Makocha wakwamisha kambi timu ya taifa kuogelea Dar

16Feb 2016
Dar
Nipashe
Makocha wakwamisha kambi timu ya taifa kuogelea Dar

KAMBI ya timu ya taifa ya kuogelea, iliyokuwa ianze jana jijini Dar es Salaam, imeahirishwa kupisha mafunzo ya makocha wa mchezo huo yanayoendelea kwenye shule ya kimataifa ya Tanganyika jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo ambayo inajumuisha waogeleaji wanaojiandaa kwenda Dubai na Mauritius kusaka viwango vya kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka huu, itafanyika chini ya kocha John Belela na msaidizi wake Khalid Rusha baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka, alisema wamelazimika kusitisha kambi hiyo ili kumpa nafasi mkufunzi Rick Power kutoka Marekani kuendesha mafunzo kwa makocha wa mchezo nchini.

Kutokana na kupigwa kalenda kwa kambi hiyo, waogeleaji wataendelea na mazoezi ya kila siku wakitokea nyumbani wakati wakisubiri kambi ya pamoja.

Aidha, kiongozi huyo alisema kamati ya utendaji ya TSA inaendelea na maandalizi ya kambi na safari za wachezaji kwenda Dubai na Mauritius.

"Kamati ya ufundi inaendelea na maandalizi ya safari hiyo, ikiwamo kutafuta wadhamini kwa ajili ya kusaidia kufanikisha mipango hiyo," alisema Namkoveka.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, waogeleaji watano watakwenda Dudai huku idadi ya watakaopelekwa Mauritius wikitarajiwa kuwa kubwa.

Katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Rio de Janeiro nchini Brazil Agosti, Tanzania inatarajia kupeleka wanamichezo wa ngumi, riadha, kuogelea na judo.