Gamondi ataja ugumu wa Ihefu Chamazi leo

11Mar 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Gamondi ataja ugumu wa Ihefu Chamazi leo
  • Mexime asema ni mechi ngumu lakini wanataka matokeo na wamejipanga...

​​​​​​​WAKATI vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wakishuka dimbani leo kusaka pointi tatu muhimu mbele ya Ihefu FC katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi, ameeleza sababu ya mchezo huo kuwa ugumu, lakini akasema "tunazitaka pointi tatu".

Mchezo huo utakapigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, majira ya saa 1:00 usiku ambapo timu zote zinahitaji pointi tatu, huku Yanga ikihitaji kulipa kisasi baada ya duru la kwanza kupoteza pointi zote tatu ugenini.

Katika mchezo wa duru la kwanza Oktoba 4, mwaka jana, Yanga walikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbalali mkoni Mbeya.

Ihefu FC ni timu pekee msimi huu imefanikiwa kuifunga Yanga ambao kipigo hicho bado kipo katika kumbukumbu zao na leo wanakutana katika mzunguko wa pili na wakitaka kuendeleza  walipoishia huku wenyeji wao wakitaka kulipa kisasi.

Kwa misimu mitatu timu hizo zilipokutana Ihefu FC imepoteza mechi tatu, imeshinda mbili na sare moja, hivyo mchezo wa leo kila moja imedhamiria kusaka pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Yanga, Gamondi amesema wametoka kucheza mechi Ijumaa iliyopita na wamerejea na kupata siku moja ya kujiweka sawa kwa ajili mchezo huo wa leo.

Amesema ataendelea kuwakosa baadhi ya wachezaji sita waliokosekana mechi iliyopita akiwamo Khalid Aucho ambaye anefanyiwa upasuaji mdogo wa goti.

“Wachezaji wako tayari kwa ajili ya kuwakabili Ihefu FC, itakuwa  mechi ngumu na ushindani kwa sababu tunakutana na timu  bora tofauti ya tuliyokutana nayo katika mzunguko wa kwanza, (hii ni kwa sababu) wamefanya maboresho kuanzia benchi la ufundi na kuongeza baadhi ya wachezaji wazuri.

"Kitu muhimu kwangu ni kutumia nafasi vizuri na  kucheza mpira mzuri ambao tutafanikiwa malengo yetu, kila  siku naomba Wananchi waje uwanjani, wasahau matokeo ya mechi iliyopita waje kwa wingi kuisapoti timu yao na kuona kiwango kizuri,” amesema Gamondi.

Kocha Mkuu wa Ihefu FC,  Mecky Maxime, amesema mechi hiyo si rahisi kwa kuwa Yanga ni bora wanaongoza ligi na wamefanya mazoezi kulingana na ubora na madhaifu ya wapinzani wao, ila  kikubwa kwao wanahitaji pointi tatu.

“Kikubwa tunaingia kwa tahadhari kucheza kwa nidhamu kubwa na kuangalia ni muda gani wa kushambulia na kuzuia, kazi yangu ni kutengeneza vijana na kuwapa njia ya kuweza kupata matokeo mazuri.

"Tunekuwa tukipata nafasi nyingi na tunazitumia chache, lakini mechi ya kesho (leo), itakuwa nzuri kwa sababu tunahitaji kupata matokeo, tuna timu nzuri na tunahitaji pointi tatu hakuna kingine, “ amesema Maxime.

Mwakilishi wa wachezaji wa Ihefu FC, Fikirini Bakari amesema wako tayari kwa mchezo wa leo na wataingia kwa tahadhari kubwa kwa sababu wanatambua ukubwa wa Yanga.

“Tumejipanga vizuri na tutacheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu tumefanikuwa kuwaona wapinzani wetu, Yanga wanavyocheza na benchi la ufundi tayari limemaliza majukumu yao kazi kubwa ni kwetu kutafuta pointi muhimu katika mchezo wetu wa leo,” amesema Fikirini.