Simba SC ambayo ilimuuza Samatta klabu ya TP Mazembe mwaka 2012, inapaswa kupata asilimia 20 ya fedha ambazo TP Mazembe imelipwa baada ya kumuuza Samatta kwenye klabu hiyo ya Ubelgiji.
Na akizungumza na Lete RAHA, Rais wa Simba SC, Evance Aveva, alisema kwamba tayari wamekwishawaandikia barua TP Mazembe ya kuwajulisha kuhusu na mgawo ambao wanastahili kupata kama moja ya klabu ambayo imemkuza Samatta kabla kutoka nje.
Aveva amesema kutokana na hilo, baada ya kutuma barua kwa uongozi wa timu hiyo, umerejesha majibu ya kuwa mara baada ya kukamilisha taratibu zote za uhamisho wa mchezaji huyo na kulipwa mgawo wao, watahamia kwenye asilimia 20 ya Simba.
"Sisi tumefanya taratibu zote zinazotakiwa kufanywa, na tumezungumza na TP Mazembe wametuomba tuvute subira kidogo, wakati wakikamilisha zoezi hilo,"alisema Aveva.
Alisema hata hivyo wao kama Simba, hawana wasiwasi na suala hilo, kwa sababu limefikia mahala pazuri baada ya mazungumzo kufanyika baina ya pande zote mbili.
Samatta alijiunga TP Mazembe mwaka 2012, akitokea Simba, kwa dau la dola za marekani 150,000, ambapo ameitumikia timu hiyo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka minne huku akiipa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika huku naye akishinda tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika Januari mwaka huu.
Baada ya kufanya vizuri, Mazembe imemuuza Samatta KRC Genk kwa dola za Kimarekani 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.7).
Samatta tayari ameanza kuitumikia klabu yake mpya ya Genk kwenye michezo ya Ligi Kuu nchini humo.










