Rukwa yaelekea kuandika historia kutokomeza mimba na ndoa za utotoni

20Jul 2023
Zuwena Shame
RUKWA
Nipashe
Rukwa yaelekea kuandika historia kutokomeza mimba na ndoa za utotoni

RUKWA ni miongoni mwa mikoa 10 bora vinara kwa idadi kubwa ya ndoa na mimba za utotoni ikifikia asilimia 40 ikimaanisha kuwa katika mabinti 100 arobaini ni wajawazito, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Watoto Duniani (UNICEF).

waziri wa afya ummy mwalimu.

Shinyanga ni wa kwanza ukiongoza kwa asilimia 59, Tabora 58, Mara 55, Dodoma 51, Lindi 48, mingine inayofuatia ni pamoja na Mbeya 45, Morogoro na Singida 42 wakati Rukwa ni asilimia 40.

Mkoa huo unakadiriwa kuwa na mabinti 77,412 wenye miaka kati ya 15 hadi 19 ambao asilimia 29 ya wasichana hao wameshapata mimba au wana watoto.

Licha ya mahakama kutaka Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 irekebishwe, inalalamikiwa kuwa inamruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi, walezi na miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama, wakati wa kiume anaruhusiwa kuoa akiwa na miaka 18.

Ndiyo sababu watetezi wa haki za watoto wanasema ndoa hizo za utotoni ni ukiukwaji wa haki za msingi ikiwamo usawa, utu na kupata elimu.

Tanzania inaruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo baada ya kujifungua, lakini wasichana bado wanakumbana na changamoto katika kumalizia elimu yao.

Jitihada mbalimbali za wadau likiwamo Shirika la Plan International kupitia mradi wa Tanzania Girl’s Get Equal Integrated, zinadhamiria kuinua wasichana kupata haki ya msingi ya elimu kwa kupinga mimba na ndoa utotoni.

Utafiti unaofanywa na Nipashe kwa kushirikiana na Plan International wilayani Kalambo, Nkasi na Sumbawanga Vijijini Mkoa wa Rukwa hivi karibuni, unaonyesha kuwa mimba na ndoa za utotoni zinapungua.

Utafiti huo unaowahoji maofisa elimu, viongozi wa dini, wahudumu wa afya, wahamasishaji rika na viongozi wa serikali, wasichana na kamati za vijiji mradi unapotekelezwa katika kata 10 kati ya 27, unatoa picha hiyo.

Takwimu mkoani hapo zilibainisha kuwa mwaka 2019 zilikuwa mimba 32 zilizoripotiwa ikielezwa kuwa kwa kiasi kikubwa zilichangiwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi salama kati ya vijana rika.

Sababu nyingine zilizochangia mimba hizo miaka ya nyuma ni umbali mrefu kutoka na kwenda shuleni na kukosa chakula shuleni, aidha mazingira yasiyo salama kwa wanafunzi pia yanatajwa.

Mwaka 2020 Plan International Tanzania ilipotekeleza mradi wa Girls Get Equal Integrated, mkoani Rukwa kwa kushirikiana na wadau kama Youth Employment Through Skills Enhancement (YES), mimba zilipungua hadi 20.

Ni baada ya kuongezeka uelewa kwa walimu shuleni, kuanzisha klabu za masuala afya ya uzazi na vita dhidi ya ndoa za utotoni, kadhalika kuongeza wahamishaji rika kueneza uelewa zaidi kuanzia shuleni hadi nyumbani.

Ofisa Elimu Sekondari Sumbawanga, Fanikio Bitende, anasema kuanzia 2021 hadi 2022, mimba zilishuka hadi saba, baada ya kuongezeka kwa elimu ya uzazi salama, kupinga ndoa na mimba utotoni na huku jamii zikielewa umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na kuwapeleka shuleni.

Aidha, anataja kuwa ni kuanzishwa huduma rafiki za afya ya uzazi na upatikanaji wa taulo za kike shuleni na kupungua utoro hivyo mwaka jana hadi Juni mwaka huu zikaripotiwa mimba mbili ikionyesha ni mafanikio makubwa zaidi.

Aidha, Fanikio Bitende, anataja jitihada za klabu shuleni, jamii na viongozi wa dini, wazazi, walezi na waelimisha rika kuendelea kusambaza na kueneza elimu ya afya ya uzazi salama.

