Watano wakosa penalti Ligi Kuu

14Jan 2024
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Watano wakosa penalti Ligi Kuu

JUMLA ya penalti 19 zimetolewa mpaka kufikia raundi ya 14 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku 14 zikiwekwa wavuni na tano zikiota mbawa baada ya makipa kuokoa au wachezaji wenyewe kukosa.

Kwa mujibu wa takwimu zetu za Bodi ya Ligi zilizotolewa, penalti hizo zimekoswa na wachezaji watano tofauti.

Wachezaji waliokosa penalti ni Bruno Gomes wa Singida Fountain Gate, Erick Mukombozi (Namungo FC), Elius Maguri (Geita Gold), Enock Mayala (Coastal Union) na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar.

Takwimu za dawati la michezo la Nipashe zinaonyesha Maguri alikosa penalti katika mechi ambayo Geita Gold ilipata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa KMC wakati Chirwa akikosa katika mechi ambayo Kagera Sugar ilichapwa magoli 4-0 na Azam FC huku Mulokozi penalti yake ikiota mbawa katika mechi ambayo Namungo ikicheza dhidi ya Ihefu na kupata ushindi wa mabao 2-0.

Mayala wa Coastal alikosa penalti timu yake ilipocheza dhidi ya Mashujaa, lakini waliondoka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mabao 14 ambayo yaliyofungwa kwenye Ligi Kuu, Saido Ntibazonkiza anaongoza kwa kufunga mabao mengi ya penalti akiwa nayo matatu mpaka sasa.