Inakadiriwa kuwa msichana mmoja kati ya wasichana 10 barani Afrika, hukosa masomo shuleni wakati wanapokuwa katika kipindi cha hedhi. Kwa mujibu wa utafiti Umoja wa Mataifa (UN).
Nchini pia kati ya siku tatu hadi saba, msichana hushindwa kuhudhuria masomo kutokana na kuwa kwenye siku za hedhi, kila mwezi.
Katika kukabiliana na hilo, klabu maalum la kuelimisha vijana kuhusu hedhi salama ‘Hedhi Huru Club’, imezinduliwa katika shule ya sekondari Hocet, iliyopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani kwa lengo la kuwa kitovu cha utoaji elimu kuhusu hedhi.
Uzinduzi huo, umeenda pamoja na ugawaji wa taulo za kike 125, pia vihifadhia taka ‘dustbin’ viwili na wasichana wamepewa ‘period trackers’ za kuwasaidia kufuatilia mwenendo wa siku zao.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Hinatas Foundation imekabidhi msaada huo, mwishoni mwa wiki hii, mkoani hapa, ikiwa ni sehemu ya kujitolea kwa jamii, kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama duniani inayofanyika kila mwaka ifikapo Mei 28.
.jpg)
Mkurugenzi Mkuu wa Hinatas Foundation, Ayshat Sanya, anasema bado jamii haina uelewa kuhusu hedhi salama hususan mashuleni.
“Msichana akiingia siku zake kuna ambao hawana uwezo kununua taulo za kike za,jisitiri. Wengi wanatumia zile za kutumika na kufua. Inapotokea bahati mbaya akachafuka nguo, huchekwa hasa na jinsi ya kiume,” anasema.
Mkurugenzi huyo anabainisha kwamba: “Tunatambua changamoto hii na ndiyo sababu tangu mwaka jana tulianza kusherehekea Siku ya Hedhi Salama, tuliitembelea shule ya sekondari Kinyamwezi na kugawa taulo za kike.
Anasema mwaka huu ni zamu ya shule ya Hocet kwa kuwapatia taulo za kike 125 na kutengenezwa kalenda maalum ‘period trackers’, msichana ataweza kuitumia kufuatilia mwenendo wa siku zake.
Amesema hatua hiyo itamsaidia kujua lini ataingia katika siku zake hivyo kujiandaa mapema, hivyo atakuwa ameepuka kuchafuka nguo yake mbele za watu.
“Period tracker, itawasaidia pia kufuatilia hali zao za kiafya, kwa sababu kuna sehemu ya kuandika notisi. Kwa mfano labda alihisi maumivu ya tumbo kupita kiasi, ikiwa atapelekwa hospitali ataweza kujieleza vizuri na kupatiwa huduma,” amesema.
Mlezi wa Hinatas Foundation, Veronica Mrema akizindua ‘Hedhi Huru Club’ anasema lengo ni kuendelea kuwezesha elimu kuhusu hedhi salama kwa wasichana na wavulana pamoja na upatikanaji wa taulo za kike.

“Takwimu za Wizara ya Afya, zinaonesha ni asilimia 28 tu ya wasichana nchini wana uelewa thabiti kuhusu hedhi salama, lakini pia kuna kundi kubwa la wasichana ambalo hukosa masomo kwa sababu ya kipindi cha hedhi,” anaeleza.
Ameongeza “Hivyo, tunahitaji kuendelea kuwapa elimu wadogo zetu wa kike wajitambue lakini pia wa kiume nao hatuwezi kuwaacha nyuma wa kiume kwa sababu wakipata elimu sahihi.
“Wataacha kuwacheka wasichana pale wanapochafuka na hivyo tutaondosha unyanyapaa, tunaamini hatua hii itasaidia kuchochea maendeleo ya ki-elimu kwa msichana.”
Veronica amesema kupitia klabu hiyo wataendelea pia kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kuhifadhia taka kwa ushirikiano na wadau wa Hinatas Foundation ambao kwa sehemu kubwa ni jamii.
“Pamoja na taulo za kike tunazokabidhi leo, tumeleta pia sabuni kusaidia katika suala zima la usafi, pia tumekuja na nguo za ndani, tutaendelea kuwashika mkono na tunazindua klabu na itakuwa chini ya mwalimu ambaye atakuwa ndiye mlezi wenu pamoja na sisi Hinatas Foundation,” amebainisha.
Hinatas Foundation huadhimisha siku ya Hedhi Salama Duniani kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), huku Dk. Happiness Mbeyela akiwahimiza wasichana kuzingatia usafi.
“Hedhi ni suala la ki-afya kwa msichana/mwanamke, ni hatua muhimu katika ukuaji na afya ya uzazi kwa ujumla wake, ni kiashiria kwamba sasa mtoto wa kike amekua na ana uwezo wa kuzaa.
“Wavulana msiwacheke wasichana wanapochafuka, si jambo la aibu ni hali ya kawaida mwanamke kuingia katika siku zake,” amesema.
“Unaweza kumuona msichana yupo kwenye hali ya maumivu, msaidie… kamueleza, msaada ama wa dawa za kutuliza maumivu au hata kumpeleka hospitalini pale inapobidi kwani wapo ambao hupitia maumivu makali hasa ya tumbo,” amesema daktari huyo.
Wanafunzi wa shule hiyo, wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema wameupokea kwa furaha msaada waliopatiwa pamoja na uzinduzi wa klabu hiyo ambapo wao ndiyo wanakuwa mabalozi.
“Ni fursa nzuri kwetu kujifunza zaidi, tumefurahi pia leo mmetupatia na elimu kuhusu afya ya aakil,” amesema mmoja wao.
Mkuu wa Shule ya Hocet, Francis Mlay ameshukuru uongozi wa Hinatas Foundation na MEWATA kwa msaada waliotoa kwa wanafunzi hao, pamoja na kuzindua Klabu ya Hedhi Huru.
“Shule hii ina wanafunzi makundi aina tatu, kuna walio yatima, kuna ambao wazazi wao wana hali duni ya maisha na waliotelekezwa na familia zao, hapa wanapata elimu bila kulipia gharama yoyote.
“Hatuna mfadhili yeyote hivyo msaada wetu mkubwa ni jamii na tuna wanafunzi 157 hadi sasa kila darasa lina wanafunzi 40, kuja kwenu hapa leo tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki sana,” amesema Mlay.










