Yanga: Tunajipanga kusimamisha Simba

16Feb 2016
Faustine Feliciane
Dar
Nipashe
Yanga: Tunajipanga kusimamisha Simba
  • **Wanajangwani wamepiga kambi Pemba kusaka ushindi wa pili mfululizo dhidi ya timu hiyo ya Msimbazi iliyojificha Morogoro.

INGAWA Yanga itakosa huduma ya Kelvin Yondani katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Simba, kocha msaidizi wa timu hiyo ya Jangwani, Juma Mwambusi amesema hawana sababu ya kuingiwa na hofu kwa kuwa wana kikosi kizuri.

Yondani, beki wa zamani wa Simba ambaye hajawahi kukosa penalti, atakosa mechi hiyo ya pili ya watani wa jadi msimu huu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa akimalizia adhabu yake ya kifungo cha mechi tatu kutokana na kumpiga daktari wa Coastal Union Januari 30.

Mbali na Yondani, Yanga pia haina uhakika wa kumtumia beki wake wa pembeni kulia, Juma Abdul, aliyeumia kifundo cha mguu katika mechi ya ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Cercle de Joachim nchini Mauritius Jumamosi.

Lakini katika mahojiano na Nipashe kwa simu akiwa kambini Pemba jana, Mwambusi alisema hawana hofu na ubora wa kikosi cha watani wao wa jadi ambacho kimefunga mabao 16 katika mechi zote saba za Ligi Kuu Tanzania Bara kilizocheza tangu kuanza kwa mwaka huu (sita chini ya kocha mkuu wa muda Jackson Mayanja).

"Kwa nini tuwahofie Simba?" Mwambusi alihoji. "Hatuna shaka nao kwa sababu tuna kikosi kizuri na kwa sasa tunajipanga kwa ushindi.

Aidha, alisema kuwa Kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm,a meandaa programu maalum wanayoifanyia kazi kwa sasa kwenye kambi yao Pemba."

Mwambusi aliendelea kueleza kuwa kukosekana kwa Yondani Jumamosi hawataki kuwe sababu ya wao kutopata pointi tatu dhidi ya Simba.

"Kweli (Yondani) ni mchezaji muhimu kwenye kikosi, lakini anapokosekana ni lazima maisha yaendelee, bado tuna wachezaji wengine ambao wataziba pengo lake," alisema Mwambusi na kuongeza kuwa bado wanafuatilia maendeleo ya enka ya Abdul.

MAYANJA ALONGA
Wakati Yanga wakizidi kujipanga Pemba, Kocha wa Simba (Mayanga), ameendelea kusisitiza umuhimu wa timu yake kupata ushindi katika mechi hiyo ya raundi ya 20 ya ligi ya Bara msimu huu.

"Nashukuru wachezaji wangu wapo na afya nzuri, naomba mambo yaende hivi mpaka siku ya mchezo," Mayanja aliambia Nipashe jana jioni.

Alitamba kuwa ushindi walioupata katika mechi sita mfululizo tangu arithi mikoba ya Mwingereza Dylan Kerr, umewafanya nyota wake kujiamini na kuamsha ari ya kupambana zaidi.

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na mtaji wa pointi 45 baada ya mechi 19 ikifuatwa na Yanga wenye pointi 43 wakiwa na mechoi moja mkononi.