JANGA LA SARATANI:Sumu yake imejificha kwenye sigara na pombe

11Feb 2016
WAANDISHI WETU
DAR
Nipashe
JANGA LA SARATANI:Sumu yake imejificha kwenye sigara na pombe

TAKWIMU za Sensa ya Watu na Makazi za mwaka 2012 inaeleza kuwa Tanzania ina watu milioni 44.9.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Hamisi Kigwangalla.

Katika idadi hiyo ya sense, takwimu za kiafya za serikali nchini zinaonyesha watu 100 kati ya 100,000 hugundulika kila mwaka kuwa ni waathirika wa saratani.

Huo ni wastani sana na asilimia 0.1 ya Watanzania ndio wana saratani. Kwa wastani mpana, idadi ya wanaogundulika kuwa na maradhi hayo kitaifa ni watu 44,000.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Jamii Jinsia Watoto na Wazee, Dk. Mpoki Ulisubisya, anasema hiyo ni sawa na asilimia 10 ya wagonjwa wote wanaofanikiwa kufika katika vituo vya afya kupata matibabu.

Pia anasema katika orodha hiyo, asilimia 80 ya wagonjwa hufika hospitalini wakiwa hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linalochangia wengi kushindwa kupona.

Pamoja na changamoto hiyo, anasema bado Tanzania ina kituo kimoja tu kinachotoa tiba ya saratani kwa mionzi, ambacho ni Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam.

Anataja baadhi ya vipimo ni vinavyotumika kwa aina tofauti za saratani, kama vile koo na shingo ya kizazi.

Pia anasema kuwa, kuna kipimo kingine kinachotumika kuchunguza tezi dume kwa wanaume.

Katibu Mkuu anatahadharisha kuwa changamoto hiyo isipoangaliwa kwa makini na serikali, itakuwa kubwa kuliko inavyodhaniwa, ikizingatiwa taasisi hiyo ina mashine tatu tu za kutola huduma, hali isiyolingana na idadi ya wagonjwa waliopo sasa.

Ulisubisya anaongeza kuwa, hadi sasa hakuna bei elekezi za vipimo vya saratani katika hospitali za umma na gharama zake ni kati ya Sh. 60,000 na Sh.120, 000.

UKUBWA WA TATIZO

Anasema, ni vigumu kukadiria ongezeko la wagonjwa wa saratani nchini, kutokana na wanaojitokeza kufika hospitalini kufanyiwa uchunguzi ni wachache kulingana na kasi iliyoko.

Katibu Mkuu huyo anaasema kuwa, licha ya saratani kuwaathiri watu wa rika lote, lakini kasi kubwa imeegemea kwa wazee kuanzia wenye miaka 65, huku akitaja miongoni mwa sababu kuu ni uvutaji sigara na matumizi ya pombe kupindukia.

Kwa mujibu wa Dk. Ulisubisya, wanaopoteza maisha kila mwaka duniani ni asilimia 13 ya wagonjwa wote, miongoni mwa vigezo vinavyolalamikiwa ni kuchelewa kufika katika vituo vya afya kwa wakati.

Anatahadharisha kuwa, iwapo hatua madhubuti za kinga na uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, kasi ya saratani itaongezeka na kufika wagonjwa wapya milioni 24 ifikapo 2035 duniani, huku Tanzania ikiwa kinara.

Anasema takwimu za Shirika la Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani(IARC), na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kila mwaka duniani wagonjwa wapya wa saratani waafika milioni 14.1, kati yao zaidi wagonjwa milioni 8.2 wanapoteza maisha.

HATUA ZA SERIKALI

Anasema ili kukabiliana na ongezeko hilo, serikali imeandaa mwongozo utakaotumika nchini kuhawamasisha raia wake kupima afya zao mapema, ili kupata matibabu kawa wakati.

“Pia vinasaba vya mwilini, lishe, unene usio wa kawaida, matatizo ya tumbo na tatizo sugu la kucheua tindikali, ni miongoni mwa visababishi vya saratani kwa mujibu wa madaktari bingwa,” anasema.

Anasema serikali katika mwongozo wa serikali, imeandaa majengo maalumu katika hospitali kubwa za rufaa kama vile Bugando, KCMC na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambavyo vitasambaziwa vifaa maalumu vya kuihudumia umma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselege, anasema takwimu za wagonjwa hao inayonyesha aina ya saratani zinazoongoza kwa wanaume ni ya Ngozi, Koo, Tezi Dume na Tezi, wakati kwa wanawake ni ya Shingo ya Kizazi, Ngozi, Matiti na Koo.

Anataja takwimu za dunia, kwamba watu miloni nane hufariki duniani kwa maradhi hayo, ilhali nchini wanafariki kati ya watu 1,000 na 1,200.

MAAMBUKIZI

Vyanzo vingine kwa mujibu wa Dk. Mwaiselege ni pamoja na maambukizi kupitia virusi, bakteria na parasaiti.

Aidha anataja katika orodha hiyo imo mtindo wa maisha, mionzi, urithi wa kifamilia katika na vyanzo vizivyojulikana.

Katika hilo, anafafanua mlo una mchango wake katika kusambaza magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo saratani ni sehemu yake.

Baadahi ya vyakula hivyo vinavvyitajwa ni mafuta hasa ya wanyama, samaki, huku tabia ya kuendekeza uzito wa mwili uliokithiri nao unaingia katika kundi hilo la zao la mlo.

Pia, anataja mwili kutofanya mazoezi, uvutaji sigara na bidhaa za starehe kama vile tumbaku na pombe kwa wingi.