Pia utafiti unabaini kuongezeka kwa ufaulu kwa madarasa ya mitihani ya taifa, kidato cha nne, kama Ofisa Elimu Sekondari anavyosema kuwa mwaka 2019-2020 ulipanda hadi asilimia 80.2, mwaka 2021 hadi mwaka jana ufaulu ulikuwa asilimia 90.

“Hii imechangiwa na kuongezeka kwa uelewa wa umuhimu wa elimu, mazingira salama shuleni na ushirikiano wa mashirika kama Plan International.” Anasema Bitende.

Upande wa shule za msingi, Wilaya ya Sumbawanga pia idadi ya mimba kwa wasichana imepungua ambapo mwaka 2019 zilikuwa nane na kupungua hadi tatu kutoka mwaka 2020-2022 na mwaka huu ni mbili, anaongeza Ofisa Elimu Sekondari.

Anasema mafanikio hayo ni matokeo ya kutoa elimu ya uzazi salama, kupungua utoro na kuboresha vifaa na miundombinu mbalimbali, vilevile kuhusisha wazazi na walezi kupitia Ushirikiano wa Wazazi, Walezi na Walimu (UWAWA) na kamati za vijiji.

Ufaulu kwa darasa la saba na la nne umeongezeka pia kwa miaka ya sasa ijapokuwa kupungua kwa ufaulu mwaka jana kumechangiwa na mrundikano wa wanafunzi madarasani na ukosefu wa walimu wa kutosha, Ofisa Elimu anasema.

Anaongeza kuwa mafanikio ya kupungua kwa mimba na ndoa za utotoni zimechangiwa na ushirikiano mkubwa kati ya serikali na wadau akitaja Plan International, wazazi, walezi viongozi wa dini kwamba ni suala linalohitaji nguvu na jitihada zaidi.

Mtoa huduma rafiki kwa vijana kituo cha afya Nkomoro Wilaya ya Nkasi, Scola Sunga, anataja uwepo wa mwamko kwa vijana wengi kuhusu afya zao na kutumia njia za uzazi wa mpango na kuhimiza kuwekeza katika ustawi wa kumwezesha msichana kuwa na mafanikio zaidi.

Scola anasema ni vyema kuboresha sheria zinazokataza ndoa utotoni, kutoa elimu ya kujamiiana kwa ufasaha, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa vijana.

Mwenyekiti wa klabu ya wazazi kata ya Matai A, Isaac Sawala, anasema maendeleo na ustawi wa jamii yanategemeana na afya, elimu na kumwezesha msichana hivyo ni vyema jamii kushikamana kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ili wawe na maisha yenye mwanga.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika mikoa ya Katavi na Rukwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Amani kwa Viongozi wa Dini Rukwa, Ambele Mwaipopo, anasema imani inafundisha kulinda na kulea vijana na kuitaka jamii nzima kushirikiana kupinga na kuzuia mimba na ndoa za utotoni.

Mwaipopo anaongeza kuwa viongozi wa dini wana jukumu la kuongoza jamii katika haki na hivyo watetee ustawi na kumwezesha msichana kielimu.

Meneja wa mradi wa Girls Get Equal Integrated, Ending Child Early an Forced Marriage Rukwa, Kisasu Sikwalanga, anasema ndoa na mimba hizo zimeendelea kuwa changamoto mkoani Rukwa.

“Hata hivyo jitihada na mipango mbalimbali imeonyesha matokeo chanya katika kupunguza tatizo hilo.”

Sikwalanga anasema jitihada endelevu zinahitajika kuongeza elimu, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kumwezesha msichana kufanya maamuzi sahihi na ushirikiano baina ya wadau katika ngazi za jamii, mkoa na taifa ni muhimu kutokomeza vyanzo vya kiini cha ndoa na mimba utotoni mkoani Rukwa.

Anataja baadhi ya mapendekezo ya utafiti kuwa ni kutetea ujio sheria ya ndoa inayoweka miaka 18 kuwa umri wa kuwa na ndoa kwa jinsia zote, kufanya kazi na taasisi za serikali katika kuendeleza na kutekeleza sera ambazo zinalinda haki za mtoto wa kike na kutoa adhabu kali kwa wanaojihuisha na ndoa za utotoni.

“Pia kufanyike kampeni kubwa ya kutoa elimu katika ngazi za jamii, kimkoa na hata kitaifa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ndoa na mimba za utotoni, vilevile kuwahusisha watu muhimu katika jamii, vijana, watu maarufu na vyombo vya habari kuhamisha ujumbe chanya na mabadiliko ya tabia,” anasema Sikwalanga.