Mjadala mzito wa Bandari Dar na mada za uzalendo zinavyoshindana

24Aug 2023
Ani Jozen
DAR ES SAALAAM
Nipashe
Mjadala mzito wa Bandari Dar na mada za uzalendo zinavyoshindana

MJADALA unaohusu ubinafisishaji Bandari ya Dar es Salaam,  unakoelekea huenda umefikia kilele, bila ishara ya wazi kuwa serikali itabadili kwa kina au chochote ambacho tayari Bunge pia lilishakikubali, licha ya maelezo kuwapo makubaliano ya awali huko Dubai.

 

Wakati matukio ya kisiasa yenye uzito wa ziada yakijitokeza, mchakato wa urasimishaji wa mkataba huo ulikuwa umefikia pengine mbali kwa kiasi fulani.

Mabadiliko madogo ya Sheria ya Bandari kuwezesha kuingia ubia wa kiuendeshaji, si ajabu hata kubadilisha mfumo wa hisa tayari vimeshaanza kuangaliwa, ili iendeshwe kibiashara.

Mjadala huo umewakumbusha watu matukio tofauti yaliyopita, kila mchangiaji katika hadhara hii au ile, ama mitaani, kwa wale wenye umri, wakilinganisha suala hilo na mengi yaliyotangulia, ambayo mikataba yake ilitikisa taifa.

Katika medani ya siasa, kumekuwa na juhudi za kuuangalia mpango huo kama hatua iliyochukuliwa na Wazanzibari hata kuwataja Rais na Waziri, lakini hilo lilikemewa kwa nguvu kuwa si hoja ni uchonganishi au uchochezi.

Mrengo mwingine wa upinzani umekuwa na mwelekeo wa kuangalia suala hilo kama kashfa, ila halikuwa na msisitizo kwani si waziri anayehusika zaidi, ni serikali yote kwa pamoja.

Dai lingine kutoka kwenye nguzo na ngazi ya juu ya kikanisa hivi karibuni, ni kwamba Watanzania wana uwezo wa kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.

Walichokuwa wanaashiria hapa inaelekea ni uwezo wa kitaaluma na siyo fedha za uwekezaji na kuboresha kila aina ya miundombinu ya bandari, iendane na viwango vya kimaitaifa vya ufanisi,hata ikashindana na nyingine kubwa mashariki na kusini mwa Afrika.

Haina sura bayana ya kihistoria ya kampuni ya DP World ilivyokuwa na kusimamiwa, hata ikawa na ufanisi wa nchi inaoutamani.

Ukiangalia kwa karibu, unaweza kuhisi kuwa kinachobishaniwa siyo umiliki halisi wa bandari kwani suala hilo limejadiliwa kwa kirefu na kukanushwa mara kadhaa na serikali.

Kinachogomba hapo kwa kuangalia hisia za jumuiya, yaani wadau wanaokuja chini ya mwavuli wa tamko hilo, inadhaniwa ni watendaji na wasimamizi wa bandari, ambao kwa sehemu isiyo ndogo watapanguliwa na wengine wachukue nafasi zao.

Ni vigumu kusema wanahofia mishahara au kuna mengine waliyozoea ambayo yanapunguza ufanisi, kwani urasimu unaponzwa na kupenyeza rupia au pesa.

Uingiliaji huo wa suala la bandari ni kama kuzaliwa upya kwa chombo hicho katika kujaribu kumulika sera za nchi, zisiende mwelekeo wa soko na ubinafsishaji.

Kuthibitisha dhamira hiyo sheria ya uwekezaji ikaongezewa kanuni au sheria mpya, kuwa mgogoro wowote kati ya mwekezaji na serikali utatatuliwa kwa sheria za nchi, katika mahakama za ndani.

Hiyo pia imebidi irekebishwe na serikali ikachagua Mahakama za Afrika Kusini, kuwa na uwezo juu ya masuala kama hayo na DP World inawaelekeza huko hivyo ina uhakika itatendewa haki.

Waliopinga kwa nguvu mkataba huo, wanajihisi wameitingisha serikali kwa kiwango fulani, ila haielekei kuwa serikali iko mbioni kurudi nyuma.

Wakati tamko la kikanisa, linakumbushia lile la Mei 1993, hakuna picha kuwa bandarini Dar es Salaam, kutafanana na suala la umeme mwaka 2004 wakati serikali ya awamu ya tatu ilipoiweka TANESCO chini ya usimamizi wa kampuni ya Net Group Solutions ya Afrika Kusini.

Wakato huo, wafanyakazi walisimama ‘ngangari’ kukataa maofisa wa Net Group wasiingie ofisini, aliyekuwa Waziri wa Kazi wakati huo, akapeleka FFU kutawanya wafanyakazi hao.

Halafu wakapewa fomu ya kujiandikisha endapo mtu anataka aendelee na kazi kwa masharti ya serikali au anapingana na mwajiri. Walisalimu amri.

Kilichoko sasa, kuna mkakati wa kurekebisha kwa kina mashirika ya umma 248 na miradi kadhaa ya kushirikisha sekta binafsi inayoanza kutekelezwa muda wowote mwaka huu wa fedha.

Hizo zikienda vyema na matokeo yakaonekana, hasa kwa upande wa bandari ya Dar es Salaam, huenda wakati huo kutakuwapo lugha au kauli tofauti.