Hatima sakata la Dube J'tano, atajwa Yanga

10Mar 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Hatima sakata la Dube J'tano, atajwa Yanga

​​​​​​​UONGOZI wa Azam FC umesema utatoa msimamo wake kuhusu uamuzi wa mshambuliaji wake, Prince Dube, aliyeandika barua ya kutaka kuondoka klabuni hapo ifikapo Jumatano, imeelezwa.

Prince Dube.

Hata hivyo taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanatajwa kumwinda mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na kiwango bora kila anapokutana na vigogo wa soka nchini.

"Kuna taarifa Yanga imeanza mchakato wa ndani wa kumwania Dube, naona ni vita nyingine na jeuri ya fedha tutaishuhudia katika usajili hapa nchini," kimesema chanzo chetu.

Machi 4, mwaka huu, Dube, raia wa Zimbabwe aliiandikia barua Azam akiomba kuvunja mkataba wake kutokana na kutaka kujiunga na klabu nyingine ili kufikia malengo yake.

Klabu hiyo yenye makao yake Chamazi, Dar es Salaam ilimjibu mshambuliaji huyo iko tayari kuvunja mkataba walioingia endapo watalipwa kiasi cha Dola za Marekani 300,000, ambacho kimeandikwa kwenye makubaliano.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabit, ‘Zaka', amesema klabu hiyo imepanga kutangaza uamuzi wake rasmi Jumatano baada ya kukaa kimya huku mshambuliaji huyo akiendelea kushikilia msimamo wake wa kutaka kuondoka.

Zaka amesema wanatambua Dube bado ni mchezaji wao halali kama mkataba unavyosema na hawana hofu yoyote juu ya uamuzi aliouchukua.

“Kwa sasa tumeamua kukaa kimya lakini ikifika Machi 13, mwaka huu, itakuwa siku ya Jumatano tutazungumza na kuweka wazi juu ya hatima ya Dube na sisi Azam FC,” amesema Zaka.

Dube pia katika barua yake aliyoandika amewashukuru wafanyakazi na mashabiki wote wa Azam FC kwa safari yao ya miaka minne waliyokuwa pamoja.

Mshambuliaji huyo pia amekaririwa akisema anataka kujiunga na timu yenye malengo ya kutwaa ubingwa na anaiona Azam FC ni klabu isiyokuwa na ndoto hiyo huku akishanganzwa na viongozi wa klabu hiyo wakiwa na 'mapenzi' na Simba na Yanga.