Kamati ya usajili pamoja na Mkuu wa Skauti Mels Daalder, tayari wameingia msituni kwa ajili ya kusaka nyota wapya kwa ajili ya kuboresha kikosi cha msimu ujao wa mashindano ikiwamo michuano ya 'Super League' inayotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.
Akizungumza na Nipashe jana, Robertinho alisema anahitaji kuimarisha kikosi chake katika usajili kwa kila nafasi kuwe na wachezaji wawili au zaidi wenye ubora na kiwango kizuri.
“Msimu huu tumeshindwa kufikia malengo kwa sababu ya kukosekana kwa nyota wa kikosi cha kwanza kuumia na kushindwa kupata mbadala wao wenye uwiano mzuri na yule tuliyemkosa, tayari nimewasilisha ripoti na mapendekezo yangu, sasa ni muda wa kuandaa timu nzuri na imara kuhakikisha tunafanya usajili mkubwa kulingana na malengo yetu tuliyojiwekea,” alisema Robertinho.
Aliongeza kuwa wanahitaji kubadilisha fikra za wachezaji na mipango yao kwa ajili ya msimu ujao ambao wamepania kurejesha makali yao.
Miongoni mwa majina yaliyopendekezwa, gazeti hili lilinasa jina la kipa wa Vipers FC ya Uganda, Alfred Mudekereza ametajwa kuwa katika mipango ya kocha Robertinho kwa msimu ujao.
Kipa huyo namba moja wa Vipers United ameonyesha kiwango kizuri katika michuano ya kimataifa na kupendekezwa kuwa miongoni mwa nyota watakaosajiliwa kwa msimu ujao wa mashindano.
Chanzo cha ndani kimesema kuwa Robertinho amewataka viongozi kuhusu suala la kipa walifanyie kazi mapema ili kuziba nafasi ya Beno Kakolanya ambaye taarifa zinasema nyota huyo atatimka Simba.










