Utaratibu wenyewe kwanza ni katiba na sheria zake, sasa unaweza kumpema Rais Magufuli, je utarartibu alioukuta kwa sababu hatujaanza kwenye mfumo sifuri, tulikuwa na serikali ya awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne na hii ya tano.
Katiba aliyoikuta, je usimamizi wake kwa siku 100 umefuatwa kwa kiasi gani? Kwa kiasi kikubwa kuna utata mkubwa sana.
Yeye alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na lazima uchaguliwe na pande zote za muungano kuwa rais.
Ulishuhudia kura alizochaguliwa nazo kule Zanzibar, matokeo kwa upande ule yalifutwa, waliopiga kura kwa Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge na wawakilishi ndiyo haohao lakini kwa kule matokeo yakafutwa.
Kumetokeo tatizo katika ule uchaguzi, dunia imesema uchaguzi huu utatuletea matatizo kama Jamuhuri ya Muungano na unamuondolea yeye uhalali wa kuwa amiri jeshi mkuu na rais wa muungano.
Kwa sababu kosa la uhaini linafanyika dhidi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ukisoma katiba ibara ya 28, fasiri ya nne, inasema uhaini ni kosa la juu kabisa linalofanywa dhidi ya Jamhuri ya Muungano na ndiyo maana ukirejea kesi ya Machano Hamis na wenzake wakati wa Salmin Amour, walivyosema kwamba walitaka kumpindua, Mahakama ya Rufani.
Tanzania chini ya Jaji Robert Kisanga, ilisema Zanzibar siyo dola, huwezi ukaipindua Zanzibar.
Jaji Kisanga alisema huwezi kuipindua Zanzibar kwa sababu siyo dola, kuna serikali tu pale ya kiuendeshaji, lakini dola ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndiyo maana ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi anayo John Pombe Magufuli, ili aweze kuhalalisha ndani ya hizi siku 100, jambo kubwa kuliko yote ambalo ni la ushirikishwanaji wa dunia ya leo, ni kutunza utu wa mwanadamu, ni kuthaminisha uhai wa mwanadamu.
Kwa Zanzibar ambayo ni upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna walakini wa hali ya juu sana, kuna wasiwasi wa hali ya juu sana na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hatupo na utulivu wa ndani ili tuweze kufanya majukumu yetu ipasavyo kwa sababu kuna viashiria vya dunia kutuonya, kututenga, na Tanzania tunaihitaji zaidi dunia kuliko dunia inavyotuhitaj sisi.
Nasikia jumuiya za kimataifa zinasema, watu mbalimbali wanasema, humu nyumbani wanasema, viongozi wa dini wanasema, kwa hiyo taifa halina utulivu.
Unaweza ukaona unafanya kazi kwa harakaharaka ya kuonyesha jamii kwamba naweza hili, naweza hili, lakini kama watu hawana amani, kama ulinzi na usalama haupo, ni kwamba utakuwa hujaanza vizuri.
Kwenye tathmini yangu, siku 100 za John Pombe Magufuli, suala la Zanzibar ni mtihani mkubwa sana kwake.
Aidha, unaweza ukabeba maji vizuri ukayafikisha mlangoni ukayamwaga, kwa hiyo utakuwa hujafanya lolote.
Kwa kuwa ameshindwa kutatua tatizo hili la Zanzibar, wapo wanaosema kuna Katiba ya Zanzibar, huwezi ukaiingilia, kuna Sheria za Zanzibar, kuna hili, ndugu zangu tusidanganyane kwa ujanjaujanja wa kisiasa.
Ndiyo maana hata tunapoanza dua zetu bungeni, tunasema ‘eeh Mwenyezi Mungu utujalie hekima na busara ya kufanya maamuzi sahihi kwa ustawi wa taifa lako’.
Hatusemi Mwenyezi Mungu tusaidie tutumie katiba, tutumie sheria, ni kwamba sheria zilizoandikwa, katiba zilizoandikwa hazizidi hekima ya mwanadamu, tunaweka katiba pembeni tunamuomba mwenyezi Mungu hekima.
Ndiyo maana wimbo wetu wa taifa tunaanza na Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, kwa hiyo tusipotumia hekima na haswa John Pombe Magufuli, asipotumia hekima yeye kama amiri jeshi mkuu, Tanzania ikivurugika ni yeye namba moja kwa sababu yeye ndiye amekula kiapo cha kulinda ulinzi na usalama wa raia wa Tanzania.
Machafuko yakitokea Zanzibar hawatasema ni Wazanzibar, ni Watanzania, yalipotokea 2001 waliokimbilia Shimoni (Mombasa) waliokimbilia Sudan, ni Watanzania, hutosema ni Wakenya, nishauri tu kwamba kwa upande wa usalama wa nchi, kwa upande wa utulivu wa Watanzania, huko mbele tunaona giza nene kuhusu tatizo la Zanzibar.
