Mvua ilivyohamishia bomoabomoa kwenye nyumba na mashamba Iringa

11Feb 2016
George Tarimo
Iringa
Nipashe
Mvua ilivyohamishia bomoabomoa kwenye nyumba na mashamba Iringa

MVUA zinazoendelea kunyesha nchini, tayari zimeshasababisha maafa kwa jamii. Hiyo ni pamoja na mazao ya chakula kuharibiwa, nyumba kuvunjwa na baadhi yake paa zimeezuliwa kutokana na upepo mkali.

Wananchi wakivusha usafiri wa pikipiki kwenye mto mapogoro kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Ni jambo linalowalazimu wananchi hao kuhama makazi yao na kwenda kwa majrani. Miongoni mwa wahanga hao ni wanaotoka katika eneo la Mapogoro, katika tarafa ya Idodi, Jimboni Ismani. Mvua hizo zilianza kunyesha Desemba mwaka jana na hata baadhi ya nyumba za ibada kuezuiliwa kwa upepo mkali.

Hivi karibuni Januari 29 mwaka huu, ikiwa ni wiki mbili tu zilizopita, wakazi walikumbwa na janga hilo hata likawasimamisha kuendesha shughuli zinazowapatia kipato na maisha yao na mali zao kuwa hatarini.

Ni tukio lililotokana na mto huo uitwao Mapogoro, kufurika na kukata kingo zake na maji yakaingia katika makazi na mashamba ya wananchi.

Maji hayo yaliyoacha njia yake kutokana mafuriko na kupasua barabara, hivyo ilikata mawasiliano baina ya wananchi wa vijiji vya Mahuninga, Tungamalenga, Kisiriwa na Makifu. Ni athari kubwa iliyokata mawasiliano ya barabara iendayo katika Hifadhi ya Ruaha ambako wananchi wanalazimika kutumia njia mbadala kwenda hifadhini huko.

Hiyo ndiyo hali iliyodumu kwa wiki moja sasa, bado kuna wananchi wanaotaabika, ingawaje kuna ukweli kwamba kuna juhudi za serikali na wananchi zinazoendelea kuhakikisha wanarudisha maji katika mkondo wake. WENYEJI WAONGEA Diwani wa kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo anasema kuwa adha waliyoipata wananchi wake ni kubwa.

Mtafitikolo anasimulia namna alivyopata habari, kwamba wananchi walimpigia simu kumueleza “maji yamejaa na yamepasua barabara haipitiki.”

Anaongeza kuwa:”Nilifika eneo la tukio na nikashuhudia maji yamepasua kingo za mto na kuacha kuingilia kwenye mkondo wake na kupasua sehemu nyingine ambapo maji hayo yaliingia mashambani mwa watu na kuharibu mazao ya mahindi na maharage.”

Mtatifikolo anakiri kuwapo mvua nyingi zinazoeendelea kunyesha, lakini anakana chanzo cha mafuriko hayo kuwa siyo mvua tu, bali na wananchi wanaolima kwenye vyanzo vya maji.

Ofisa Tarafa wa Idodi, Yakob Kiwanga, anasema madhara makubwa yanaanzia katika vijiji anavyovitaja kuwa ni; Tungamalenga, Mahuninga, Kisiriwa na Makifu ambao hawana mawasiliano kwa sababu hakuna mtu anayevuka kwenda upande wa pili.

Anasema kuwa licha ya kukata mawasiliano hayo, bado kuna changamoto kubwa iliyosababisha mazao ya wananchi shambani kuzolewa na maji na nyumba zao kujaa maji.

Yuditha Msovela, ni miongoni mwa wananchi waathirika waliolazimika kuhama makazi kukimbia mafuriko na sasa amehifadhiwa na jirani anasema. Anasimuilia mkasa ulivyowakumba akitamka kuwa: “Juzi majira ya saa nane usiku, nimelazimika kuhama nyumba yangu ambapo maji yalipasua ukuta na kuingia ndani.
“Nilitoka kuomba msaada kwa majirani, lakini maji hayo yalishindikana huku yakichukua mazao yangu, chakula pamoja na wanyama na hadi sasa ninaishi kwa majirani.” Anaongeza:“Hata kama mvua zikiacha kunyesha na maji yakapungua, siwezi kurudi tena katika nyumba yangu kwa sababu nahofia usalama wa maisha yangu.”

