Russia yaahidi kuboresha uchumi Afrika

31Jul 2023
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Russia yaahidi kuboresha uchumi Afrika

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali ya Russia imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwamo Tanzania.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa aliyasema hayo baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Russia, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, mkutano huo ulifanyika kwenye kituo cha mikutano na maonyesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Russia.

“Mwelekeo wa mkutano wa leo (juzi) ulikuwa kuona namna gani tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Russia. Wao wametoa mwelekeo wa namna ambavyo wataweza kushirikiana na nchi za Afrika kuboresha uchumi wa kila nchi na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye nchi yetu ambao Rais Vladmir Putin ameuridhia,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Tanzania itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa kutumia rasilimali zake ikiwamo madini, maliasili na kilimo hasa upatikanaji wa mbolea.

“Tumesisitiza pia, matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi wa vijijini ili nao wamudu kutumia nishati mbadala kukuza uchumi wao,” alisema.

Alilitaja eneo lingine kuwa ni kukuza biashara ya mazao baina ya Afrika na Russia  na kwamba yenyewe inaweza kuwa soko la moja kwa moja au kwa kuwatumia marafiki zake.

“Ili kufikia hayo, jitihada za kila nchi kwenye kilimo zimesisitizwa. Tanzania tumeeleza mkakati wa kukuza kilimo ikiwamo umwagiliaji. Pia tunahitaji mbolea, dawa na vitendea kazi ili tufanikiwe kwa kasi zaidi,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao wa Afrika juu ya Mkakati wa Rais Samia wa kutoa elimu bure na vifaa vya kufundishia kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wazazi.

Akifungua mkutano huo, Rais Putin alisema nchi za Afrika zimekuwa na uhusiano mzuri na wa muda mrefu na Russia na kwamba nchi hiyo imekuwa ikiendelea kutoa misaada bila vikwazo kwenye maeneo mbalimbali.

Rais Putin alisema nchi 40 kutoka Afrika zimenufaika na misaada ya kijeshi ikiwamo mafunzo.

“Ukaribu wa uhusiano kati ya Afrika na Russia unazidi kuongezeka. Tunatarajia kufungua balozi zetu kwenye nchi nyingine kama vile Burkina Faso na Equatorial Guinea. Pia tunatarajia kufufua vituo vya utamaduni vya Kirusi. Hivi sasa, vituo kama hivyo vinafanya kazi kwenye nchi nane tu,” alisema.

Kiongozi huyo alisema nchi hiyo itaendelea kutoa misaada kwenye sekta ya kilimo ili kuimarisha upatikanaji wa chakula.

“Jana ndiyo maana nilitoa ahadi ya kuzipatia nafaka nchi sita, tani kati ya 25,000 hadi 50,000 na kwamba zitasafirishwa bure. Nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Zimbabwe, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Eritrea na Somalia,” alisema.

Alisema Russia imepanga kutoa Dola za Marekani milioni 90 kwa nchi za Afrika kulingana na maombi ambayo yamepokewa kutoka Umoja wa Afrika (AU).

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema mwishoni mwa mkutano huo watoke na tamko la kisera ya kwamba mataifa ya nje yanapaswa kununua kutoka Afrika bidhaa zilizosindikwa badala ya mazao ghafi.

“Napendekeza tutoke na tamko la kisera kwa nchi zote kwamba wakija kwetu wanunue chokoleti badala ya kakao, kahawa iliyosindikwa badala ya ghafi na bidhaa za chuma zilizosanifiwa badala ya chuma ghafi,” alisisitiza.

Alisema bara la Afrika linahitaji zaidi kupata teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa mbolea ili liwe na uhakika wa kuzalisha chakula.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alisema umefika wakati wa mataifa mengine kukubali kuwa nchi za Afrika zimeanza kutengeneza hatma yao na kwamba anaunga mkono hoja ya Rais Museveni ya kutouza bidhaa ghafi nje ya nchi zao.

Ili kuhakikisha kuwa maamuzi ya kikao hicho yanafanyiwa kazi kwa haraka, Rais Ramaphosa alipendekeza kuwa ni lazima waandae mpango wa ufuatiliaji na tathmini.

Alitumia fursa hiyo kuwaalika viongozi wenzake washiriki Mkutano Mkuu wa 15 wa BRICS unaotarajiwa kufanyika Afrika Kusini, kwa siku tatu kuanzia Agosti 22, mwaka huu.