Kuhusu hizi changamoto nyingine, ni rai yangu kwamba, mamlaka inatoka kwa watu na dunia ya leo kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ni kwamba raia wanataka waishi namna gani, kwa maslahi yao, wanatoa kauli zao na mitazamo yao, zaidi ni suala la katiba.
Ili aweze kufanikiwa, turudi kwenye suala la katiba kwa haraka sana ili tuweke utaratibu ambao tutauheshimu sote, tuone Tanzania ya miaka 10 au 20, na ya kutatua hata hilo tatizo la Zanzibar ambalo nimesema ni la awali.
Kwa kuitendea zamira yangu haki, niseme tu ukweli kwamba kwa sasa kuna mchoko kwenye jamii, Watanzania tumekuwa tukiongoza taifa hili kwa matukio na Watanzania wanasahau sana mambo ya huko nyuma.
Ukiangalia wakati Mkapa (Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa), anaingia madarakani, watu walikuwa wamemchoka sana Mzee Mwinyi (Rais wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi), watu wakashangilia kweli kweli, Mr clean, Mr Clean, ikaja tume ya Warioba (Jaji Mstaafu, Sinde Warioba) ya rushwa, lakini baada ya muda hakuna lililofanyika, yote yakafunikwa.
Wakati Kikwete (Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete) anaingia, Mkapa wakawa wamemchoka hawataki, Kikwete akaingia kwa zaidi ya asilimia 80 (ya kura), Watanzania wakawa na matumaini makubwa kweli kweli, Kikwete akatembelea wizara mbalimbali, akatembelea maeneo mengi, kama anavyofanya Magufuli, kila Mtanzania akawa anashangilia, ari mpya, maisha bora kwa kila Mtanzania, Watanzania watapata milo mitatu, wakawa wanashangili, Kikwete, Kikwete.
Kikwete ameondoka madarakani, Watanzania hawataki kumuona, leo hii Magufuli ameingia madarakani, anazungumzia upasuaji wa majipu, fisadi namba moja wa nchi yetu ni katiba, huu upasuaji wa majipu mimi niseme tu ni vipele, vichunusi anavipangusa na majipu huwezi kuzungumza kwa matukio, unaanza na hili moja, unafanya na lile, limekuwakuwaje kwa mfumo wa namna gani, ndiyo maana alipoingia mara TRA, haikuchukua muda tukasia Magufuli yule yule anatoa muda kwa ambao hawakulipa kodi waanze kuilipa.
Kauli hizi hizi ni zile za Kikwete, kwa hiyo hakuna utofauti wowote, kwa mtazamo wangu, ingawa hii kauli ya kupasua jipu imekua maarufu, lakini hayo ni matukio tu.
Nasema watu walio makini, walio na utulivu wanajadili hoja, hawajadili matukio, haya matukio tunayoyaona yatakuwa ya muda mfupi, na siku zinavyokwenda yanazidi kupungua, ni tofauti na wiki ya kwanza aliyoanza, wiki ya pili, yuko
Muhimbili, yuko wapi, ile kasi inapungua ndani ya siku hizi 100 tu, sasa tusubiri ifike miezi sita, mwaka mmoja Watanzania watakiri kuwa tumekuwa ni watu wa kushabikia matukio zaidi badala ya kuwa na utulivu na kuona hoja za msingi.
Tumekuwa ni watu wa kusubiri tukio litokee ndipo tuanze kelele. Ili tuondokane na hayo, mfano tunasema elimu bure, tafsiri yake nini, kuna mihimili mitatu, Bunge, Serikali na Mahakama.
Bunge ndiyo linapitisha bajeti ya serikali, sasa kwanini wasingeweka utaratibu wa kuleta hapa, huwezi ukasema fedha hizi zitoke hapa labda ni za sikukuu ukasema peleka barabarani, unaanza kuvuruga utaratibu mwenyewe na itakuwa ni matatizo makubwa.
Kwenye siku ya mahakama tumeona, huwezi kusema majaji hukumuni kesi (za ukwepaji kodi ya Sh. trilioni moja) hivi, mkihukumu hizo pesa mtakazopata nitawapeni, tayari umeshaharibu kesi.
Magufuli ana nia njema, lakini nchi hii ilivyo, kidole kimoja hakivunji chawa, weka mifumo itakayofanya kazi.
Bila mifumo, mkakubaliana hiyo mifumo, hutoweza wewe mwenyewe, hata mawaziri wako wakisema ni wao wenyewe watashindwa, kwa hiyo nisema ndiyo ameanza vizuri, lakini ili Watanzana wasimchoke mapema, ili wasianze kumtupia madongo kwa haraka, ili wasikate tamaa haraka, arudi kuwatengenezea katiba ambayo italinda vizazi hivi na vijavyo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








