Bao pekee lililofungwa dakika nne baada ya saa ya mchezo na beki wa zamani wa Simba, Miraji Adam, lilitosha kuwapa mabingwa hao wa Tanzania Bara 1988 ushindi wa tatu kwenye ligi msimu huu.
Matokeo hayo yalihitimisha safari ya kikosi cha Mwingereza Stewart Hall kutopoteza mechi msimu huu baada ya kushinda 13 na kutoka sare mara tatu kabla ya kipigo cha juzi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kipigo hicho pia kimeweka rekodi ya kuwa cha kwanza baada ya Azam kucheza mechi 19 mfululizo za VPL (mbili za mwisho msimu uliopita) tangu Mei 3, 2015 walipofungwa 2-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mantiki hiyo, Wanalambalamba wamepoteza mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu baada ya siku 287, huku mechi zote akidaka kipa Aishi Manula ambaye amefungwa mabao 11 msimu huu.
Takwimu za Nipashe zinaonyesha kuwa kipa huyo (20), amefungwa mabao 16 katika mechi zote 31 alizokaa kwenye lango la Azam kwenye mashindano yote msimu huu waliouanza kwa kutwaa Kombe la Kagame bila kupoteza mechi na kufungwa goli hata moja.
Bao la juzi la Miraji ambaye pia alifunga la kwanza katika ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Yanga Januari 30, lilikuwa la nne Coastal Union kuifunga Azam FC katika mechi 10 zilizopita za VPL.
Katika mechi hizo zinazoanzia msimu wa 2011/12 Azam FC imeshinda mechi saba na kutoka sare mara mbili kabla ya kipigo cha jana. Timu hiyo ya Chamazi pia imefunga mabao 18 katika mechi zote ilizokutana na Coastal Union Ligi Kuu tangu ipande Ligi Kuu msimu wa 2008/09.










