Ngoma sasa aandaliwa mkataba mpya Simba

15Jan 2024
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Ngoma sasa aandaliwa mkataba mpya Simba

KLABU ya Simba ipo mbioni kumuongeza mkataba mwingine wa miaka miwili kiungo wake, Febrice Ngoma kwa ajili ya kuzuia jaribio la klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco inayoonesha nia ya kumhitaji.

Febrice Ngoma.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimesema kuwa tayari yameanza mazungumzo na mchezaji huyo ili kusaini mkataba wa miaka miwili kutokana na kuonesha kiwango cha hali ya juu kwa siku za hivi karibuni, ikiwemo kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Kama kawaida, mchezaji akianza kuwaka Simba lazima zitokee timu zinaanza kuwanyemelea, Wydad Casablanca wameonesha kuwa wanamhitaji, walimuona katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo tumecheza nao, pia wanamfahamu kwa sababu alikuwa kule kule akicheza Ligi ya Morocco katika klabu pinzani ya Raja Casablanca," kilisema chanzo hicho.

Taarifa zinasema Wydad Casablanca walionyesha nia mara baada ya mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Desemba 19 mwaka jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 2-0.

"Naona jamaa wameonesha nia hasa kwa hiyo uongozi umeamua kufanya naye mazungumzo ili kumuongeza mkataba kwa sababu sasa hivi Simba imeshajifunza kuwa ukitaka kuwa na timu imara ni lazima ubaki na wachezaji wako tegemeo, kile kitendo cha kuwauza kirahisi Luis Miquissone kwenda Al Ahly (Misri), na Clatous Chama kwenda RS Berkane (Morocco) kimewafunza kitu kwa sababu baada ya pale timu iliyumba na haijakaa sawa mpaka sasa," chanzo kiliendelea kutoa taarifa.

Ngoma, raia wa Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo aliichezea Raja Casablanca kuanzia 2019 hadi 2022 alipotimkia Al Fahaheel SC ya Kuwait, kabla ya kutua Al Hilal ya Sudan, lakini alivunja mkataba na timu hiyo mwaka jana kutokana na machafuko ya nchini humo kabla ya kutua Simba.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amesema kwa sasa ambacho wanafikiria viongozi wa Simba ni kuimarisha kikosi na si kukibomoa.

"Nawahakikishia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa mchezaji yoyote ambaye yupo kwenye mipango ya mwalimu Benchika (Abdelhak) hatoondoka na timu imara inajengwa na kikosi imara, tuna ndoto zetu ambazo tumeziweka muda mrefu, hivyo ni lazima uwe na wachezaji wenye viwango vya juu na bora, hivi sasa tunaendelea kusaka wachezaji wenye ubora, siyo kuwauza. Siwezi kusema kama hili lipo, lakini mchezaji mzuri ambaye anahitajika hawezi kuondoka," alisema.

Wakati huo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Imani Kajula ameeleza kufurahishwa na jinsi kikosi chao kinavyoimarika, hasa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

"Timu yenu inazidi kuimarika ikiwemo eneo la magolikipa, hivi sasa tuna chaguo pana sana kwenye upande huo, tuna Ayoub Lakred, Aishi Manula, Ally Salim, Hussein Abel, michuano hii imetusaidia sana kwa sababu tumetumia vijana wengi ambao huwa hawachezi mechi zingine hasa za ligi, kina Hussein Kazi wamecheza vizuri sana, tumemuona Israel Mwenda akicheza vema, michuano ya Kombe la Mapinduzi tumeitumia kwa ajili ya kujenga timu yetu, tunawapongeza wachezaji na benchi la ufundi, pamoja na mashabiki wa hapa Zanzibar, pamoja na waliotoka Bara kuja kutushangilia," alisema Ofisa huyo.