“Ili kuzuia ugonjwa wa saratani na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza, ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema, unasaidia kuzuia mtu kupata maradhi hayo,” anaongeza Dk. Mwaiselege.

Aidha, anatumia fursa hiyo kuwashauri watu kuchunguzwa afya zao dhidi ya maardhi kila fursa inapotolewa bure.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaiselege, saratani ni kundi la magonjwa yanayosababishwa na mgawanyiko usio sawa na usiothibitika wa seli na kuunda uvimbe unaovamia na kudhuru tishu (mishipa laini).

MAKUNDI NA INAVYOSAMBAA

Anafafanua kuwa, kuna aina zaidi ya 100 za saratani kulingana na aina ya kiungo kilichoathirika mwilini.

Mkurugenzi huyo anasema, katika aina zote hizo, kuna sifa tatu kuu tatu zinazofanana ambazo ni; Ukuaji usiothibitika wa seli; Uwezo wa kuvamia na kushambulia ‘tishu’ nyingine na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine kupitia mishipa ya damu au mikondo mingine ya mfumo wa mwili.

Anaeleza kuwa, saratani isiyotibiwa inaweza kuwa ugonjwa unaoshambulia tishu nyingine za mwilini na kusabisha kuisambaa kwake hadi kifo kwa mgonjwa.

Dk. Mwaiselege anasema, saratani inasababisha mwili kuwa na madhara pale inapoharibu chembea hai na kuzifanya zigawanyike bila kudhibitika.

Anasema kuwa uvimbe wa tishu unaojulikana kitaalam kama ‘tumor’ (isipokuwa katika saratani ya damu) huzuia utendaji wa kawaida wa damu kwa kuzifanya chembe hai kuwa na mgawanyiko usio wa kawaida katika damu.

Anasema mwili wa binadamu umeundwa na idadi isiyohesabika ya chembehai,
hivyo mwenendo huo unaratibiwa vyema na kusimamiwa na vinasaba au DNA vilivyo ndani yake.

SARATANI INAPOANZIA

Mkurugenzi huyo wa taasiso ya saratani anasema kuwa wakati mtu anapokuwa mtoto tumboni mwa mama yake, chembehai zake hugawanyika kwa haraka na kumfanya akue.

Baada ya mtu kukua, chembe hai hizo hugawanyika kwa ajili ya kuchukua nafasi ya zile zilizozeeka na kufa au kwa ajili ya kukarabati majeraha.

Anasema,saratani huanza wakati sehemu mojawapo ya mwili zinapoanza kukua bila kudhibitiwa na ukuaji wa seli ya saratani hutofautiana na ule wa kawaida.

Mtaalamu huyo anasimulia kuwa, mwenendo wa ukuaji huo uinakuwa wa kasi na badala ya kufa pale zinapozeeka, zenyewe zinaendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida.

Dk. Mwaiselege anasema chembehai hizo za satarani hushambulia kwa kuingia ndani ya tishu nyingine, jambo ambalo halishuhudiwi katika zingime za kawaida.

Mkurugenzi huyo wa Tasisi ya Saratani ya Ocean Road, anasema kuwa kukua kusikodhibitiwa na kwa namna isiyo ya kawaida kwa chembehai na tabia ya kuzishambulia tishu nyinginezo, huzaa chembehai ya saratani.

BALAA LA TUMBAKU

Katika kupambana na ongezeko hilo, wadau nchini wanaitaka serikali kuweka sheria na sera madhubuti za kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini.

Watumiaji wa bidhaa hiyo wanaeleza kilio chao kwamba, licha ya kuwa zao la biashara linaloingiza taifa pato kubwa, lakini katika medani ya dunia, kuna watu milioni sita wanaokufa kila mwaka kwa kuvutishwa sigara kupitia moshi wake kutoka kwa wavutaji wengine katika maeneo ya wazi.

Mkurugenzi wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (UICC), Lutgard Kagaruki, anataoa rai kwa serikali kuwa umefika wakati wa kodi na bei ya tumbaku nchini kuongezwa.

Anasema kuwa hiyo itasaidia kupunguza ushawishi kwa vijana watumia tumbaku, kundi linaloathirika kasi zaidi mna matumii ya tumbaku.

Kagaruki anasema kila mwaka serikali hutumia fedha Dola za Marekani milioni 4 sawa na Sh. bilioni 8.7 kupambana na ugonjwa wa saratani.

Anasema kiwango cha asilimia 32 ya bajeti tajwa (Sh. bilioni 2.18) mzizi waje uko katika matumizi ya tumbaku.

“Wavutaji sigara wapo katika hatari zaidi kupata saratani, hasa vijana na kwa sasa huchochewa na uingizwaji wa tumbaku aina ya shisha na sigara za umeme katika kumbi za starehe,” anasema Kagaruki.

Anasema, changamoto iko katika kilimo cha tumbaku kinachoongezeka nchini na kuwaathiri wakulima, wakausha tumbaku na anawashauri wakulima kupatiwa kilimo mbadala, ili waepuke matatizo yanayowakabilia.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Satarani yana kaulimbiu ya ‘Tunaweza, Naweza.’

Mantiki yake ni kuhamasisha jamii kwa sasa ni kupambana na ugonjwa wa saratani kwa ushirikiano wa pamoja.

Imeandikwa na Efracia Massawe na Christina Mwakangale

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: +255 753 390772 au barua pepe: efraciajoseph@yahoo.com