Kiwanda cha pamba Singida chatoa ombi kwa Tanesco

20Aug 2023
Thobias Mwanakatwe
Singida
Nipashe Jumapili
Kiwanda cha pamba Singida chatoa ombi kwa Tanesco

KIWANDA cha Kuchambulia Pamba cha Biosustain (T) Limited kilichopo mjini Singida kimeliomba Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (TANESCO) kuangalia uwezeko wa kuzing'oa nguzo zilizopo kando ya barabara na kuzisogeza kwenye ukuta wa kiwanda ili lipatikane eneo ambalo litakuwa linatumika-

-kuegesha malori yanayopeleka pamba kiwandani hapa.

Meneja wa kiwanda hicho, Salum Halfani Salum ametoa ombi hilo kwa Tanesco kufuatia msongamano mkubwa wa malori yenye shehena ya pamba kandokando ya barabara inayotoka katikatika ya mji kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mandewa Singida hali ambayo imesababisha malalamiko na kero kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo na hivyo kuhatarisha uwezekano wa kutokea ajali.

"Ni kweli barabara hii imekuwa na msongamano wa malori yanayoleta pamba kiwandani kutoka mikoa ya Simiyu,Shinyanga na Tabora, alikuja Mkuu wa Wilaya tukamweleza ili changamoto hii iweze kutatuliwa Tanesco wasogeze nguo za umeme karibu na ukuta wa kiwanda na itapatikana eneo ambalo malori yatakuwa yanapaki na hivyo kuacha kuegeshwa kandokando ya barabara inayoelekea Hospital ya Rufaa," amesema.

Salum amesema njia nyingine inayoweza kusaidia kumaliza changamoto ya msongamano wa malori yaliyosheheni pamba kando ya barabara hiyo ni serikali ingilie kati kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kwa wananchi waliovamia eneo la kiwanda na wengine kujenga makazi wakati hawana hati miliki ya eneo hilo.