TARSI yajitosa elimu madereva mabasi ya shule

16Jul 2023
Halfani Chusi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
TARSI yajitosa elimu madereva mabasi ya shule

TAASISI ya Mpango wa Usalama Barabarani, (TARSI), imezindua mafunzo ya siku mbili kwa madereva wa mbasi ya wanafunzi yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kupunguza ajali za barabarani.

Mkurugenzi wa TARSI, Maliki balongo akitoa maelezo kwa madereva (hawapo pichani) waliohudhuria kwenye semina ya kuwajengea uwezo wa kujiepusha na ajali za barbarani pamoja na ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi. PICHA: HALFANI CHUSI

Akizungumza wakati wa kuzindua mafunzo hayo, katika hafla iliyofanyika jana Mkoani Dar es Salaam, Wilayani Kinondoni Mkuu wa Wilaya hiyo, Saad Mtambule, amesema mafunzo hayo yataleta tija kwa kuwa eneo lake ni wahaga namba moja wa vitendo hivyo.

Amesema, madereva na walezi hao ndio wanaokaa muda mwingi na watoto kuliko wazazi, hivyo kwao ni rahisi kugundua kama mtoto ana tatizo kwa kumuangalia namna atakavyokuwa anashirikiana na wenzake kipindi chote anapokuwa shule au kwenye gari wakati wa kumchukua na kumrudisha.

"Mtoto mara nyingi utasikia amebakwa na mzazi wake wa kumzaa, amebakwa na mjomba wake ukimpeleka shule utasikia nako amebakwa na mwalimu wake, kwenye nyumba za ibada nako hivyohivyo sasa wakati mwingine unajiuliza hawa watoto wetu wapi watakuwa salama?.

“Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika na kosa la kumfanyia mtoto ukatili, tutachukua hatua kali dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine” ameonya kiongozi huyo

Pia amewataka wananchi kutoa taarifa mapema pale wanapoona ukatili umefanyika, na kushiriki mahakamani kutoa ushahidi pale wanapohitajika, ili mhalifu wa vitendo hicho apatiwe adhabu anayostahili kwa muujibu wa sheria.

Aidha amepongeza taasisi ya TARSI kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka madereva na walezi wakayatumie katika maeneo yao ya kazi ili kuleta tija.

Mkurugenzi wa TARSI, Maliki Barongo, amesema lengo la kuja na programu hiyo ni kuwajengea uwezo madereva na walezi katika suala la malezi na usalama barabarani, akisistiza kuwa lengo lao ni kuifika nchi nzima.

Amesema, mafunzo hayo, yatasaidia madereva hao kupunguza ajali za barabarani pamoja na ukatili wa kijinsia na hatimaye kupelekea watoto kufika salama na kutimiza ndoto zao.

Vilevile amewaomba wadau wengine wajitokeze kuiunga mkono taasisi yao ili kuwezesha kuifikisha elimu ya usalama barabarani nchi nzima.

Mkuu wa Dawati la Elimu ya Usalama Barabarani nchini, kutoka kikosi cha usalama barabarani makao makuu, Michaeli Deleli, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi kwa madereva wa magari ya shule na kuwa chachu ya kupunguza ajali za barabarani.

Mmoja wa madereva, waliohudhuria mafunzo hayo Salum mayanda, kutoka shule ya Green Acre, ameshukuru taasisi hiyo kwa kuwapa mafunzo pamoja na Serikali kuamua kila basi la shule kuwa na walezi wanawake kwa kuwa walijikuta wakati mwingine wakisingiziwa vitendo ambavyo hawajavifanya.

Mlezi Kutoka Shule ya Feza, Malina Mboma, amesema tangu vitendo vya ukatili wa kingono vikithiri, wamekuwa makini na watoto wanapopanda kwenye mabasi ya shule ikiwamo, kuwazuia kubebana.