataka kuongoza, mimi tayari ni msimamizi. Wale ambao tulidhani wanaweza kumrithi (Mugabe), hatuna tena imani yoyote nao," mwanamama huyo alisema kwenye mkutano huo wiki iliyopita.
Mnangagwa hakujibu maombi kadhaa ya kumtaka kutoa kauli yake kwa ajili ya makala hii.

Masunungure wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe alisema jukwaa linaweza kuwa linasukwa kwa ajili ya kuondolewa madarakani Mnangagwa, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya kutoswa kwa Mujuru.

Alisema hiyo inaweza kumaanisha kambi mbili kubwa ambazo zimekuwa zikiwania kumrithi Mugabe tangu mwaka 2000 zitafagiliwa kutoka ndani ya chama hicho.

"Somo kwa Mnangagwa ni kwamba unaweza kubishana, unaweza kuhaha miongoni mwenu, maadam tu usifanye dhambi kubwa zaidi ya kutaka kuchukua madaraka wakati rais bado yupo hai," aliongeza.

"Nafikiri huo ni mstari mwekundu kwa Rais Mugabe. Sasa rais anaelezwa kwamba mtu huyu amevuka huo mstari mwekundu."