Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema Gamondi ameweka wazi yuko tayari kuwatumia wachezaji waliopo na kusubiri wakati wa dirisha kubwa la usajili ili kupata mchezaji mwenye kiwango sahihi anachohitaji.
"Kocha amefikia uamuzi huo baada ya kuona viongozi wanahaha kusaka straika wa viwango vya juu, amesema kama ni ngumu kupata straika wa maana, ataendelea kuwatumia viungo washambuliaji walioko (Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz Ki), kupachika mabao kwa sababu bado wana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo na timu ikaendelea kutisha," kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza pia Gamondi amefikia uamuzi huo baada ya kubaini straika mpya atakayetua atahitaji muda wa kuzoeana na wenzake jambo ambalo linaweza kuwagharimu wakati timu iko katika mbio za kutetea ubingwa na kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Kocha amewaambia kama hatopatikana straika wa viwango vya juu basi hakuna haja ya kusajili mtu ambaye ligi ikiisha atawasumbua kuvunja mkataba na kumlipa, waache tu ataendelea na Kennedy Musonda na Clement Mzize, lakini msingi wake mkubwa itakuwa ni Pacoma, Mazi na Aziz Ki," kilisema chanzo kutoka klabuni hapo.
Yanga inatajwa ilianza mazungumzo na straka, Glody Kilangalanga, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), anayeichezea Bisha FC ya Saudia Arabia, lakini mazungumzo yanadaiwa kusuasua kutokana na sababu mbalimbali.
Nyota huyo alitajwa kuna kuchukua nafasi ya Hafidh Konkoni, ambaye hajacheza mechi yoyote ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Pamoja na kucheza mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara na kufanya vyema kwenye baadhi ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, bado wanachama na mashabiki wa Yanga wamekuwa wakilalamika timu yao kutokuwa na straika mwenye makali kama Fiston Mayele, aliyeuzwa katika klabu ya Pyramids ya Misri.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA huku msimu uliopita ikicheza fainali ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.