Azam yaibipu Yanga, Fei Toto hashikiki Ligi Kuu

08Mar 2024
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Azam yaibipu Yanga, Fei Toto hashikiki Ligi Kuu

​​​​​​​SARE ya bao 1-1 iliyoipata juzi usiku Azam FC kwenye uwanja wake wa nyumbani, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam dhidi ya Coastal Union imeifanya timu hiyo kukaa juu ya msimamo wa Ligi Kuu, huku ikisubiriwa mechi ya leo kati ya Namungo FC dhidi ya Yanga.

Feisal Salum.

Dakika tisa kabla ya mechi kumalizika, Feisal Salum aliisawazishia Azam bao, akiiokoa timu yake kwa kipigo, lakini akifikisha idadi ya mabao 12 na kuzidi kumuacha Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyeongoza kwa kipindi kirefu, akiwa na mabao 10.

Kabla ya bao hilo, Coastal Union ilipata bao dakika ya 68 lililowekwa wavuni na Semfuko Charles.

Matokeo hayo yameifanya Azam kuongoza ligi, ikifikisha pointi 44, ikiiacha Yanga ikiwa na pointi 43, kabla ya kucheza mechi ya leo ugenini, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi ambapo, matokeo ya mchezo huo yataamua kama Wanalambalamba wataendelea kusalia kileleni au la.

Fei Toto amefikisha mabao 12, akiwa pia ametoa pasi za mwisho tano kwa timu yake, hivyo kuchangia jumla ya mabao 17 kwenye timu yake ya Azam aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Yanga.

"Nafurahi kufunga mabao na kuisaidia timu yangu, na hata kama itatokea nikawa mfungaji bora ni vizuri pia, mimi ni mpambanaji, kawaida yangu kupambana wala sishindani na mtu, ninachofanya ni kuipeleka juu Azam, ikitokea nikichukua kiatu cha dhahabu sawa, akichua mwingine wala sitokuwa na kinyongo," amesema Fei Toto.

Aziz Ki wa Yanga ametupwa nafasi ya pili kwa mabao 10, Jean Baleke aliyekuwa akiichezea Simba, Maxi Nzengeli wa Yanga, Waziri Junior wa KMC na Marouf Tchakei wa Tabora United ambao wote wana mabao manane.

Wachezaji wenye mabao saba ni Prince Dube wa Azam FC, Adam Adam wa Mashujaa na Samson Mbangula wa Prisons.

Baada ya sare ya bao 1-1 jana dhidi ya Azam, Coastal Union imekwea hadi nafasi ya nne ya msimamo ikiwa na pointi 27 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.