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Iringa, Mhandisi Daniel Kindole, ambaye ameweka kambi katika eneo la tukio, anasema siku zote hadi sasa operesheni maalum iliyowaweka mahali hapo ni kurudisha mawasiliano na kujenga daraja la kudumu. Mhandisi Kindole anasema kuwa tatizo kubwa lililoleta majanga yote ni mto kukata kingo zake na kufanya maji yatawanyike bila ya mwelekeo maalum. KAULI YA SERIKALI Mkuu wa wilaya ya Iringa,
Richard Kasesela, anakiri kusuhudia majanga yaliyowakuta wananchi na kusimamia kwa karibu hatua zinazochkuliwa kurejesha hali ya kawaida.

Anasema kuwa,wamekubaliana kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa haraka, ikiwemo Tanroads inamtafuta mkandarasi kwa haraka barabara zilizoharibika, kwa kusaidiana na wananchi.

Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa iliitisha kikao cha dharura cha wananchi kwa lengo la kutathmini namna ya kuwezesha maji yanarudi katika mkondo wake wa kudumu.

Wananchi waliazimia kujitokeza kwa wingi wakiwa na nyenzo mbalimbalika vile sepeto na panga, ili kujaza viroba zaidi ya 600 zenye udongo ili kwenye kingo za mtoili kuyarudisha maji, wakati Tanroads wakitengeneza daraja la kudumu.

Kasesela anasema, baada ya kutokea mafuriko hayo katika Kata ya Idodi, katika kijiji cha Mapogoro, kitongoji cha Kitanewa katika tarafa hiyo ya Idodi, kaya zaidi ya 80 zipo hatarini kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Ofisa Tarafa Kiwanga anaongeza kuwa, tayari serikali imeshatenga eneo jipya la wananchi na kuanza kuwahamisha, huku juhudi zikifanyika kuurudisha mto kwenye mkondo wake wa asili.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Faustino Luhova, anasema viongozi wa serikali na wananchi wamejitokeza kusaidia kuurudisha mto katika hali yake ya kawaida na wananchi, walishaanza kujaza vifusi kwenye viroba kukabnlisha kazi hiyo. Hata hivyo baadhi ya wananchi ambao ndio wahanga wa mafuriko hayo, wanasema kuwa hawana pingamizi lolote la kuondoka eneo hilo, kwani hali yao sasa ni mbaya na hawawezi kuendelea kukaa kwenye eneo hilo hatarishi.
Elimala Mbiiji ambaye ni mkazi wa kitanewa Mapogoro, anasema hawezi kung'ang'ania kuishi eneo hilo, kwani hata maji yakipungua, anakiri kuwa hali hiyo si salama tena.

Mkuu wa Wilaya –Kasesela, akishirikiana na wananchi kuurudisha Mto Mapogoro katika mkondo wake, anasema serikali wilayani Iringa inaendelea kufanya tathimini ya hasara iliyotokana na mafuriko hayo.

Pia, anakiri kwamba hali bado ni tete katika eneo hilo na ni vyema wakazi wakahamisha familia zao kwenda sehemu za mbali.

Kasesela anasema, katika suala la mazao,a anmuagiza Ofisa Tarafa kupeleka taarifa kwa Mwenyekiti wa Maafa wa Wilaya katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ili tathimini ya mazao na nyumba ifanyike.

Janga linalotokea katika Tarafa ya Idodi ni mfano tu wa kinachojiri kwigineko nchini, ikiwemo wilayani Kilosa ambako mafuriko yameshasabanisha majanga kama hayo ya mkoani Iringa na maelfu ya wakazi wake wakikosa makazi, kutokana na mafuriko kukumba nyumba zao.