Akizungumza leo Agosti 21, 2023 katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba amesema Tanzania inatekeleza mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa dola hivyo kuendelea kushikilia pesa hizo kuna athari ya kupata hasara badala ya faida.
“Niwaombe (wanaoshikilia dola) mziweke sokoni katika mfumo ulio rasmi. Tutawachukulia hatua za kisheria wale wote watakao bainika kujihusisha na biashara haramu ya soko la fedha (black market),” amesema Tutuba mjini Arusha.
Tutuba amesema Serikali inapata dola za Marekani kupitia utaratibu wa kawaida ukihusisha mikopo, misaada, mauzo ya nje na kwamba kunaongezeko la watalii ambao pia wamekuwa wakichangia katika upatikanaji wa dola.
Kwa mujibu wa Gavana, upungufu wa dola ni tatizo la kiduni lililochangiwa na wachapishaji wa fedha hiyo Marekani, ambayo imeamua kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza usambazaji wa dola sokoni.
Marekani imepanga mpango huo utaendelea hadi Mwakani ili kuongeza thamani ya dola na kupunguza mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma katika taifa hilo kubwa Duniani.










