Licha ya hayo, usafiri huo unatoa ajira kwa wafanyakazi wengi ambao hutegemewa na familia zao katika kuyaendesha maisha yao.
Hata hivyo, kuna kero kubwa wanayokabiliana nayo watumiaji wa usafiri huo ni lugha chafu zinazotolewa na baadhi ya makondakta ambao hawajali kama wamebeba abiria wenye hadhi gani kwa jamii zao.
Pamoja na kazi hii kuwa si ajira rasmi, baadhi ya wafanyakazi wa magari haya maarufu kama daladala, ni kero kwa jamii.
Usafiri huu hutumiwa na watu wa rika zote, yaani watoto, vijana au wazee. Hii ni biashara ambayo kwa asilimia kubwa wamiliki wake ni wale wenye shughuli nyingine ambao yawezekana si wafanyakazi wa daladala hizi.
Hivyo makondakta wanaofanya kazi katika magari haya , baadhi yao kwao mteja si mfalme!. Lugha za kashfa, matusi ya nguoni hukosi kukumbana nayo au kuyasikia, iwapo ni mtumiaji wa mara kwa mara wa usafiri huu.
Hali hii imegeuka kuwa mazoea kwa makondakta hao, kiasi cha kuaminika katika jamii kuwa hali hiyo inatokana na wao kuwa na msongo wa mawazo, kwa madai kuwa kazi yao ni ngumu.
Wafanyakazi wa daladala, wanaufanya usafiri huo kuwa ni moja kati ya maeneo ambayo yanaifanya jamii kuwa na mtazamo usiofaa, hasa kwa watoto wadogo wakiwemo wanafunzi wanaotumia usafiri huo kila siku.
Mazingira ya kazi, yakiheshimiwa kwanza na mtoa huduma ni rahisi hata anayehudumiwa kujenga heshima.
Kazi ya ukondakta ni kazi kama kazi nyingine mathalani ukandarasi, udaktari, uuguzi, ualimu, uaskari, uandishi na kazi nyinginezo. Makondakta, waanze kuziheshimu kazi zao kwanza, ili jamii iige mfano huo.
Ifikie wakati mtu akipanda daladala afike akae au asimame ajue wajibu wake ni kulipa nauli na kondakta wajibu wake ni kumsafirisha abiria aendako.
Suala la kusema kazi hiyo ni ngumu inawafanya baadhi ya makondakta wasiiheshimu kazi hiyo..Haikubaliki hata kidogo kwa jamii kufanya mambo ya hovyo kabisa. Lugha za staha na heshima ni matarajio ya kila abiria .
Kondakta akutanapo na wateja wake na lugha zisizofaa ziwe marufuku kwa jamii.
Katika hili tunaweza kuwafanya watoto wetu kujifunza namna nzuri ya kuwasiliana na wakubwa hata wadogo wenzao na si kuwaharibia mtazamo wao kifikra na watu wachache.
Lugha hii itaifanya jamii kuendelea kuwaheshimu wakubwa, kwani imefikia wakati mtu anaona aibu kwenda kupanda daladala na mama, baba, dada, kaka, mjomba au shangazi yake, kutokana na kuogopa na kukutana na kadhia hiyo.
Haifai, kukutana na lugha chafu zinazoidhalilisha jamii na jamii kuendelea kukalia kimya jambo hili.
Mamlaka husika zichukue hatua kukomesha utovu huu wa nidhamu ulipitiliza wa makonda wa daladala.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








