Ndugai ahadharisha uagizaji nje mafuta ya kula

20Aug 2023
Ibrahim Joseph
KONGWA
Nipashe Jumapili
Ndugai ahadharisha uagizaji nje mafuta ya kula

SPIKA Mstaafu wa Bunge, Job Ndugai, ameshauri serikali kuangalia suala la uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kwa kuwa linashusha uzalishaji wa alizeti nchini kutokana na kuwapo kwa bei isiyo na tija kwa mkulima.

Job Ndugai.

Akizungumza wilayani hapa kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti kinachomilikiwa na Quickstep Investment Limited kilichofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Ndugai alisema bei ya alizeti na mafuta ya kula kuanzia mwaka jana imekuwa si ya kuvutia kwa wakulima kutokana na kikwazo cha soko na bei katika mnyororo wa thamani.

“Bei inapokuwa ndogo mkulima anapata hasara na analazimika kulima mazao mengine badala ya alizeti. Mwaka jana serikali iliweka kama azimio hivi la kuhakikisha tunajitosheleza kwa mafuta ya kula nchini kwa kutenga mikoa ya Dodoma, Singida na Simiyu kwa kuanzia kama mikoa maalum ya kilimo cha alizeti,” alisema.

Alisema jambo hilo lilipokewa vizuri na wakulima na alizeti ilizalishwa kwa wingi sana lakini ilikumbana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ambao ulishusha bei na kuwavunja moyo wakulima na mwaka huu uzalishaji umepungua.

“Inawezekana uzalishaji kurudi tena na kuvuka pale tulipokuwa endapo bei itakuwa nzuri. Suala la kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ni la kuliangalia sana, rafiki zetu wa TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na wengine wote.

“Hebu jaribuni kujifunga mkanda angalau kwa miaka miwili au mitatu tutafika mahali ambapo tunaweza kabisa kujitegemea kwa mafuta ya kula na zaidi, ardhi tunayo ya kutosha,” alisema na kusisitiza kuwa bei ikiwa nzuri kila mkulima atakwenda shambani kuzalisha alizeti.

Ndugai alisema suala lingine ambalo serikali inapaswa kuzingatia ni mbegu za alizeti ambazo zinahimili vikwazo na kutoa mafuta mengi.

“Mbegu nyingi zilizopo unapata mbegu bora. Mwaka  juzi kama ulilima ukarudia tena mwaka jana, mwaka huu ukilima hupati kitu. Ni mbegu zile ambazo uzalishaji wake unapungua mwaka hadi mwaka.

“Kilimo chetu sasa ni lazima uende dukani kila mwaka ukanunue mbegu. Kwa  hiyo mbegu ni ghali hazipatikani na zingine ni feki. Mkulima  anaingia gharama kubwa, eneo hili la mbegu ni muhimu kuangaliwa sana,” alisema.

Hata hivyo, alisema bidhaa ya mashudu yanayotokana na alizeti bado hayatumiki ipasavyo nchini na yamekuwa yakinunuliwa na kupelekwa Kenya.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kiwanda hicho, Mkurungenzi wa Maendeleo ya Viwanda kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Lugano Wilson, alisema mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ni asilimia 60.

Dk. Wilson alisema serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuwasaidia kutafuta soko la ndani na nje la mafuta ya alizeti yanayozalishwa nchini.

Alisema ili kufanikiwa katika kuanzisha viwanda vingi zaidi hasa maeneo ya vijijini nishati ya umeme inahitajika kufanikisha lengo hilo.

Awali, akitoa salamu za UNIDO, Gerald Runyoro alisema shirika hilo limefadhili mashine hizo za kusafisha mafuta ya alizeti baada ya kuridhishwa na andiko la watu waliojitokeza kuomba.

Runyora alisema mashine hizo zimetengenezwa nchini na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Dodoma kwa thamani ya mashine moja Sh. milioni 17.9, hivyo kwa mashine tatu ni Sh. milioni 53.7.

Aliongeza kuwa mashine hizo mbili zimekwenda kwa wananchi wilaya ya Kongwa na moja itakwenda Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma na itakuwa ikitumika kutoa mafunzo kwa wananchi wengine ili kuongeza thamani ya mafuta yanayotengenezwa nchini na kupata soko la nje ya nchi.