Wanaharakati wa mabadiliko ya kisiasa, maridhiano na ahadi za ujio wa katiba mpya, wanaona kama masuala yanachelewa kwa vile hakuna kilichozungumzwa hadi sasa.
Wanaona muda unakwenda kwa kasi na pengine serikali ilitakiwa kufanya jambo wakati mchakato huo unapoanza mwezi ujao.
Wanayasema hayo wakiangalia kuwa ni mwezi wa pili tangu kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 kwenye Wizara ya Katiba na Sheria.
Ni katika kikao cha mjadala unaofanyika kwa njia ya mtandao ukiandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wa Twitter Space.
Washiriki wanaona kuwa Watanzania wengi bado hawajui umuhimu wa mchakato huo na kuonyesha wasiwasi kuwa kuna kasi ndogo ya kuanza mchakato wa kupatikana katiba mpya.
Mwezi uliopita Waziri Ndumbaro, anatangaza kuwa mchakato huo utafanywa na wasomi, asasi za kiraia, mashirika ya dini ili kubainisha mazuri na mabaya ya katiba ya sasa na kutoa mapendekezo stahiki kabla ya kuanza uandishi wa katiba mpya. Wakirejea vipaumbele vya Wizara Sheria na Katiba ya mwaka 2023/24, mojawapo ni kutekeleza mkakati wa kutoa elimu ya katiba kwa umma ili waweze kuelewa umuhimu wake.
Rejea ya hotuba ya Waziri Dk Damas Ndumbaro bungeni jijini Dodoma, inaweka kipaumbele hicho, huku kukiwa na kilio cha muda mrefu kuhusu madai ya katiba mpya kutoka kwa wanaharakati, wadau wa siasa za vyama vingi na wengine wanaotamani mchakato huo uanzishwe haraka.
Katika mjadala wa Twitter Space washiriki wanakumbusha kuwa Watanzania wengi bado hawajui umuhimu wa mchakato huo. Baadhi ya washiriki ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Dk. Anna Henga, Rose Mwakitwange, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dk. Benson Bagoza, Ananilea Nkya na mwanasheria Fulgence Miku,
Wakijadili kuanza kwa mchakato wa katiba mpya, huku swali likiwa je, wananchi wamejiandaa au wameandaliwaje? Katika mchango wake Rose anasema licha ya nia njema ya serikali ya kutaka nchi ipate katiba mpya, kasi ya kufikia hatua hiyo inasubiriwa na kwamba uwekezaji katika programu ya uhamasishaji nchi nzima ni mdogo. Mwanaharakati huyo anasema bado hajaona dhamira ya dhati ambayo itawezesha kuanza mchakato huo, huku akitamani juhudi zifanyike ili Tanzania ipate katiba mpya yenye ubora. Kauli yake inaungwa mkono na mwanasheria Fulgence Miku, ambaye pia anasema ni muhimu kuwa na dhamira ya dhati, ili kutekeleza mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya kwa ajili ya maendeleo ya nchi, ambayo ni ahadi inayotolewa bungeni. "Bila kuwa na dhamira ya dhati kwenye mchakato huu, inaweza kuwa vigumu kupata katiba mpya, hivyo wito wangu ni kuwapo nia na juhudi hizo ili kuhakikisia wananchi wanafikia katiba wanayotamani” anasema Miku. MIDAHALO ZAIDI Askofu Dk Bagonza wa KKKT Dayosisi ya Karagwe anasema vikao na midahalo ya kitaifa vinahitajika ili kuwaamsha watu katika maeneo mbalimbali yanayotakiwa kuboreshwa na ujio wa katiba. "Mchakato wa katiba mpya umegubikwa na pengo kubwa kati ya mamlaka na wananchi hivyo kuwawia vigumu watu kujua umuhimu wake, hivyo ipo haja ya kuwa na mbinu hizo," anasema Dk. Bagonza. Kwa mujibu wa Askofu huyo, Watanzania wengi hawajui umuhimu wa katiba mpya, na kwamba ni wachache wanaoifahamu, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza uelewa," anasema."Uelewa huo utawawezesha kuwa tayari kutoa mchango chanya katika kuboresha rasimu ya katiba mpya na hatimaye waweze kupata katiba wanayoitaka kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla," anasema. Anasema bila kuwa na vikao na midahalo ya kitaifa, mchakato wa kupata katiba mpya inayotokana na wananchi unaweza kuwa mgumu, na kwamba ni muhimu kuwaamsha ili watoe maoni yao. SIASA KIKWAZO Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga anasema kuweka mbele maslahi ya vyama kwenye mchakato wa kuandaa katiba mpya ni kikwazo, na kwamba hilo lisipewe kipaumbele. "Kama mnakumbuka, mchakato wa mwisho wa katiba ulikwamishwa na siasa, kulikuwa na mgongano mkubwa wa kimaslahi miongoni mwa wanasiasa," anasema Dk. Anna. Anasema kuwa kuna haja ya wadau wa mchakato wa katiba mpya kuepuka kuweka mbele maslahi ya vyama, badala yake nchi kwanza ili kusaidia kupata katiba bora ya nchi inayokubalika kwa wengi. "Katiba mpya inapaswa kugusa wananchi kwa kuhakikisha maoni yao yanachukuliwa na kuingizwa humo kwa ajili ya maendeleo endelevu badala ya kuegemea vyama, ambavyo ni kikwazo," anasema. Mkurugenzi Mtendaji huyo wa LHRC anaongeza kuwa mchakato wa katiba hiyo uharakishwe ili ikiwezekana ipatikane haraka ili ianza kutumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka ujao. Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Ananilea Nkya, anasema Watanzania wengi hawajui kuwa katiba ndiyo sheria kuu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yao. "Kuna haja ya kuwaelimisha waelewe umuhimu wa katiba kama ambavyo Wizara ya Katiba na Sheria iliahidi kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kutoa kuelimisha umma kuhusu katiba," anasema Ananilea. Ananilea ambaye pia ni Mtaalamu Mwandamizi wa Vyombo vya Habari, anasema Watanzania wasiachwe nyuma kwenye suala la katiba kwa kuwa ndio mkataba kati yao na wanaowatawala. MCHAKATO ULIVYO Mwaka 2014 mchakato wa katiba mpya ulikwama baada ya kumalizika Bunge Maalum la Katiba lililoandaa katiba pendekezwa, huku bunge hilo likiwa limesusiwa na vyama vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.
Baadaye wadau na wanasiasa wakatoa wito wa kupatikana katiba kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, lakini hawakuweza kushawishi serikali, hadi hivi karibuni ilipotangaza kuanza kwa mchakato huo.










