wilayani Itilima mkoani Simiyu, wakulima waliwasilisha kilio chao kuhusu kushuka kwa bei ya pamba na kuchangia kuendelea kutafunwa na umaskini kauli ambayo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, aliahidi kuzungumza na serikali kuona namna ya kuitatua.
Akijibu swali la wakulima katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Laini, Kinana alisema changamoto hiyo inapaswa kutatuliwa na serikali.
Kinana aliahidi kuliwasilisha ngazi za juu ili kuona namna ya kujenga viwanda vya ndani vya kuchakata zao hilo kwa kutengeneza nyuzi na nguo na kunusuru bei ambayo inashuka kila msimu.
Malalamiko ya wananchi yanalenga zao hilo kuwa na bei elekezi ili kuondokana na changamoto ya kila msimu pamba kuuzwa bei ya chini na hata inapouzwa malipo huwa nusunusu na kushusha thamani yake huku gharama za uzalishaji zikipaa.
Akizungumza na wananchi Kinana alisema: “Jambo hili si la kwenu wakulima ni la serikali na mimi nalichukua kwenda kuonana na wakubwa kuwaambia, wakulima wanalima bei inashuka kwa sababu hakuna viwanda nchini.”
Alisema serikali inapaswa kujitahidi kujenga viwanda vya kuchakata zao hilo ikiwamo kutengeneza nyuzi na nguo ili wakulima wasitegemee soko la nje ya nchi pekee katika kuuza.
Pia, alisema kuendelea kupeleka pamba kwenye soko la nje ya nchi ni wazi kwamba bei ya zao hilo itaendelea kuwa ya chini kwa kuwa wao wanapanga wanunue malighafi hiyo kwa bei ya chini.
“Jibu lingine la bei nzuri ya zao hili kila mkulima anatakiwa kulima kilimo cha kisasa, mfano nimeona Singida kuna mkulima mmoja anapata kilo 1,000 wakati Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliyelima karibia heka moja alipata kilo 500.
“Wewe unayelima hapa kwa utaratibu wako heka moja unapata kilo 150 hamuwezi kufanana kimapato. Sasa ni kazi ya serikali kuwaleta wataalamu wawafundishe wananchi walime kilimo cha kisasa," alisema.
Kinana alisema kutokana na changamoto hiyo anakusudia kuonana na Waziri wa Kilimo ili kuzungumza naye kuhusu kusuasua kwa malipo ya wakulima baada ya kuuza zao hilo.
“Kuendelea kulipwa nusunusu kila wanapouza pamba yao linafanya zao linakosa thamani na kuendelea kuwasumbua wakulima wanaotumia gharama kubwa katika uendeshaji wa zao hili,” alisema Kinana.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marko Mtunga, alisema asilimia 80 ya pamba inayozalishwa inapelekwa nje ya nchi ndiyo maana hakuna bei elekezi inayojulikana.
“Ni vigumu kwa wakulima wanaokwenda shambani mwezi Desemba kufahamu bei na ili tuweze kuwaeleza bei, tunapaswa kuwa na mfuko wa kinga ya bei. Ukiwa na fedha kwenye mfuko bei, ikishuka mfuko unatoa fedha unajazia,” alisema Mtunga.
Hata hivyo, alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua na katika mwaka huu wa fedha, imeanzisha mfuko wa kilimo ambao, moja ya kazi yake ni kudhibiti soko na kuwafanya wakulima kuwa na uhakika.
"Ni ukweli mwaka huu bei imeshuka. Mwaka jana wapo waliouza kwa bei ya Sh. 2,000 kwa kilo moja wakati bei elekezi ikiwa Sh. 1,560 na wakati tunapanga bei hiyo msimu uliopita katika soko la dunia bei zilikuwa kubwa," alisema Mtunga.
Mkulima Eliya Ngenda alitaja changamoto nyingine wanayokutana nayo ni pembejeo.
"Dawa wanazoletewa kwa ajili ya zao hili zimekuwa chini ya kiwango, tunapulizia ndani ya muda mfupi magonjwa kama funza wanaendelea kushambulia mazao," alisema Ngenda.
Mkulima Sagata John alisema: “Serikali imekuwa kimya na chama hakijaja kutoa elimu bei imeshuka na tunapaswa kufanya nini? Wametuacha tukipambana na madalali kila kukicha na hakuna wakutusaidia.”









