Yametimia, Yanga Pemba, Simba 'Mji Kasoro Bahari'

15Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yametimia, Yanga Pemba, Simba 'Mji Kasoro Bahari'
  • ...Timu hizo zinakutana huku Simba ikiwa na pointi 45 wakati Yanga wenye mchezo mmoja pungufu wakiwa na pointi 43

BAADA ya kutumbua 'jipu' moja nchini Mauritius, mabingwa Yanga wamerejea nchini na kwenda moja kwa moja Kisiwa cha Pemba, Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki moja kabla ya kuivaa Simba Jumamosi hii.

WACHEZAJI WA SIMBA

Wapinzani wao, Simba baada ya kung'ata mara sita mfululizo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, wamekwenda kupiga kambi ya siri 'Mji Kasoro Bahari' akitokea Shinyanga.

Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius.

Wawakilishi hao wa Bara kwenye michuano hiyo, walirejea nchini jana asubuhi na jioni walitarajia kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema kikosi chake hakina muda wa kupumzika, hivyo wanaanza mazoezi mara moja kujiandaa kuivaa Simba.

Kocha huyo rai wa Uholanzi alisema akili yake sasa iko katika mchezo huo, ambao wamepania kushinda.
"Hatutakuwa na mapumziko, tuna ratiba ngumu mbele yetu, tunahitaji kushinda mchezo huu," alisema kwa kifupi hocha huyo.

Kuhusu mchezo dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, alisema: "Hatukucheza vizuri, lakini kubwa tunaangalia mechi iliyo mbele yetu."

Kwa upande wa Simba, timu hiyo imekwenda kuweka kambi mjini Morogoro kwenye Chuo cha Masomo ya Biblia kilichopo eneo la Bigwa.

Simba watakuwa wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa chuo hicho, kabla ya kurejea jijini kwa ajili ya mchezo huo.